MHE. MORRIS J. MAKOI aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Barabara ya Mbokomu - Mti Mrefu kilometa 13.94 kwa kiwango cha lami ili kuchochea utalii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Morris Joseph Makoi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Barabara ya Mbokomu – Mti Mrefu katika Wilaya ya Moshi. Katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali ilitenga bajeti ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami nzito (asphalt concrete) mita 200 na tayari zimekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imetenga bajeti ya shilingi milioni 225 kwa ajili ya ujenzi ya barabara hiyo kwa urefu wa meta 200.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mahitaji makubwa ya matengenezo ya barabara kiwango cha lami, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa awamu, ahsante.