Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mwanaenzi Hassan Suluhu (1 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni katika Mkutano wa Pili na Mkutano wa Tatu wa Bunge
MHE. MWANAENZI HASSAN SULUHU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi kuweza kuchangia taarifa iliyowasilishwa na Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati kwa uwasilishaji mzuri alioutoa, na pia niipongeze Kamati kwa maoni na mapendekezo yaliyotolewa katika kuchambua sheria hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kada ya sheria ni kada muhimu sana katika Taifa letu, kada hii ndiyo inaenda kuamua maendeleo na lile tabasamu alilolikusudia Mheshimiwa Rais kuliwasilisha kwa wananchi. Sheria Ndogo ni miongoni mwa sheria ambazo zinapaswa kuzingatia misingi ya uandishi wa kisheria ikiwemo usahihi, uwazi, ufanisi na uthabiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, masharti haya yasipozingatiwa, basi sheria ndogo hizi zitashindwa kutekelezeka. Katika uchambuzi, Kamati ya Sheria Ndogo wakati sheria hizi zilivyowasilishwa Mezani, tumekuta changamoto mbalimbali ikiwemo ya kukinzana kwa sheria, yaani kanuni inaenda kukinzana na sheria mama.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linazorotesha kutekelezeka kwa kanuni zile kwa sababu masharti hayajazingatiwa kwenye sheria mama. Kwa mfano, GN namba tisa Kanuni ya 24 imekuja kutoa adhabu ambayo tayari katika sheria ya mama imeshawekwa. Kwa mfano, ndani ya Sheria ya Leseni ya Usafirishaji Kifungu cha 36 kimekuja kuweka masharti ya kuzingatia wakati mwombaji wa leseni akienda kinyume na masharti hayo adhabu yake ni nini? Sasa Kanuni ikaja ikaweka tena masharti yale, jambo ambalo linaenda kukinzana na sheria mama na hivyo kupelekea sasa sheria ile kutokutekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kada hii iweze kufikia malengo, nitoe rai kwa wale wote wanaopewa mamlaka ya kutunga sheria hizi, basi wazingatie miongozo na masharti ya utungaji wa sheria ili ziendane na sheria mama na ziweze kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, ninaunga mkono hoja na niwaombe Waheshimiwa Wabunge waweze kuipitisha taarifa hii ili iende kutekelezeka, ahsante. (Makofi)