Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Benjamin Lukubha Ngayiwa (2 total)

MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuipandisha hadhi Hospitali ya Manispaa ya Kahama kuwa Hospitali ya Rufaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kufanya maboresho katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, ikiwa ni pamoja na kuwezesha utolewaji wa huduma za kibingwa. Huduma za kibingwa zinazotolewa ni pamoja na huduma za magonjwa ya ndani (internal medicine), matibabu ya mifupa, magonjwa ya uzazi, magonjwa ya macho, pamoja na huduma za uchunguzi wa mionzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Kahama Manispaa ina upungufu wa miundombinu muhimu ikiwemo jengo la huduma za dharura, jengo la huduma za wagonjwa mahututi na baadhi ya vifaa vya huduma za uchunguzi. Serikali itaendelea kutenga fedha, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu muhimu katika hospitali hiyo kisha kufuata Miongozo ya Wizara ya Afya kupandisha hadhi kuwa hospitali ya hadhi ya mkoa.
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa chujio la maji la Buzwagi na tenki la maji la Shunu/Lugela ili kupunguza kero ya kukatika kwa maji Kahama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Benjamin Lukubha Ngayiwa, Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi inaendelea na mradi wa ujenzi wa mtambo wa kutibu na kusafisha maji (treatment plant) katika eneo la Buzwagi Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga. Utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa 79% na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2026.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji Lugela unaojumuisha ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 75,000 katika eneo la Lugela Kata ya Nyahanga wilayani humo. Kazi nyingine zinazotekelezwa ni pamoja na ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa tisa ambapo umeanza kutoa huduma kwenye baadhi ya maeneo ya Lugela.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa mradi huo umefikia wastani wa 78% za utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Juni, 2026 na kunufaisha wananchi wapatao 2,682 wanaoishi katika eneo la Lugela.