Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Fadhili Fabian Ngajilo (4 total)

MHE. FADHILI F. NGAJILO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kupewa nafasi hii kuuliza swali la nyongeza. Mkoa wa Iringa unasemekana una maeneo yenye madini. Ukienda mfano Ihomasa, Ihandutwa, Sinai, Ulata, Mtera, Kitonga, Image na maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa. Swali, je, ni lini sasa Serikali wataifungua na kuipa kipaumbele Iringa ili mkoa huu ujulikane ni mkoa wa madini kwa kufanya mining survey lakini kutangaza maeneo yenye madini na kuwawezesha vijana kwa teknolojia ya kuchimba madini na kutengeneza mabilionea kutoka mkoa wa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri na nimjulishe tu kwamba Iringa nayo ni mikoa yetu ya kimadini, wana madini ya aina mbalimbali na nimpe ushauri kwamba atembelee Kituo chetu cha Jiolojia (TGC) pale GST kwa sababu kuna kitabu ambacho huwa kinahuishwa kila baada ya miaka mitatu, kinachoeleza madini yanayopatikana katika kila eneo la nchi yetu ikiwepo Mkoa wa Iringa.

Mheshimiwa Spika, hatuishii hapo tu, tuna wachimbaji wadogo wengi pale Iringa, eneo la Nyakavangala ambalo lipo katika Jimbo la Mheshimiwa Lukuvi, tayari ambako kuna wachimbaji wa dhahabu na madini ujenzi. Hivyo ni wajibu wetu kama Wizara kuendelea kutoa elimu kwa vijana ili waingie katika sekta hii kwa wingi, kwa sababu madini haya yanaenda kubadilisha sura ya uchumi wa wananchi wetu na vijana hasa ambao wanahitaji ajira.

Mheshimiwa Spika, kwa suala la survey, sisi kama Wizara ya Madini kwa maelekezo ya Rais tuko katika mchakato wa mwisho wa kununua ndege yetu wenyewe ya kufanya survey, lakini pia tuna wadau wa sekta binafsi ambao wameanza kurusha ndege, wameanza kurusha helikopta, wameanza pia kurusha na zile ndege nyuki katika kutafuta madini yalipo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Tumeshafanya hivyo Shinyanga, wiki iliyopita na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. FADHILI F. NGAJILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi linahusu skimu za umwagiliaji. Pale Iringa Mjini kuna skimu ya umwagiliaji ya wenyeji inayojulikana kwa jina la Mkoga Chelahani inapatikana Kata ya Isakalilo. Hii skimu imeajiri watu wengi sana zaidi ya 10,000 ambao wanaitegemea. Sasa swali, je, Serikali iko tayari kuijenga upya, kuiboresha ili iweze kutoa ajira zaidi kwa wananchi wa Iringa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Vilevile ninamshukuru Mbunge wa Iringa Mjini, Bwana Fadhili Ngajilo na nimwondoe shaka tu, aende akawathibitishie tu wananchi wa Jimbo la Iringa Mjini kwamba, Serikali tuko tayari kufanya ukarabati na kuboresha skimu hiyo ili kuhakikisha kwamba inaleta tija kwa wananchi wale.
MHE. FADHILI F. NGAJILO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kwa sababu, daraja hilo, wananchi wamekuwa wakiahidiwa muda mrefu zaidi ya miaka 20 iliyopita na sasa Serikali imetoa kauli yake. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, moja, nataka kujua, na wananchi wa Iringa Mjini wanataka kufahamu vizuri, ni lini hasa sasa mradi huu utaenda kukamilishwa na fedha zitatoka?

Mheshimiwa Spika, pili, wananchi wanataka kujua je, mradi huu utatekelezwa kama full package? Kwamba, daraja la mita 40 pamoja na kipande cha lami cha kilomita tatu, kama alivyopendekeza msanifu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, kwenye huu Mradi wa TACTIC, Awamu ya Pili, ndani ya Manispaa ya Iringa Mjini, Serikali haina tatizo la fedha. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan ametenga shilingi bilioni 20, kwa ajili ya huu Mradi wa TACTIC.

Mheshimiwa Spika, mradi huu tunautekeleza kwa awamu mbili, kama nilivyoeleza. Tayari tumeshaanza awamu ya kwanza kwa kujenga Soko la Kihesa, kujenga barabara za Mkimbizi – Bima, Mtwivila, Viziwi na Bontank.

Mheshimiwa Spika, awamu ya pili ndiyo ujenzi wa daraja hili, pamoja na barabara za maingilio kwenye daraja hilo. Siyo hivyo tu, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Mradi wa RISE kwenye hii Manispaa ya Iringa Mjini anajenga barabara kwa kiwango cha lami, kilomita 37, kutoka Ipogolo kwenda Kilolo. Mradi huu tunautekeleza kwa pamoja na wenzetu wa TANROADS.
MHE. FADHILI F. NGAJILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kutujengea soko hili la Machinga Complex ndani ya Iringa Manispaa. Kwa kweli jambo hilo litakuwa limefurahisha sana wananchi wa Iringa Mjini na tupo tayari kutoa ushirikiano kwa ajili ya ujenzi wa hilo soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana na mimi pia kwamba masoko ya namna hii, sehemu nyingi za nchi yetu yakijengwa huwa yanatelekezwa na machinga wenyewe au wafanyabiashara kwa sababu wanakuwa hawakushirikishwa wakati wa ujenzi, na usipomshirikisha mfanyabiashara maana yake atashidwa kujua afanye nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, je, Wizara inanihakikishiaje kwamba kabla ujenzi huu wa hili soko itawashirikisha wadau wakubwa wa ujenzi ambao ni machinga wenyewe wa Iringa Manispaa katika huu ujenzi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini sasa mradi huu utaanza kujengwa? Ninashukuru kwa majibu mazuri, lakini ni lini sasa mradi huu utaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza, ninapokea pongezi nyingi za Mheshimiwa Ngajilo kwa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita na ni hakika kwamba Serikali hii imefanya kazi kubwa sana katika ujenzi wa miundombinu ya masoko, stendi na miradi mingi ya kimkakati na zoezi hili linaendelea kutekelezwa kwa awamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Ngajilo kwamba katika ujenzi wa miradi yote ya kimkakati, jambo la kwanza halmashauri zenyewe, mabaraza ya madiwani, na Mkurugenzi lazima wawashirikishe wadau wa eneo husika. Kwa hiyo, ninatumia nafasi hii kukuhakikishia kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tutashirikiana kwa karibu na Mkurugenzi wa Manispaa na Baraza lake la Madiwani katika Manispaa ya Iringa kuwashirikisha wadau, wafanyabiashara wadogo na machinga kuridhia eneo hili na aina ya majengo na mpangilio wa majengo kwa bidhaa husika ili wafanyabiashara hawa wapate eneo mwafaka kwa ajili ya kufanya biashara zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kabla hatujaanza ujenzi, tutajihakikishia kwamba tumepata consensus ya pamoja, tumekubaliana, na ujenzi utaanza ili soko hili lisitelekezwe, liwe na tija kama yalivyo malengo ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tayari kwa mwaka wa fedha ujao 2026/2027 Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imetenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuanza, lakini tunamwelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kuandaa andiko la mradi wa kimkakati, wawasilishe Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tulifanyie tathmini, lakini waendelee kutenga fedha kwa awamu kwenye mapato ya ndani wakati Serikali Kuu inatafuta fedha kuwaunga mkono kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo.