Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Fadhili Fabian Ngajilo (2 total)

MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza:-

Je, lini Daraja la Isakalilo – Kitwiru litajengwa, ili kufungua Utalii wa Mbuga ya Wanyama Ruaha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, Fadhili Fabian Ngajilo, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Daraja la Isakalilo – Kitwiru lipo katika Barabara ya Isakalilo – Kitwiru yenye urefu wa kilomita tatu, ambayo inaunganisha kati ya Barabara ya TANZAM na Iringa kwenda Msembe. Daraja hili ni kiunganishi muhimu kuifikia Mbuga ya Wanyama ya Ruaha.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mradi wa TACTIC, Awamu ya Pili, imefanya usanifu wa mradi. Baada ya kukamilika kwa usanifu, mradi huu unaojumuisha ujenzi wa daraja pamoja na barabara za maingilio zenye urefu wa kilomita taru utaanza kutekelezwa.
MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: -

Je, lini Soko la Machinga Complex Iringa litaanza kujengwa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais kwenye Kampeni za Mwaka 2025?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Fadhili Fabian Ngajilo, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa ujenzi wa Soko la Machinga ulibuniwa na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa mwaka wa fedha 2024/2025 ili kukabiliana na changamoto inayowakabili wafanyabiashara wadogo na wa kati, hususan ukosefu wa maeneo sahihi ya kufanyia biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu utajengwa katika eneo la stendi ya mabasi ya zamani lenye ukubwa wa meta za mraba 6,505 lililopo Mtaa wa Stendi Kuu, Kata ya Kitanzini, kwa gharama ya shilingi bilioni 4.67. Soko litakalojengwa litakuwa na vizimba 800, maduka 150 na migahawa nane vyenye uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 958 ambapo kati yao wafanyabiashara wadogo 800, wafanyabiashara wa kati 150 na mama na baba lishe wanane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi, ahsante.