Supplementary Questions from Hon. Alan Thomas Mvano (4 total)
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kakonko Mkoa wa Kigoma tunao uchimbaji wa madini ya dhahabu Kata ya Nyamtukuza, Vijiji vya Nyamtukuza maeneo ya Nyamwilonge. Tarehe 10 Disemba tulikwenda na Mkuu wa Mkoa pale na akazuia shughuli za uchimbaji kwa sababu zilikuwa zinakiuka sheria za mazingira na zinaathiri wananchi wa Vijiji zaidi ya saba vya Kihomoka, Kumwiyando na Vijiji vingine vya Bwera mpaka Nyamwilonge. Je, ni hatua gani zimechukuliwa na Serikali ili kunusuru maisha ya wananchi hao kwa sababu mto ule haufai kabisa kwa matumizi ya binadamu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la uchimbaji wa madini linaendeshwa kwa mujibu wa sheria na suala la uhifadhi wa mazingira linasimamiwa kwa mujibu wa Sheria, Sura ya 191.
Mheshimiwa Spika, ninaomba nitumie nafasi hii kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Kakonko kwamba kipaumbele cha kwanza ni kutunza mazingira, lakini Serikali itaendelea kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wa madini ili kunufaika na rasilimali za madini vilevile kutunza mazingira katika maeneo hayo. Tutawasiliana na Ofisi ya Wizara ya Madini ili tuweze kuliweka sawa na wananchi waweze kuendelea kuchimba madini.
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nipongeze na nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa, Mkoa wa Kigoma umekuwa ukizalisha zaidi ya tani milioni moja za muhogo kwa mwaka. Wilaya ya Kakonko imekuwa ikizalisha zaidi ya tani 184,000 na Wilaya ya Kibondo mathalani zaidi ya tani 174,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza la nyongeza; je, Wizara ya Kilimo ina mpango gani wa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kupanua wigo wa masoko ya zao hili la muhogo ndani ya Wilaya ya Kakonko na Mkoa wa Kigoma? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa bei ya zao la muhogo ilianguka sana, kutoka kuuzwa shilingi 800 hadi 1,000 kwa kila kilo moja kwenda kuuzwa shilingi 150 hadi shilingi 200. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwanusuru wananchi ambao ni wakulima wa zao la muhogo ambao hadi sasa wameshindwa kuvuna zao hilo, kwa sababu hata wakivuna hawawezi kuuza kwa bei iliyoko sokoni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia bwana Alan Mvano ameanza vizuri kuwafuatilia wananchi wake wa Jimbo la Kakonko na ninaomba nimjibu kwamba, moja sisi kama Serikali, Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara tumekuwa tukifanya kazi kwa ukaribu sana. Ndiyo maana utaona katika moja ya hatua ya awali sisi ambayo tunaifanya sasa hivi ni jukumu la kujenga soko katika Halmashauri ya Kakonko. Wizara ya Viwanda na Biashara itakuja ku-complement jambo hili kwa kujenga viwanda ambavyo vitasaidia wakulima katika eneo hilo. Kwa hiyo, huo ni mpango ambao upo na ni endelevu kwa muda wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mpango wa Serikali baada ya bei kushuka; mpango wa Serikali ndiyo huo ambao tumeainisha kwamba kwa nini tunajenga soko. Lengo ni kuhakikisha kwanza moja, tunaongeza thamani, ndiyo maana utaona tumeainisha hapa kwamba tunataka wananchi waongeze tija kwa kuchakata yale mazao yao yaweze kudumu kwa muda mrefu ambapo tunaamini kwamba ukishakausha muhogo badala ya kuuza katika bei ya chini unaweza ukakaa kwa muda mrefu na ukapata bei ambayo ni nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi kama Serikali, jambo hili tunalifahamu na tunalifanyia kazi kwa ukaribu kabisa. Kwa hiyo, tu nimthibitishie tu Mbunge kwamba moja ya kazi kubwa ambayo tutaendelea kuifanya katika eneo hili ni kuboresha haya mazingira ili bei ya muhogo isiweze kushuka kama ambavyo ameainisha hapa.
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. Wilaya ya Kakonko ina mtandao wa barabara wa kilometa 391.24 na uwezo wa TARURA ni kufanya matengenezo kilometa 120 tu sawa na 30.6%. Je, ni lini Serikali itaongeza bajeti ya TARURA katika Wilaya ya Kakonko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba bajeti ya TARURA kila mwaka, kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 imeendelea kuongezeka. Kwa mfano, kutoka shilingi bilioni 210 mwaka 2021/2022 mpaka mwaka huu wa fedha zaidi ya shilingi bilioni 870, ukiondoa fedha za dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunatambua kwamba uhitaji wa fedha ni mkubwa zaidi, lakini tutaendelea kutenga fedha kwa awamu kujenga barabara za Kakonko ili wananchi waweze kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa ufanisi mkubwa zaidi.
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ninaipongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali yetu hii inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara hii ya Ujenzi inafanya kazi kubwa sana katika nchi yetu. Pongezi kubwa sana na ushirikiano tunauona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa barabara hii ya kutokea Kakonko kwenda kwenye mpaka wa Burundi eneo la Muhange ni potential sana kwenye Wilaya yetu. Kwa sababu ya umuhimu wake jambo la kwanza ninamuomba Waziri utayari wake, twende Kakonko aone barabara hii, kwanza aone umuhimu wake vilevile aone hali ya barabara kwa sasa. Jambo la muhimu sana hilo ninaomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kwamba, barabara hii inategemewa na wananchi wa Kata za Nyamtukuza, Nyabibuye, Gwarama, Muhange, Kasuga, na Kakonko; wananchi zaidi ya 60,000 wanaitegemea barabara hii. Sasa kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha barabara hii imekwishapandishwa hadhi, sasa hivi ipo TANROADS.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuhakikisha kuwa barabara hii inapitika vizuri kwa sababu siku chache zilizopita lori limeanguka, limepata ajali katika barabara hii kwa sababu ya ubovu wa barabara kwa ajili ya mvua …
MWENYEKITI: Swali, Mheshimiwa tunakushukuru.
MHE. ALAN T. MVANO: … sasa nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba barabara hii inapitika kwa viwango vya TANROADS wakati tukisubiria upembuzi yakinifu ufanyike? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mvano, Mbunge wa Kakonko, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa niaba ya Serikali na kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, tupokee pongezi zake kwa kazi kubwa ambazo zinafanyika katika shughuli ya miundombinu na hasa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hii barabara kwanza ilikuwa ipo chini ya Wakala wa Barabara Vijijini; na kwa sababu ya umuhimu wake, tunajua ni barabara ya mpakani, ndiyo maana imepandishwa hadhi. Si hadhi tu, kwa sababu inaunganisha nchi na nchi, tunajua wenzetu wa Burundi wamesogeza makao yao makuu ndiyo maana hata imepandishwa kutoka hadhi ya barabara ya mkoa kuwa trunk road. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba umuhimu huo tunautambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimuhakikishie nipo tayari, tutakapopata muda wakati wowote tunaweza kwenda tukaiona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupitika ni suala la kiutendaji. Ninaomba nimuagize Meneja wa Mkoa wa Kigoma ahakikishe kuwa tutakapomaliza Bunge hili apate muda wiki hii akaione na ahakikishe kwamba anafanyia ukarabati ili iweze kupitika na wananchi waweze kupata huduma bora za usafiri na usafirishaji katika barabara hiyo. (Makofi)