Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa nafasi hii. Awali ya yote kwa kuwa nami ni mara ya kwanza ninasimama mbele ya Bunge hili Tukufu, ninaomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ameendelea kutujalia kheri na afya njema sisi wote ambao tuko hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii vilevile, kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwanza kabisa kwa kuaminiwa na Watanzania kwa kupigiwa kura nyingi za kishindo na kwa ushindi mkubwa alioupata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kuniteua chini ya vikao alivyoviongoza yeye mwenyewe. Mimi ndugu yenu, kusimama na kuomba ridhaa kwa wananchi wa Kakonko na ninawashkuru sana wananchi wa Kakonko kwa kuniamini na kunichagua ili niweze kuwawakilisha katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ahadi yangu ni kwamba sitowaangusha, nitafanya kazi usiku na mchana kwa nguvu zangu zote na kwa akili yangu yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa vilevile, kupongeza kazi kubwa ambayo anaifanya Mheshimiwa Rais wetu. Sisi kule Kakonko na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla, niseme Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia heshima kubwa sana wananchi wa Mkoa wa Kigoma. Hii ni kwa sababu miaka ya nyuma watu walikuwa wanaichukulia Kigoma kama eneo ambalo halifai. Watu walikuwa wanaamini watumishi ambao wanafanya vibaya Serikalini wakipelekwa Kigoma maana yake wamepewa adhabu, lakini leo Mheshimiwa Rais huyu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameionesha heshima ya wananchi wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayasema haya kwa sababu miaka ya nyuma hatukuwa tumeunganishwa na barabara za lami kuelekea mikoa mingine, lakini leo ukitoka Mwanza, ukitoka Dar es Salaam, ukitoka Tabora, ukitoka kona yoyote ya nchi hii ukienda Kigoma utafika kwa barabara za lami, huyo ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya Kakonko, kwa miaka minne ambayo Mheshimiwa Rais wetu aliongoza Taifa hili, kipindi kile cha kwanza alituletea fedha nyingi za maendeleo jumla ya fedha alizozileta ni shilingi 28,910,712,714.65. Ninaomba Mheshimiwa Rais huyu apokee shukurani nyingi sana kutoka kwa wananchi wa Kakonko. Ndiyo maana tuliona hospitali ya wilaya ilijengwa, stendi mpya ya kisasa ikajengwa, chuo cha VETA kikajengwa, barabara zikajengwa, shukrani nyingi sana na pongezi nyingi sana zimwendee Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie nafasi hii kuwapongeza viongozi wote wanaomsaidia Mheshimiwa Rais wetu. Kwa nafasi ya pekee nimpongeze sana Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba anafanya kazi kubwa sana. Wasilisho aliloleta hapa kwetu linaonesha namba ambavyo tunaona matumaini makubwa katika Taifa letu na nimesimama hapa kwa kweli kumtia moyo na kuwaambia Watanzania kwamba, Serikali tuliyonayo na viongozi tulionao, Mawaziri tulionao na Naibu Mawaziri tulionao, wanafanya kazi kubwa sana, wanapaswa kutiwa moyo ili waendelee kufanya kazi kwa moyo wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi hiki kifupi, ninaendelea kutoa shukurani kwa Serikali yetu hii. Mwaka huu Wilaya yetu ya Kakonko imepokea jumla ya watumishi 142. Serikali yetu hii imefanya kazi kubwa sana, ninamshukuru sana na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ametuletea mbegu ya ruzuku ya alizeti tani 10 kwa kipindi kifupi hiki. Vilevile, tunashuhudia ujenzi wa soko la kisasa katika Wilaya yetu ya Kakonko. Hayo ni mambo ambayo lazima niyaseme ili Watanzania wajue kazi kubwa ambayo Serikali yetu inafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo hayo, nimekuwa nikifuatilia michango ya Wabunge wengine na kwa kweli nimejifunza mengi na nimesimama hapa kusema kwamba, pamoja na mambo mengine yote, bajeti iliyowasilishwa kwetu na mipango iliyowasilishwa inaonesha namna ambavyo Taifa letu linakwenda kuzalisha kwa kiwango kikubwa mazao ya kilimo, mazao ya uvuvi, kwenye utalii na sekta nyingine za uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tuweze kufika huko tunahitaji fedha. Kwanza kabisa lazima tukubali kwamba, fedha tunazozipata kutoka kwenye makusanyo lazima zitumike vizuri kwa uwazi na kwa uwajibikaji. Wale wote ambao hawatatumia fedha zetu vizuri lazima wachukuliwe hatua ili fedha zote zinazopatikana kutoka kwenye sekta zote ziweze kuelekezwa kwenye maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wilaya ya Kakonko yapo mambo ambayo tunatamani kuona yanafanyika. Kwenye upande wa afya, tunatamani kuona kata saba ambazo hazina vituo vya afya nazo zinapata vituo vya afya, lakini vilevile, tunatamani kuona maeneo yale yaliyotengwa kwa ajili ya chuo cha uuguzi, basi chuo hicho kikaanzishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo vilevile, tunatamani kuona tunakuwa na kiwanda cha kuchakata zao la muhogo. Vilevile, tuone kwamba ile miundombinu ya umwagiliaji ambayo imechakaa ifanyiwe kazi ili wakulima wetu waweze kuzalisha katika misimu yote. Vilevile, tumetenga ekari zaidi ya 1,000 kwa ajili ya kilimo cha parachichi, tunatamani kuona eneo hilo linaendelezwa ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa barabara mvua zilizonyesha zimeathiri sana maeneo yetu, watu wa Itumbiko, Katanga na Njoomulole wanashindwa kufanya shughuli zao kwa sababu mvua zimeharibu miundombinu ya barabara. Kwa hiyo, maeneo yote hayo yanahitaji fedha ili wananchi wetu waweze kufanya shughuli zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mkoa wa Kigoma yapo mambo tunatamani kuona yanafanyika. Kwanza kabisa, tuna reli ya kisasa ambayo mradi wa ujenzi unaendelea lot six, tunatamani kuona Serikali imeweka kipaumbele katika eneo hilo ili tuweze kukuza biashara na nchi za jirani zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Ziwa Tanganyika ni ziwa la kimkakati, tunahitaji kuona tunakuwa na meli nzuri kwa ajili ya kusafirisha watu wetu. Tumeshuhudia siku chache zilizopita watu nane wamepoteza maisha, lazima kama Taifa tuweke meli nzuri kule ili watu wetu waweze kusafiri vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba uniruhusu nitoe mapendekezo yangu kwa bajeti hiiā¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)