Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Arif Suleiman Premji (5 total)

MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali iliahidi kuboresha miundombinu ya maji kwa kuwajengea tenki la lita 1,000,000 Kijiji cha Likonde, Kata ya Mayanga na ahadi hiyo iitolewa tarehe 27 Septemba, 2022 ambalo litaenda kuwasaidia wakazi zaidi ya 24,000. Je, ahadi hiyo itatekelezwa lini? Ninaomba nisisitize neno “lini?”

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, samahani kidogo, ninaomba kujua ni jimbo gani.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, ni jimbo gani tena?

MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni Jimbo la Mtwara Vijijini.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza miradi nchini kote na nchi yetu ina vijiji takribani 12,318. Katika utekelezaji wa miradi ni vijiji 1,575 tu ambavyo vimebaki kutofikishiwa huduma rasmi ya maji. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, eneo hilo tunalichukua likiwemo ndani ya miradi 878 ambayo haijakamilika yenye gharama ya shilingi trilioni 1.3. Tunaamini kwamba miradi hii itakapokamilika yote kwa ujumla na eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliongelea basi litakuwa limekamilika katika utekelezaji huo. (Makofi)
MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri, Kijiji cha Namuhi na Kijiji cha Mnyija, katikati hapo kuna daraja ambalo limeathirika na kuharibika sana kutokana na athari za mvua na hapa tunapoongea sasa hivi wananchi wengi pamoja na wanafunzi wanapitia tabia hiyo ya hilo daraja kuvunjika. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuwasaidia wananchi na wanafunzi hao waweze kupata hiyo access kwa ajili ya kupita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mvua nyingi kunyesha maeneo mengi ya nchi yetu, Serikali kupitia TARURA tumeendelea kufanya tathmini ya maeneo yote ambayo yameathirika na mvua na ndani ya Serikali tunaendelea kujipanga kwa ajili ya kupata fedha ili tuweze kukabiliana na changamoto hii ya kukatika kwa barabara ambayo imeletwa na neema ya mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie Wabunge wote, maeneo yote ambayo yameathirika, Serikali inayafuatilia kwa ukaribu kwa kufanya tathmini na tunajipanga kwa ajili ya kuyafanyia matengenezo.
MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji wa Soil Solution ni wa kimkakati, unaenda kusaidia Taifa hili kupunguza gharama ya Dola za Kimarekani milioni 400 kwa kuagiza mbolea. Majibu ambayo yametolewa ni mepesi mno, uhitaji wa Soil Solution ni gesi na gesi inatoka Mtwara, hadi sasa hivi ni mwaka mzima anazungushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipi kauli rasmi ya Serikali kuhusiana na mradi huo wa kimkakati ambao unaenda kusaidia Taifa letu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mbunge kutoka Mtwara, Ndugu yangu, Mheshimiwa Arif, amekuwa akiniuliza sana swali hili, amekuwa akifuatilia sana kuhusu huyu mwekezaji ambaye kimsingi anatoka Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba Soil Solution Limited ni mojawapo ya uwekezaji wa kimkakati, kulingana na vigezo vyetu, mwekezaji yeyote wa nje anapokuja kuwekeza akiwa na zaidi ya milioni 50 USD ni mwekezaji wa kimkakati, huyo wa kwetu ana zaidi ya milioni 150, anazo milioni 627 za Kimarekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye swali la nyongeza la Mheshimiwa Asha Motto, naomba niseme kwamba Serikali ipo on top of that, na tumekuwa na majadiliano na wenzetu wa Wizara ya Nishati. Ninamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Ndejembi, amekutana mara nyingi sana na huyu mwekezaji na wamemhakikishia kwamba baada ya mipango ya upatikanaji wa gesi itakapokuwa vizuri, tunamhakikishia ujenzi wa kiwanda utaanza. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara kwa kiwango cha lami Barabara ya Ziwani – Madimba – Msimbati – Madimba – Tangazo – Kilambo, kwani kupitia Kikao cha RCC jukumu hilo walipewa watu wa TANROADS, na ukizingatia feasibility study pia ilishafanyika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge. Tunajua umuhimu wa barabara hiyo ambayo inaenda huko Msimbati. Sisi kama TANROADS tulishafanya upembuzi, tulishafanya usanifu na tulishapeleka maombi Wizara ya Fedha, ambao ninajua wanaandaa malipo, ili tuweze kupata kibali cha kuitangaza barabara hiyo. Hii pia ni barabara ambayo inakwenda Daraja la Kilambo ambalo tunashirikiana na wenzetu wa Mozambique, na vile vile wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Nje.
MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itapeleka gari la kubebea wagonjwa Kituo cha Afya Kilambo, Mtwara DC ukizingatia kituo hicho kipo mpakani mwa Msumbiji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu magari ya kubebea wagonjwa, tuna maeneo yenye upungufu kweli, tunakiri, na tumeendelea kuyaomba magari haya pamoja na yale mengine ambayo tayari Serikali imeshayatoa katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ombi lake tunalichukua kwa maana ya kwamba tunapoenda kuomba magari mengine na yeye awe mnufaika katika gari hili la ambulance. (Makofi)