Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Arif Suleiman Premji (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninachukua fursa hii kumshukuru Rais kwa kuwa Jimbo la Mtwara Vijijini kuna miradi mingi sasa hivi imeanza kutekelezwa. Kuna mradi wa maji wa kama shilingi bilioni saba ambao umeshaanza kufanya kazi na kutekelezwa, lakini kuna mradi wa bandari ambao una thamani ya shilingi bilioni mia nne thelathini na nne, kuna mradi pia wa kuchimba gesi asilia pale Ntorya, ambao una thamani ya shilingi bilioni 120. Kwa hiyo, kwa hilo kwanza ninamshukuru sana Rais pamoja na watendaji wote wa Serikali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna msemo wanasema ukimtegemea nduguyo, utakufa maskini, hapo kidogo ninaomba nielezee kuhusiana na mafuta. Nchi yetu tangu ipate uhuru imepitia changamoto ya mafuta mara tano mpaka mwaka huu. Ukianza na mwaka 1970 palikuwa na vita ya Yom Kippur ambayo ilisababisha mafuta yawe yanapatikana kwa shida, lakini mwaka 1979 tulikuwa kwenye Vita ya Kagera na Mapinduzi ya Iran pia, pakawa na changamoto ya mafuta tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2011 pakawa na mgogoro baina ya wafanyabiashara na EWURA, 2022 Vita ya Ukraine na sasa hivi 2026 ni Vita ya Mashariki ya Kati, Iran hapo. Hii ni historia fupi ambayo tunapita na tuliipitia lakini je, tunajifunza nini? Tunajiandaa vipi? Historia hii hapo tunajiandaa vipi?

Mheshimiwa Naibu Spika, inanishangaza sana kuona kwamba Mwenyezi Mungu ametujaalia rasilimali ya gesi, gesi ambayo iko Msimbati, gesi ambayo iko Ntorya, gesi hiyo ikichakatwa inaweza ikabadilishwa ikawa diesel. Siyo diesel tu hata jet fuel, mafuta kwa ajili ya ndege na ukiangalia sasa hivi ATCL kama performance inafahamika. Kwa hiyo, vitu hivyo tunavyo na tumeshapitia hiyo changamoto kwa muda mrefu, tunashindwa nini kuwekeza humo, maana yake kama mradi kuna watu walishawahi kufika wakafanya feasibility study, shilingi milioni mia nne ishirini inahitajika kwa ajili ya kubadilisha gesi kwenda kwenye diesel, ambapo tunaweza tukapata takribani mapipa 3,000 kwa siku na pipa moja ni lita 159, tunashindwa nini, tunachelewa wapi, tunamsubiri nani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa kwanza ulikuwa kwenye suala hilo la mafuta ambalo tunahitaji tujitathmini wenyewe na tuweze kutoka kwenye janga hilo ili tupunguze athari hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, imeomba shilingi trilioni 12.5, katika shilingi trilioni 12.5, shilingi trilioni 8.5 ni za kuendesha ofisi na shilingi trilioni 3.7 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Sasa huwa nashangaa kitu kimoja, kumwona Waziri Mkuu anazunguka nchi nzima kwenda kutatua changamoto ilihali wapo watendaji, kwenye bajeti tunayoenda kule ya Mwaka wa Fedha 2026/2027 tunawatengea shilingi trilioni 8.5, yaani tumsubiri Waziri Mkuu aje atatue changamoto za wananchi wakati kuna watu wanapokea shilingi trilioni 8.5, tujitafakari!

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninashauri jambo moja kwenye hilo, shilingi trilioni 8.5 hizi fedha ni dhamana za wananchi za walipakodi na siyo za watu, tunapaswa tuangalie nidhamu ya watumishi wetu, watendaji wetu ili hizi shilingi trilioni 8.5 tunapozitoa, basi zifanye kazi kwa kuleta tija kwa wananchi, lakini kupunguza ukiritimba pia kwenye ofisi hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna suala la accountability na transparency, uwazi na uwajibikaji kwenye miradi ya maendeleo. Shilingi trilioni 3.77 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni lazima ziende zikasimamiwe kwa uadilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuzungumzia kwenye suala lingine la upande wa vijana. Shilingi bilioni 183.95 ndiyo zipo kwenye mambo ya vijana chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini ukiangalia 2024/2025, Shirika la Dunia la Kazi na Taasisi ya Takwimu ya Taifa ya kwetu walifanya analysis kidogo, walipata kujua kwamba 24.3% ya vijana ambao hawana ujuzi, hawapo kwenye elimu na hawana ajira (NEET), not in employment, training na education hawapo, 23.4%. Ukiangalia takwimu ni sawasawa na vijana milioni 4.3 wa nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa bajeti iliyotengwa kwenye hilo suala la vijana ni shilingi bilioni 183.95 na ukichukulia uwiano tu, ukachukua shilingi bilioni 183.95, ukagawanya na vijana hao milioni 4.3, ni takribani shilingi 44,000. Ninaomba sana, kwenye suala hilo la vijana, bajeti hiyo ya 183.95 billion ni ndogo, twende na uhalisia uliopo kwamba vijana ni wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamalizia kwenda kwenye Jimbo langu la Mtwara Vijijini. Tunatambua jitihada nyingi za Serikali za kuleta maendeleo ambayo yanafanyika kwenye Jimbo la Mtwara Vijijini, lakini kuna suala la elimu, tuna uhaba mkubwa wa kidato cha tano na sita, tunazo Kata 21 na tunayo shule moja tu ya kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa faida ya muda, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)