Supplementary Questions from Hon. Emmanuel John Khambay (3 total)
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza. Kama ambavyo amekiri mwenyewe kwamba Gereza la Babati ni miongoni mwa magereza yaliyojengwa kwa miaka ya zamani, je, ni nini mpango wa Serikali wa kujenga gereza lingine jipya ambalo pia litakuwa ni gereza la kisasa linaloendana na wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Emmanuel kwa swali lake la nyongeza ambalo ni la muhimu sana. Kwanza tukiri ni kweli tuna uhitaji mkubwa wa magereza nchini, kwani katika hali ya sasa nchi nzima tuna idadi ya magereza 129. Kati ya magereza hayo, magereza 10 yana hadhi ya magereza ya kanda, magereza 76 yana hadhi ya magereza ya mikoa na wilaya na magereza 43 ni magereza ya wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo, tuna upungufu wa takribani wilaya 50 ambazo hazina magereza, lakini kazi inayoendelea sasa ya ujenzi wa magereza katika maeneo mbalimbali ambayo kwa kweli kwa baadhi ya maeneo imepiga hatua nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Wilaya ya Karatu gereza limekamilika, Wilaya ya Kilosa limeanza ujenzi, Wilaya ya Gairo linaendelea, Wilaya ya Kingurungundwa kule Mchinga nalo linaendelea. Ninaamini kwamba na maeneo mengine pia tutaendelea na hatua kama ambavyo nimetaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali kwenye ujenzi wa magereza haya ni kuendelea kuweka fedha kwenye bajeti, kwani tayari tumeshafanya tathmini ya uhitaji wa magereza hayo kwamba kila gereza moja linahitaji wastani wa shilingi bilioni nane kulijenga. Hivyo, kwa magereza 50 tunahitaji wastani wa shilingi bilioni 40 ili tuweze kujenga magereza hayo. Sambamba na hilo, tunafahamu pia ipo changamoto kubwa ya makazi ya Askari Magereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo hilo, pia Serikali imeandaa mpango wa muda mrefu ambao utajenga wastani wa nyumba 6,368 za magereza zitakazoweza kukaliwa na wastani wa kata 21,187. Bajeti ya fedha hizo zinahitajika zaidi ya shilingi trilioni 2.88 kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kituo cha Afya cha Nangara kimejengwa na nguvu za wananchi na ni jengo moja tu la OPD. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha nyingine ili kuweza kumalizia majengo mengine ili wananchi hao ambao wanafuata huduma umbali mrefu waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki cha afya, kwanza tunawashukuru sana wananchi kwa kutoa nguvu zao na kuweza kuunga mkono juhudi za Serikali, lakini pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nimeshaongea na Mkurugenzi, na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI niendelee kumwelekeza Mkurugenzi kutenga fedha za ndani ili kukamilisha baadhi ya majengo katika kituo hiki baada ya kutoa OPD waendelee kutoa na huduma nyingine ambazo zinatakiwa kwenye kituo cha afya. (Makofi)
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, Ziwa Babati limevamiwa na magugu na linaenda kupotea. Nini mpango wa Serikali katika kulinusuru Ziwa hilo ambalo ni muhimu kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Babati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, Serikali inao mpango endelevu wa kukabiliana na athari za mazingira ambazo zimetokea kwenye maziwa yetu, siyo tu Ziwa Babati, tunalo Ziwa Victoria, Ziwa Jipe pamoja na na maziwa mengine.
Mheshimiwa Spika, kwa Ziwa Babati, cha kwanza ambacho tumeweka mkakati ni kushirikiana na Wizara ya Maji ambao ndio wanaohusika na mabonde pamoja na maji ili kwanza tuweke mipaka kwa maana ya kuweka beacons za mipaka ambazo zitaonyesha ukomo wa eneo la shughuli za kibinadamu.
Mheshimiwa Spika, pili, Serikali itaendelea kuwatafutia wananchi wa maeneo yanayozunguka maziwa shughuli mbadala ambazo hazitaathiri maeneo haya ambayo tunalenga kuyahifadhi.