Supplementary Questions from Hon. Jafari Wambura Chege (3 total)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina swali la nyongeza. Mradi wa Maji wa Miji 28 Rorya, Tarime umesimama kwa muda mrefu na Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana nami mradi ule umekwenda kwa kusuasua sana kwa muda mrefu kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi huo.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Mradi huu wa kutoka Tarime – Rorya ambao awali tulitegemea mradi huu pia ukatoe huduma maeneo ya Serengeti, Mugumu kule ni kweli umesuasusa. Hata hivyo, Wizara tumechukua hatua ya kukaa na Wakandarasi wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha. Mradi huu Mkandarasi aendelee kuutekeleza ili lengo ni kwamba atakapokuwa ana-raise certificate, basi Serikali itaweza kumlipa kulingana na kazi atakayokuwa ameifanya. Ninakushukuru sana.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi. Barabara ya Utegi – Shirati – Kirongwe yenye kilometa 56, kwa bahati nzuri kilometa 27 za Utegi – Shirati zilitangazwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami. Ninataka nipate status, so far barabara ile sasa imefikia wapi kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, hiyo barabara inasubiri tu kufanya signing tutakapokuwa tumekamilisha taratibu zote.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka nijue ni lini Uwanja wa Ndege wa Musoma, kama kielelezo cha Mkoa wa Mara, utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa Mkoa wa Mara, ilianza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mara. Pale Serikali inajenga runway, kwa maana ya njia ya kuruka na kutua ndege, pia inajenga na majengo mbalimbali. Tayari runway imekamilika, tunakwenda kumalizia majengo yaliyobaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema ninaomba kurejea kauli yangu niliyoitoa siku tano au sita kwamba, kuanzia mwezi ujao au unaofuatia, Serikali ina mpango wa kuanza kufanya testing ya ndege za Shirika letu la Ndege ATCL kwenye viwanja vitatu; Uwanja wa Musoma, Shinyanga na Sumbawanga. Hii ni kuthibitisha dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba, ameamua kuitendea haki nchi hii kwenye sekta ya anga.