Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Japhael Masanja Lufungija (5 total)

MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Napenda kumwuliza Naibu Waziri kwamba, Jimbo la Ulyankulu kuna mradi wa bwawa la umwagiliaji pale Kata Konanne, ambapo Serikali imeahidi kwa muda mrefu kulijenga, lakini pamoja na Bwawa la Mwamnange, je, ni lini utekelezaji wa miradi hii utaanza kufanyika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika miradi ambayo Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, tumepanga kuitekeleza kuanzia mwaka wa fedha unaokuja ni pamoja na ambayo baadhi ameitaja Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, matarajio ni kwamba sasa tunakwenda katika utekelezaji baada ya kukamilisha upembuzi na usanifu wa kina.
MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, ninaanza kwa kupongeza kwa juhudi kubwa za namna ambavyo Serikali inaendelea kuongeza mtandao na fedha kwenye barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza. Kwa kuwa barabara ya Chemba – Nhw’ande – Twigu inayounganisha Kata ya Sasu ni barabara ndefu sana ukilinganisha na fedha zilizotengwa. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba sasa zinajengwa karavati ili barabara iweze kupitika kwa wakati wote?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Barabara ya King’wangoko – Usonga imepewa fedha shilingi milioni 416; lakini barabara hiyo inapitika kwa kipindi cha kiangazi tu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inajenga daraja pale Mto Igombe? Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi baada ya Bunge kwenda kutembelea barabara hizo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Japhael Masanja Lufungija amefuatilia sana ujenzi wa barabara katika Jimbo la Ulyankulu. Nimhakikishie kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha kuwa barabara za vijijini na mijini zinajengwa na zinapitika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, barabara hizo ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja, zote mbili nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kwanza na tathmini ya mahitaji ya fedha kufuatia uharibifu wa mvua nyingi zilizoonyesha pote nchini, ikiwemo katika Jimbo la Ulyankulu; na tutapeleka fedha kwa awamu kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, kumwelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Tabora na Wilaya ya Kaliua kuhakikisha kwamba wanafanya tathmini na kuwasilisha ongezeko la mahitaji ya fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo. (Makofi)
MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Margaret Sitta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kilimo cha mahindi ni zao la mkakati katika nchi yetu, na ni zao linalolimwa na wananchi wengi, wakiwepo wananchi maskini na hasa wale ambao wanahudumiwa na Serikali, kwa maana ya TASAF, ukilinganisha gharama ya mbegu kwa wastani kilo mbili za mbegu zinanunuliwa kwa shilingi 15,000 kwa maana ya ekari moja inatumia mifuko minne kwa thamani ya shilingi 60,000, ukijumlisha pamoja na mbolea na gharama za kilimo inapelekea wastani wa heka moja cost yake kama 350,000, je, Wizara ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba gharama ya mbegu inashuka ili kuweza kuzibeba na familia maskini ziweze kulima vizuri zao la mahindi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Katika Mkoa wa Tabora, na hasa kwenye Jimbo la Urambo, Ulyankulu, Kaliua na majimbo mengine, lipo tatizo la wadudu waharibifu wa mahindi hasa yakiwa na kina kuanzia futi moja mpaka futi tano. Wadudu wanaitwa al-maarufu rusomi, wanashambulia sana mahindi na kuyaharibu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba dawa za kuwatibu wadudu wale zinaingia kwenye ruzuku?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, ameuliza maswali ya msingi kwa niaba ya Mheshimiwa Mama Sitta. Nimwambie tu kwamba moja ya mpango wa Serikali katika kupunguza gharama kwa mkulima ni pamoja na kuweka ruzuku. Miongoni mwa ruzuku tulizoweka, tumeweka ruzuku katika mbegu, lakini vilevile tumeweka ruzuku katika mbolea na viuatilifu, lengo tu ni kupunguza gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, bado Serikali tumeendelea na mikakati ya kuhakikisha kwamba uzalishaji wa mbegu unaongezeka. Ndiyo maana sasa hivi kwa wakulima ambao wanataka kuingia katika kile kilimo cha kimkataba katika mashamba ambayo yanamilikiwa na Wakala wetu wa Uzalishaji wa Mbegu (ASA), tumekuwa tukiruhusu watu kuingia katika kilimo cha kimkataba ili tuongeze uzalishaji wa mbegu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba bado tunaendelea na michakato ya kuhakikisha kuwa tunaongeza uzalishaji ili tuhakikishe kuwa bei inashuka pamoja na kwamba tumeweka ruzuku ndani yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hawa wadudu waharibifu ambao ameainisha, watu wetu wa TPHPA wanaendelea na hiyo kufanya tathmini kwa sababu uwekaji wa ruzuku katika viuatilifu ni hatua kwa hatua. Kwa hiyo, tumeweka sehemu katika mazao kama ya parachichi, tumeweka sehemu katika mazao ya korosho na vilevile tutaangalia katika wadudu waharibifu wa mahindi. Kwa hiyo, na lenyewe lipo katika mchakato na tukishalikamilisha tutatolea taarifa hapa. Ahsante sana.
MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Maaskari wa Polisi katika Jimbo la Ulyankulu, wafanyabiashara wa Kata ya Uyowa Kijiji cha Mwamnange, pamoja na wafanyabiashara wa Kata ya Kona Nne Kijiji cha King'wangoko walijenga kituo cha Polisi kwa ajili ya malengo ya kuimarisha usalama wao. Hata hivyo, vituo hivi vimeshindwa kukamilika. Mbaya zaidi, Kituo cha Polisi cha Kona Nne kimepanga kwenye nyumba ya mtu, ambapo zaidi ya miaka tisa hajalipwa. Je, Serikali ina kauli gani kuhusiana na kukamilika kwa vituo vya Polisi hivi viwili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Lufungija kwa hoja yake ya kukamilisha vituo vya Polisi katika eneo la Ulyankulu kama ambavyo ameainisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati najibu swali la msingi na la awali katika Bunge hili, nilieleza kwamba vipo vituo 77 vya Polisi katika kata mbalimbali ambavyo bado havijamalizika, na vipo katika ngazi ya maboma. Tulieleza kwamba kwenye awamu ya kwanza ya ujenzi wa vituo, vituo 77 hivi vitaingia kwa ajili ya kumaliziwa na vile vipya kuweza kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Ulyankulu kwamba, mara baada ya kutenga fedha na kupata bajeti hiyo mwaka wa fedha 2026/2027, tutaanza kukamilisha maboma haya ya vituo vya Polisi ambavyo bado havijakamalika.
MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi. Jimbo la Ulyankulu ni miongoni mwa majimbo yenye hali ngumu ya kimawasiliano hasa katika Kata ya Uyowa, Kijiji cha Mwamnange chenye wakazi wengi na kijiji cha kibiashara Kata za Sasu, Ilege na Nhwande kwa maana ya Kata ya Mwongozo. Lini Wizara itakwenda kujenga minara kwenye maeneo hayo ili wananchi waweze kunufaika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, tunatambua changamoto ya mawasiliano iliyopo katika jimbo hili na hivi karibuni, ninadhani wiki hii iliyopita wataalamu wa UCSAF walikuwa kwenye eneo la jimbo hili kufanya tathmini. Tunasubiri taarifa yao ili utekelezaji uanze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya taarifa hiyo ya wataalamu kuwasilishwa Wizarani tutafanya mpango wa dharura wa kuhakikisha kwamba katika maeneo ambayo hayana mawasiliano kabisa katika Jimbo lake la Ulyankulu yanafanyiwa kazi, ninashukuru.