MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi. Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa sana za kukabiliana na madhara yanayosababishwa na wanyama waharibifu aina ya ndovu. Njia zinazotumika kukabiliana na wanyama hawa kwa sasa ni pamoja na kuwafunga chip maalum za utambuzi, kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kuwahamisha.
Mheshimiwa Spika, sambamba na jitihada hizi, bado hakuna matarajio makubwa yaliyopatikana ukilinganisha na madhara yanayopatikana katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo kupoteza mazao ya wakulima pamoja na kuua wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutumia njia ya culling (kuwaua ndovu kwa utaratibu maalum ili kuwapunguza bila kuathiri sera na sheria za Kimataifa) ili kuweza kunusuru hali iliyopo sasa katika maeneo mbalimbali nchini? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninatambua jambo hili ambalo Mbunge wa Nachingwea, Mheshimiwa Liwaka amelisema. Ni kweli kumekuwa na kilio kikubwa maeneo mengi kuhusiana na uharibifu huu ambao unafanywa na wanyama wakali, hususan ndovu ambao umekuwa ukijitokeza kutokana na kutawanyika katika maeneo ya makazi na maeneo ya mashamba kwa wanyama hao.
Mheshimiwa Spika, nimelipokea pendekezo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelitoa, lakini ninaomba niseme kwamba, Tanzania ni mwanachama wa mikataba mbalimbali ya Kimataifa. Kwenye mikataba hiyo ya Kimataifa yapo makundi na aina za wanyama ambayo yamewekwa kwenye kundi la wanyama ambao wapo hatarini kupotea, na ndovu ni miongoni mwa wanyama hao ambao wanachukuliwa kama sehemu ya kundi la wanyama ambao wapo hatarini katika kupotea.
Mheshimiwa Spika, kwenye mikataba ya Kimataifa, wanyama wa aina hiyo wanalindwa na mikataba hiyo na hawaruhusiwi kuuawa ama kusafirisha mazao yanayotokana na wanyama hao mpaka kwa utaratibu maalum. Kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa mikataba hiyo, kwa sasa pendekezo hilo la kuwavuna (kuwaua) wanyama wa aina hiyo linaingia kwenye utaratibu ule unaochukuliwa kwamba unakiuka mikataba ya kuwalinda aina ya wanyama ambao wapo hatarini kwenye kupotea.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo Serikali kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo, imeendelea kuchukua hatua zikiwemo kuongeza vituo katika maeneo mengi. Hata kote nilikopita kwenye ziara, wananchi walikuwa wanaomba vituo viongezeke vya kukabiliana na wanyama wakali aina ya ndovu na kuwadhibiti, kutokwenda kwenye makazi na mashamba ya watu kila wakati.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wizara ya Maliasili na Utalii, itaendelea kutekeleza uanzishwaji wa vituo hivyo karibu kila eneo ambalo lilikuwa na hatari hizo ili kuweza kukabiliana na tishio hilo na athari ambazo zimekuwa zikijitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Serikali imeendelea kuja na utaratibu mpya wa namna ya kuwafukuza. Katika baadhi ya maeneo na katika baadhi ya mikakati ambayo Wizara imekuja nayo ni ya kuwa na ndege nyuki (drones) ambazo zitatumika kuweza kuwafukuza punde watakapokuwa wamebainika kwamba uelekeo wanakokwenda kutakuwa na madhara, ili mambo haya yawe yanafanyika kabla hawajaleta athari katika maeneo husika.
Mheshimiwa Spika, kadhalika, Wizara itaendelea kuongeza idadi ya Askari katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa na upungufu wa Askari. Wizara itaendelea kuongeza idadi ya Askari ili waweze kukabiliana na wanyama kwa uharaka.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi kilichopita uelekeo na nguvu, kama nchi na kama Serikali ulikuwa umeelekezwa kukabiliana na majangili, lakini kwa sasa tunaenda pia kuelekeza nguvu kubwa kukabiliana na wanyama wasiende katika maeneo ya wananchi ili kuweza kuleta athari ambazo zimekuwa zikijitokeza.
Mheshimiwa Spika, utakubaliana na mimi, kuna muda kulikuwepo na kilio kikubwa sana cha kwamba uelekeo umeelekezwa zaidi katika kuwalinda wanyama kuliko kulinda athari za wanyama wanazoleta kwa mashamba pamoja na wanadamu. Tumeshalipokea hilo kama Serikali, na ndiyo maana umeona Wizara sasa inaongeza idadi ya Askari na idadi ya vituo ili kuweza kudhibiti madhara hayo kabla hayajajitokeza.