Supplementary Questions from Hon. Dr. Emanuel Qambaji Nuwas (5 total)
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Mbulu Vijijini, kuna Barabara ya Geterer kupitia Hydarer kwenda Orbesh ambayo inaunganisha halmashauri tatu: Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Vijijini; Halmashauri ya Hanang; na Halmashauri ya Babati Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Kivuko cha Dagay au Hydarer ambacho kimekuwa kikishidwa kuhimili maji. Katika msimu huu wa mvua imesababisha kukwamisha wananchi kusafiri ikiwemo wagonjwa kwa zaidi ya mara 10, na pia maji yalipovuka yaliathiri nyumba zaidi ya 10 na kuathiri mali za wananchi. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja katika eneo hilo ili kuweza kuwasaidia wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu Vijijini, ni barabara muhimu kwenye eneo lile. Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara kwenye Mkoa wa Manyara na eneo hilo la Mbulu na sisi TAMISEMI tuliambatana naye.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaielewa changamoto hiyo anayoizungumza Mheshimiwa Mbunge, na barabara hii inakwenda kwenye Hospitali ya Haydom ambayo ni Hospitali ya Rufaa, hospitali muhimu sana kwenye Mkoa huo wa Manyara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu alishaitolea maelekezo barabara hii, tumeichukua kwenye bajeti zetu na kwa kweli inakwenda kujengwa kama ambavyo kiongozi wetu ameahidi.
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Mji Mdogo wa Haydom ambao unategemea umeme kutoka Mji wa Katesh ambapo umeme huo hupita umbali mrefu sana na hivyo Mji huu kupata changamoto ya umeme kukatikatika mara nyingi, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kituo cha kupoozea umeme ili kuwahakikishia wananchi hao kupata umeme wa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali siyo tu kuhakikisha taa zinawaka, lakini pia ni kuhakikisha nishati ya umeme inatumika kwa ajili ya uchumi. Kwa sababu hiyo, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wanapata umeme wa kutosha ambao utawasidia katika kuendesha maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mheshimiwa Mbunge nimelipokea, tutajenga substation katika eneo hili ili kuimarisha upatikanaji wa umeme ambao unaweza kusaidia katika uchumi wa eneo lake. Ahsante.
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa chanzo hiki cha maji cha Dambiya kina maji ya kutosha na kitakwenda kuhudumia zaidi ya vijiji 21, tuna mji wa Dongobesh ambao ni Makao Makuu ya Halmashauri, una hospitali ya halmashauri, una kituo cha afya na vilevile una shule za sekondari mbili na shule za msingi tano. Mji huu sasa hivi hauna maji na unapata mgao wa maji angalau mara mbili....
SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye swali.
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani kuweza kuvuta maji kutoka chanzo hiki ambacho ni chini ya kilometa saba na matanki yapo katika mji huu ili kuweza kuwasaidia wananchi hawa ambao wana tatizo la maji na huduma ziweze kuendelea?
Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza. Tunao mradi katika Kijiji cha Qaloda Kata ya Dongobesh ambao sasa Kijiji hiki kina kaya 386 na mradi huu umekwama kwa zaidi ya miaka miwili, na una mabomba pale. Je, Serikali ina mpango gani kukamilisha mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Dkt. Emanuel, Mbunge wa Mbulu Vijijini. Ni kweli kabisa mradi huu ambao unatekelezwa wenye gharama ya shilingi bilioni 41.2 ambapo Serikali mpaka sasa imeshamlipa mkandarasi takribani shilingi bilioni tisa.
Mheshimiwa Spika, mradi utakapokamilika utaweza kuhakikisha kwamba vijiji 76 vya Mbulu Vijijini vitakuwa vimepata huduma ya majisafi na salama. Vilevile, katika vijiji ambavyo vimebaki, ndani ya nchi yetu kati ya vijiji 12,318 ni vijiji 1,575 tu ambavyo vimeshabaki, ambapo miradi zaidi ya 3,714 vyenye gharama ya shilingi trilioni 1.8 vimeshakamilika na miradi 878 inayoendelea yenye gharama ya shilingi trilioni 1.3.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika miradi inayoendelea pamoja na huu ambao amesema kwamba unasuasua, tunaenda kuhakikisha mradi huo unakamilika na wananchi wake wa Mbulu Vijijini wanapata huduma ya majisafi na salama.
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninashukuru sana kwa kazi nzuri ambayo inafanywa na Serikali na kazi inaendelea, lakini bado speed siyo kubwa. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Tuna wananchi ambao barabara imewafuata kwa upande wa Mbulu – Garbabi na Labay – Haydom. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kuwalipa fidia wananchi hawa na kumwezesha mkandarasi kuikimbiza hii kazi kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Tuna kipande cha Garbabi – Dongobesh – Labay, kilometa 35, ambayo bado mchakato wake haujaanza, na Barabara hii inategemewa sana na wakulima wa kilimo cha umwagiliaji. Je, ni lini Serikali itaanza mchakato wa ujenzi wa kipande hiki cha katikati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hawa wananchi ambao barabara imewafuata, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutahakikisha wanalipwa kabla hawajaondolewa kwenye maeneo yao ambayo barabara imewafuata. Kwa hiyo, tutahakikisha, kwa sababu barabara tumeshaanza kuijenga, na ili tujenge, ni lazima tuwalipe. Kwa hiyo, niwahakikishie tutawalipa hiyo fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la Garbabi – Dongobesh, ninadhani ndiyo barabara ambayo inaenda Dareda. Tumeshaanza upande wa Dareda Mission, tunajenga, na tutahakikisha tunaikamilisha hiyo barabara kwa kiwango cha lami, kadri fedha itakavyokuwa inapatikana. (Makofi)
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa shamba hili ni shamba muhimu sana na limezungukwa na wananchi ambao wana uhitaji mkubwa, lakini pia wamekuwa wakipata changamoto, ninashukuru kupata majibu mazuri ya Serikali. Sasa wakati wa kampeni ya Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba baada ya kampeni shamba hili litaweza kufanyiwa mapitio ili kuweza kufanyiwa uamuzi wa mwisho. Je, nini kauli ya Wizara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Waziri yuko tayari kufika katika Jimbo la Hanang ili kujionea mateso ambayo wanapata wananchi wanaozunguka shamba hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ambayo yameulizwa na Mbunge kutoka katika Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Asia Halamga kwa kazi kubwa anayoifanya. Mimi ni shahidi, amekuwa akiisumbua sana Serikali kuhusu haya mashamba mawili, shamba ambalo linamilikiwa na huyu mwekezaji Ngano Limited vilevile shamba ambalo kimsingi linasimamiwa na Serikali ya Halmashauri ya Hanang.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninawahakikishia, watu wa Hanang hawakukosea kumchagua Mheshimiwa Asia Halamga na sisi kama Serikali tupo tayari kumpa ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, ninaomba kujibu maswali mawili kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, Rais alipoenda kufanya ziara pale Manyara alitoa commitment kwamba kwa kupitia taasisi yetu TISEZA kwamba tufanye tathmini ya kina tuone kama kuna haja ya kuendelea na yule mwekezaji au Serikali ichukue maamuzi mengine. Tayari sisi kama Serikali tulishanza kufanya tathmini na tunaendelea na hiyo tathmini.
Ninaomba nikuahidi, baada ya tathmini ile kukamilika tutatoa taarifa kwenye Kamati yetu ya Utawala, Katiba na Sheria, lakini Kamati yetu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma ambako kimsingi TISEZA anaripoti ili vilevile muweze kupata taarifa na sisi kama Serikali tutachukua uamuzi wa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ninakubali kwamba baada ya Bunge hili tutafanya mkutano kule Manyara hususan katika Jimbo la Hanang pamoja na Mbunge ili tukasikilize kero za wananchi hususan wafugaji na wakulima katiKa Jimbo la Hanang, ninashukuru. (Makofi)