Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Devotha Daniel Mburarugaba (5 total)

MHE. DEVOTHA D. MBURARUGAMBA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimshukuru Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye sekta ya elimu. Pia naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Je, ni lini Serikali itaondoa vigezo hivi ili kuweza kuweka usawa kwa shule hizi za sekta binafsi, kwani tunafahamu kabisa kwamba wanafunzi hawa wanaosoma sekta binafsi wanasaidiwa na wazazi ambao wanajikwamua kwenye kipato cha chini, yaani wanajinyima, pia wanasaidiwa na marafiki, ndugu, jamaa na watu mbalimbali kutoa misaada hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, ni lini Serikali itaondoa vigezo hivi ili kuwatia moyo wazazi hawa ambao wameweza kujinyima kuwalipia ada na watu mbalimbali wanaochangia hizi ada, ili kupunguza msongamano kwenye shule za umma kwa maana ya shule za Serikali? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, mwongozo wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu hauhitaji kigezo cha aina ya shule aliyosoma mwombaji, iwe ya Serikali ama iwe ya binafsi. Hivyo, wanafunzi wote sifa za kupata mkopo wa elimu ya juu hupatiwa mkopo huo kwa mujibu wa utaratibu wa vigezo vilivyowekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba, Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Sura 178, imeweka vigezo mahsusi ambavyo mwanafunzi mlengwa hutakiwa awe navyo. Vigezo hivyo ni pamoja na; awe Mtanzania mhitaji, awe amepata udahili katika taasisi zinazotambulika, pia awe amejaza fomu hizo kwa usahihi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi na swali la nyongeza, ni kwamba hakuna kigezo kinachowapunguzia fursa wanafunzi wa shule binafsi kupata mikopo.
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Ni lini Wilaya ya Kyerwa itaweza kupata maji ya uhakika? Kwani mradi ambao uko Wilaya ya Kyerwa unatekelezwa kwa kusuasua. Nilitaka kujua shida ni mkandarasi au kuna mkakati mwingine?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kuna baadhi ya miradi ambayo inaendelea kutekelezwa lakini kuna mingine ambayo inasuasua. Nimwelekeze RM Mkoa wa Kagera aende Kyerwa leo akafanye tathmini na kujiridhisha kuna changamoto gani, ili atuletee kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki kulingana na uzembe ambao unaweza ukasababishwa na wakandarasi, na kama siyo mkandarasi, tujue kwamba tatizo liko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana.
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa kwamba kumekuwa na changamoto kubwa katika urejeshaji wa mikopo na tunafahamu Serikali yetu imekuwa ikitenga fedha kwa kila halmashauri kila mwaka, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri, changamoto za urejeshaji zimekua ni kubwa sana.

Je, ni lini Serikali itaamua kuweka elimu ya fedha kwa wanufaika hawa ili waweze kuelewa biashara wanazoenda kuzifanya, ili tuweze kukusanya mapato yetu kwa ukamilifu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Devotha Daniel kwa kuuliza swali la nyongeza ambalo anawapambania wananchi, hasa wa Mkoa wa Kagera, lakini ni kwa nchi nzima ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, tumekwishaelekeza watalamu wetu, Maafisa Maendeleo waweze kutoa elimu ya mikopo. Sambamba na hilo Kamati ya TAMISEMI ilitoa maelekezo mahsusi na sisi kama Wizara tumeyachukua na tumewaelekeza wataalam wetu kule halmashauri waweze kutoa elimu ya mikopo hii na pia waweze kutoa elimu ya namna ya kusaidia vikundi hivi kuweza kufanya marejesho, lakini pia waweze kupata zile kazi za 30% za PPRA ili kuweza kusaidia vikundi hivi katika mikopo viweze ku-qualify na vile vingine ambavyo ni vipya vianze kukopeshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la mikopo hii liko wazi katika miongozo kwa maana ya kwamba ni kuwasaidia mitaji. Kwa hiyo, tunawaomba sana Watanzania wanaopata mikopo hii ya vikundi waweze kufanya marejesho kwa wakati ili tuweze kuwakopesha na wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Tunalo suala la double allocation, na hili limeleta migogoro mingi kwa wananchi. Serikali imejipangaje ku-solve tatizo la double allocation?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote ambayo yamepatikana pasipo kufuata utaratibu wa kisheria, mamlaka zinaturuhusu kusikiliza changamoto hiyo na kumfutia yule ambaye amepata ardhi hiyo bila kufuata utaratibu, na yule ambaye amethibitika kuwa ni mali yake anapewa. Kwa hiyo, tunamfutia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama kuna makosa yametendeka, huwa tunaongea kwa utaratibu wa kiutawala na kufanya umilikishaji wa maeneo mengine, lakini la msingi ni kufuta umiliki wa yule ambaye amepata pasipo utaratibu.
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa maslahi mapana ya wananchi wa Mkoa wa Kagera, ni lini Barabara ya Nyakahura – Rulenge - Murugarama itajengwa kwa kiwango cha lami? Tunafahamu barabara hiyo ina kilometa 141 na ni barabara ya kimkakati ndani ya Wilaya ya Ngara.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara aliyoitaja kwanza tunaitambua, ndiyo barabara ambayo inaenda kwenye machimbo ya Nikeli. Kwa hiyo, kama Serikali ninapenda umhakikisha Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Ngara kwamba Barabara ya Nyakahura, Muguga, Rulenge hadi Ngara yenyewe, ipo kwenye mpango.

Mheshimiwa Spika, ninamhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mtupitishe bajeti kwa sababu iko kwenye mpango wa kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Ninadhani ataiona kwenye bajeti yetu siku tutakapokuwa tunaisoma hapa, ahsante.