MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA aliuliza:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kurekebisha kigezo kinachowapunguzia fursa wanafunzi wa shule binafsi kupata mikopo ya elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba nijibu swali la Mheshimiwa Devotha Daniel, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upangaji na utoaji mikopo ya elimu ya juu unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (Sura 178) ambayo inabainisha sifa za msingi za mwombaji, zikiwepo sifa za kitaaluma za kujiunga na taasisi za elimu ya juu kwa waombaji waliothibitika kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaotoka katika kaya maskini bila kujali mwombaji ametoka shule za Serikali au shule binafsi. Kwa msingi huo, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo imeweka utaratibu wa kuzingatiwa kwa waombaji wote, bila kujali shule aliyosoma ilimradi mwombaji amekidhi vigezo vilivyowekwa ikiwemo ujazaji wa taarifa sahihi.
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA aliuliza:-
Je, hatua gani inachukuliwa kuhakikisha usimamizi, utoaji, urejeshaji wa mikopo 10% ya halmashauri unakuwa wazi na unawafikia walengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Daniel Mburarugaba, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Kagera kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kuhakikisha mchakato mzima wa usimamizi, utoaji na urejeshaji wa mikopo unakuwa wa uwazi na usawa. Utaraibu huo umeainishwa kwenye kanuni na katika mwongozo ambao halmashauri zote nchini zimepatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni, mwongozo pamoja na vitini vya mafunzo vinaelekeza halmashauri baada ya kukusanya fedha kwa ajili ya mikopo zinapaswa kutoa tangazo kwa njia mbalimbali ili kuufahamisha umma. Sambamba na hilo Serikali imeunda mfumo wa kielektroniki wa utoaji na usimamizi wa mikopo ambapo kila mwombaji anautumia kuomba mkopo. Mfumo huu unatumika pia katika usimamizi wa shughuli za vikundi pamoja na kufuatilia marejesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua hii imesaidia kuweka wazi uwajibikaji katika kila hatua ya utoaji wa mikopo, usimamizi na marejesho. Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa kunakuwa na uwazi katika uombaji na utoaji wa mikopo, kama kanuni na miongozo inavyoelekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)