Supplementary Questions from Mhe. Dickson Nathan Lutevele (3 total)
MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali. Kwanza kabisa niishukuru Serikali kwamba Halmashauri ya Mji wa Mafinga ni moja kati ya miji ambayo ilipata Mradi wa Maji wa Miji 28 na mradi huu ilikuwa ukamilike mwezi Juni mwaka uliopita, lakini mpaka sasa hivi mradi huu uko 28% tu ya utekelezaji wake. Ninaomba kauli ya Serikali, je, ni lini mradi huu utakamilika ili wananchi wa Mafinga waweze kupata maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana kaka yangu Mwenezi wa Wilaya na Mbunge wa Jimbo hilo ambaye ameanza kwa kasi kubwa sana, na mwezi mmoja tu uliopita nilikuwa naye kwenye ziara katika jimbo lake, na tulipitia baadhi ya miradi, na mradi ambao ameuongelea ni mradi unaotekelezwa na Jandu Plumbers ambapo ni kweli ulikuwa unasuasua, lakini tuliwaita wakandarasi tukakaa tukakubaliana warudi site waweze kuendelea kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaamini kwamba kwa kadiri fedha ambavyo zitakuwa zinapatikana tutahakikisha tunamwezesha mkandarasi aweze kukamilisha huu mradi kwa wakati. Ninashukuru sana.
MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wafanyakazi hawa wa Kiwanda cha SPM - Mgololo walishinda kesi ya msingi mwaka 2007 na katika kesi hiyo ya msingi Mahakama iliamuru wadai hawa walipwe kwa pande zote mbili, kwa maana ya mwekezaji kwa wale wafanyakazi wachache aliokuwa amewachukua, lakini na Serikali iwalipe wale wafanyakazi 760 ambao walikuwa hawajapewa barua ya kusitishiwa ajira yao na wala hawaendelei na kazi; kwa maana kwamba walikuwa wameachwa hewani. Mahakama ikaamuru kwamba walipwe tokea mwaka 2007.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; sasa je, Serikali haioni kama ipo haja ya kuumaliza huu mgogoro ili Watanzania hawa ambao walifanya kazi kubwa ya uzalishaji katika kiwanda kile, katika kujenga nchi yetu na wao wakapata haki yao ambayo wameitumikia kwa muda mrefu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Rais wetu mpendwa kupitia Bunge hili alisema anatamani wakati anaondoka, angeacha tabasamu kwa Watanzania. Serikali haioni kama ipo haja ya kuumaliza huu mgogoro kwa kuona ni namna gani wanawafidia wafanyakazi wale ambao kwa kipindi kirefu sasa wanaisubiri hii fedha na kiwanda kile kilikuwa kikifanyiwa kazi na Watanzania kutoka nchi nzima na wanashindwa kuondoka Mgololo kwa sababu wamefanya kazi muda mrefu, hawana fedha na hawajapata mafao yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba majibu ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi na utu ndiyo kaulimbiu yetu na tabasamu la utu katika utumishi ni moja ya malengo ambayo tunayafanyia kazi chini ya maelekezo yake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Rais wetu. Kwa muktadha huo, ninaomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lutevele, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaingia hapa kwa sababu yenyewe ndiyo ilikuwa mmiliki wa kiwanda hiki kabla ya ubinafsishwaji wake. Kimsingi ninaomba nikiri kwamba madai haya chimbuko lake ni kupunguzwa kazi kwa baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hiki na mwekezaji ameshalipa madai ambayo yanayomhusu kwa upande wake. Uhakiki ulifanyika kwa upande wa Serikali katika dhana ile ile ya kuacha tabasamu la utu na tayari Serikali ilifikia tamati kwa kupata kiwango cha fedha ambacho ni malipo stahiki kwa watumishi wa kiwanda hicho. Serikali ilitoa fedha hizo katika mwaka 2017 na 2018. Hata hivyo, wafanyakazi hao walikataa kuchukua kiasi hicho kwa madai kwamba ni kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa, Serikali imeshtakiwa na suala hili bado liko Mahakamani na kinachogombewa hapa ni kwamba, kiwango ambacho kimetoka ni kidogo, lakini nia ya Serikali ni kumaliza mgogoro huo ili wananchi hawa wapate haki yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Mji wa Mafinga tulipata mradi wa stendi ambayo ilikuwa ikamilike kujengwa mwaka uliopita, lakini mpaka sasa tunaambiwa kwamba, wakandarasi wapo kwenye hatua za drawings. Sasa naomba nipate kauli ya Serikali kwamba, ni lini stendi hii itajengwa kwenye Mji wa Mafinga ambao mpaka sasa hatuna stendi ya kisasa na tunaihitaji sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, Serikali iliweka mpango kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa katika Mji wa Mafinga na Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mheshimiwa Villa, amekuwa akifuatilia mara kwa mara. Ninaomba nimhakikishie kwamba, kama alivyosema, tayari tuna mkandarasi, lakini kazi haijaanza na tunajua kuna sababu ambazo zimesababisha mkandarasi kutokamilisha kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI pamoja na Halmashauri ya Mji wa Mafinga tuko kwenye hatua za kuhakikisha mkandarasi anarejea kazini, anaanza kufanya kazi hiyo, ili kukamilisha ujenzi wa sehemu hiyo. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kazi hiyo itafanyika.