Supplementary Questions from Hon. Mabula Johnson Magangila (3 total)
MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, je, ni mpango upi wa Serikali wa kujenga kiwanja kikubwa cha kisasa katika Mji wa Kahama ambao unakua kwa kasi sana sasa hivi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mipango hii ya kuhakikisha vile viwanja ambavyo vipo chini ya Halmashauri vinajengwa kulingana na vipaumbele vya Halmashauri na jinsi wataalam wetu wanavyoweza kuibua miradi katika maeneo yao. Kama kitakuwa kipo ndani ya Halmashauri kiwanja hicho, tutaweza kuhakikisha kinajengwa kwa wakati, na kama kipo kwa wenzetu Wizara ya Michezo wataweza kutolea majibu katika swali hilo.
MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Nami naomba niulize swali la nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala. Kwa kuwa, Mji wetu wa Kakola, unakua kwa kasi sana, yaani Bulyang’ulu, ambapo ninafahamu wewe pia ni mwenyeji sana pale, kuna mahitaji makubwa sana ya soko pamoja na stendi. Je, ni lini Serikali itakwenda kuanza ujenzi wa soko na stendi pale Kakola? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mabula, Mbunge wa Jimbo la Msalala kwamba, Msalala ni moja ya halmashauri ambayo inakua kwa kasi na ina wafanyabiashara wengi, na kwa kweli kuna kila sababu ya kuendelea kuboresha miundombinu ya stendi na soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ya Halmashauri, kwa maana ya Halmashauri ya Msalala na Serikali Kuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tutaendelea kufanya tathmini, kuandaa michoro na kutafuta maeneo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi na masoko kwa awamu. Dhamira ikiwa ni kuhakikisha kwamba, huduma hizo zinaboreshwa katika Halmashauri ya Msalala. (Makofi)
MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, Mji wa Isaka ni bandari kavu ndipo ambapo Station ya SGR inajengwa pale katika Mji wa Kahama, je, ni lini Serikali itaweka mpango wa kuujenga ule mji kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, barabara zetu zinaendelea kujengwa kwa awamu, na Serikali imetambua maeneo yote ambayo yanahitaji kujengwa barabara za changarawe, barabara za lami na tunaendelea kutambua maeneo hayo kulingana na uhitaji, na Serikali inatambua kwamba, Mji wa Isaka ni wa kibiashara unaokua haraka.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna station ya SGR, lakini pia, shughuli za kiuchumi zimeendelea kuongezeka. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa awamu na kufanya tathmini ili kuweza kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami au changarawe kwa kadri ambavyo itakuwa inawezekana.