Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mvita Mustafa Ali (1 total)

MHE. MVITA MUSTAFA ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali langu la kwanza linasema; kuna wanufaika wangapi wanawake ambao wamehitimu katika mpango huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili linasema; je, unaweza kuliambia Bunge hali zao hao wanufaika kiuchumi katika mpango huu kwa ujumla wake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa kunusuru kaya maskini ni kuhakikisha kwamba walengwa wanapatiwa uwezo na mwisho wa siku wana uwezo wa kujitegemea. Kwa kufikia hivyo, Serikali imefanya tathmini ya kutosha na kubaini kaya 431,730 ambao tayari wameweza kujitegemea na sasa hawategemei tena ruzuku ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kaya hizo wapo wanawake 757,730 ambao wameweza sasa kusimama na kujitegemea kiuchumi. Hata hivyo, swali lake la pili linasema hali za kiuchumi, hali zao za kiuchumi kwa hawa walengwa ni nzuri na wanaendelea kuimarika kwa kufuatiliwa kwa karibu na mamlaka za halmashauri za vijiji na mamlaka za halmashauri zetu za mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba walengwa waliohitimu baada ya kuwezeshwa wapo, lakini pale walipowezeshwa basi wameendelea kusimama vizuri.

Mheshimiwa Mweyekiti, ninaendelea kutoa wito na kukumbusha halmashauri zetu nchini kwamba waendelee kufuatilia kaya hizi kwa karibu ili kuhakikisha kwamba zile kaya zinaendelea kuimarika lakini waweze kuwaunganisha na fursa zinazopatikana ndani ya halmashauri ikiwemo mikopo ya 10%; 4/4/2 ili waweze kuendelea kujitegemea kiuchumi badala ya kutegemea ruzuku ya Serikali, ahsante.