MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Ikungi Mashariki, kuna visima vingi vilichimbwa, lakini maji hayajaweza kusambazwa katika maeneo mbalimbali. Mfano mzuri ni Kijiji cha Misule, Kata ya Misughaa. Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuhakikisha kwamba wananchi wale wa Kata ya Misughaa, Kijiji cha Misule wanaweza kusambaziwa maji na wanaweza kupata hayo maji ili waweze kuwa na imani ya Serikali yao kwa maana ya kumtua mama ndoo kichwani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa maeneo ya Misughaa, kwanza kabisa Serikali itachimba visima na baada ya kuchimba visima tunafanya pump test na baadaye tunajiridhisha na que ya maji. Tukishajiridhisha na que ya maji, maana yake sasa ndiyo tunafanya usanifu wa kutengeneza mtandao unaoendana na maji ambayo yanazalishwa pale. Kwa hiyo, tukishajiridhisha, baadaye sasa tunayafikisha kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bajeti ya kwanza ilikuwa kuchimba visima, bajeti ya pili ni kusambaza baada ya kujiridhisha na uwingi wa maji yaliyopatikana katika visima. Ninamtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwa vile tumekamilisha uchimbaji wa visima na pump testing imeishafanyika. Sasa tuko kwenye mchakato wa kuingiza katika bajeti ya kuhakikisha kwamba sasa tunaenda kujenga mtandao wa maji ili maji yawafikie watumiaji na wananchi wa Misughaa. Ninakushukuru sana.