Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Chief Thomas Mgonto Kitima (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia japo kidogo kwenye hoja aliyoleta Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kifupi ameweka hoja ambayo imesheheni mambo mbalimbali. Kwa hiyo, ninachukua fursa hii kwanza kabisa kumpongeza yeye, kuipongeza Serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu, kwa hatua kubwa na katika kupanga safu ambayo ndiyo inakwenda kuweka msingi wa awali wa Dira yetu ya Miaka 25 ijayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hoja hii iliyoletwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa, maana ya bajeti ya kwanza kabisa, ndiyo inayoweka msingi imara. Wanasema, nyumba bila msingi imara, hiyo nyumba huenda isiwe imara, kwa maana hiyo, hapa ndiyo tunaanza kuweka ule msingi wa miaka 25 kwa Bunge hili. Bunge hili litaweka historia kama tukiweka msingi wa zege, msingi wa mawe, basi msingi huu ndiyo utakaotuhakikishia hii miaka 25 tunaenda kuivuka vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ziara yake aliyokuwa akiifanya mikoani. Pia, ninatumia fursa hii kumpongeza Mkuu wangu wa Mkoa na Mkuu wangu wa Wilaya kwa sababu, wamekuwa wakitembea kutatua kero na kuzisikiliza. Kwa namna nyingine wameweza kusaidia kuhudumia wananchi wa Mkoa mzima na Wilaya yetu ya Ikungi, ninawapongeza sana na watendaji wote wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye hoja aliyoleta Mheshimiwa Waziri Mkuu, amesema katika dhima hii ambayo ameiita “Mageuzi Katika Kukuza Uchumi na Kuzalisha Ajira” kwa maana ya Mpango wa Nne wa hii miaka mitano, ambayo tunaianza sasa hivi. Tunategemea kwamba, haya yote Waheshimiwa Wabunge waliyozungumza yataakisi haya mageuzi, ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu amekwishayataja, ambayo ni mageuzi katika uchumi, mageuzi katika kukuza viwanda vyetu na mageuzi katika kushirikisha sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaungana na wenzangu kwa suala ambalo wamelizungumza takribani Waheshimiwa Wabunge wote. Waheshimiwa Wabunge wote wameongelea kuhusiana na barabara na ninaanzia hapohapo; tuna Barabara ambayo inatajwa kwamba, inatokea Handeni kupitia Kiberashi – Chemba – Kwamtoro na hapo Singida, ambapo inagusa moja kwa moja Jimbo la Ikungi Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwenye Jimbo la Ikungi Mashariki ni takribani kilometa 40 tu. Katika hizo kilometa 40, kama kweli tunataka kuwasaidia watu wetu, kuna kama kilometa 15 kutoka njia panda, kupitia Unyankhanya mpaka Siuyu na Makiungu. Pale Makiungu kuna hospitali kubwa ambayo mwekezaji huyo amejenga ile hospitali ambayo inahudumia watu kutoka mikoa mbalimbali, Simiyu, Manyara na mikoa ya jirani, lakini ni hospitali ya rufaa, ni hospitali kubwa sana ambapo, hata Serikali mle ndani tuna watumishi wetu ambao wanafanya kazi pale. Pamoja na yote ina upungufu wa watumishi upande wa Serikali, lakini ni hospitali kubwa ya Kitaifa, ambayo inatumika kusaidia hospitali hizi ambazo tunazijua za rufaa, kama Muhimbili, Benjamin, pamoja na Bugando.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiki kipande cha kilometa 15, kama kitawekwa lami, kitasaidia sana kuepusha adha ambazo wanakutana nazo wagonjwa, hasa mama zetu, wanapokuwa pale hospitali, wanapofanyiwa operesheni, wanapojifungua na wanaporudi makwao kupitia hiyo barabara, ina rasta nyingi, yaani ina mashimo mengi makubwa hata inafika wakati ile mishono inafumuka. Hawa wagonjwa wanapata tabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba hii barabara pamoja na kwamba ina urefu wa kilometa 340, hiki kipande cha takribani kilometa 15 kiangaliwe kwa jicho tofauti, kwa sababu huyu mwekezaji amewekeza pale na sisi tuna-promote PPP kwa maana ya ubia kati ya Serikali na sekta binafsi. Kama huyu amekwishawekeza hospitali kubwa pale tena ya rufaa inahudumia watu kutoka mbali, hiki kipande kifupi kuwasaidia hawa wagonjwa wasipate taabu ama wasidhurike na madhara yatokanayo na barabara, ninaomba sana katika hili liwekewe msisitizo mkubwa na hiki kipande cha kilometa 15 kiweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara Wabunge wote inapopitia wamekwishaitaja, Mbunge wa Kilindi juzi alitaja, Mbunge wa Chemba juzi alitaja, lakini Mbunge wa Kiteto naye pia aliitaja na mimi pia kwa kumalizia kwa sababu inaenda kuishia kwangu, ninaomba kama ikiwezekana wapatikane wakandarasi tofauti tofauti; wengine waanzie huko Handeni lakini wengine waanzie hapa Singida pale njia panda ili huduma iweze kupatikana kwa wepesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka toka nipo darasa la nne mwaka 1997 huku, nyumba zilikwishawekwa X muda mrefu sana na kipindi hicho watu wakawa wanajua kuna matumaini makubwa ya kwamba hii barabara inaenda kuwekwa lami na watu wakawa wameshajiandaa kuhama. Bahati mbaya kwa sababu zile nyumba nyingi ni za tope kila mara ile X huwa inafutika na pengine watu wa sasa hivi wasijue kwamba zilishapigwa X. Zimeshapigwa X muda mrefu toka 1997 huko mwaka 2000, mwaka 2005, lakini bado haikujengwa kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Rais tarehe Mosi Machi, 2025 akiwa Handeni aliitaja hii barabara, akaiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wakae wamtafute huyu Mbia ili hii barabara iweze kujengwa. Sasa kama Rais anatoa maagizo, sisi watendaji huku hatuoni kwamba mfalme ameshasema na kauli ya mfalme huwa haipingwi na kauli ya mfalme huwa ndiyo final? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilitegemea kwamba nione Wizara inakimbizina kuhakikisha kwamba hii barabara inajengwa mara moja kwa sababu ni agizo na ni kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa kule Handeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kipindi hapa niliwahi kumshuhudia Mbunge mmoja, kipindi mimi sijaja Bungeni, huyo Mbunge aliwahi kupiga sarakasi hapa Bungeni, baada ya kupiga sarakasi muda siyo mrefu ile barabara yake ikajengwa. Sasa kwa sasa hivi tunaongea kwa upole kwa sababu tunaamini Serikali hii ni sikivu, inaenda kuhakikisha kwamba inasikiliza maombi ya Wabunge wote. Kwa hiyo, sina haja ya kupiga sarakasi kama yule alivyopiga kwa sababu ninaamini watakwenda kuijenga hii barabara ya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza kwa upole ila wakati utakuja tutazungumza kwa nguvu kubwa… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana muda wako umeisha, naomba uunge mkono hoja.

MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana, kwa sababu kuna wakati mwingine tutapata nafasi ya kuzungumza na bado kuna Wizara nyingi, bado hoja ambazo ninazo nitazizungumza wakati huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika mipango na bajeti ambayo Serikali imetuletea siku ya leo. Kwa sababu leo ni mara yangu ya kwanza kuchangia, basi ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii, uhai na kutujalia afya tele sisi wote tulio hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee, ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia fursa ya kuwepo maeneo haya kwa sababu tulipitia michakato mingi kwenye kura za maoni huko na hatimaye tukaingia kwenye uchaguzi mkuu na tukaweza kufika hapa eneo lako hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niwapongeze sana Spika, wewe Naibu Spika, na Wenyeviti wote kwa kuchaguliwa. Zaidi ya yote niwapongeze wananchi wa Jimbo la Ikungi Mashariki kwa kunipatia ushindi mkubwa, kuipatia hii Serikali ya Chama cha Mapinduzi ushindi mkubwa, tukiongoza kwa kura nyingi sana za kishindo na Mheshimiwa Rais akiwa ameongoza sana katika Jimbo la Ikungi Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachangia Mpango elekezi wa Maendeleo wa Muda mrefu; Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo ya Taifa miaka mitano; Mapendekezo ya Mpango wa Taifa kwa mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti katika muda wa kati (2026/2027 hadi 2028/2029).

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kwa namna mawasilisho yaliyowekwa Mezani, ni mawasilisho mazuri ambayo yanavutia na kila mtu akiyasikiliza anapata hamu ya kuona utekelezaji wake unafanyika haraka. Kila mtu anashawishika kuona kwamba, kama kweli hii mipango ambayo iko Mezani itatekelezwa kwa asilimia zote, basi Tanzania itaenda kuwa nchi yenye uchumi mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia mipango inasema, pato la Taifa (GDP) inaweza kufikia dola za Marekani trilioni moja, lakini pato la mtu mmoja mmoja linategemewa kufikia dola za Marekani 7,000 ifikapo 2050. Sekta binafsi inatakiwa kuchangia 70% ya gharama ya Mpango. Kwa mantiki hiyo, unaona ni namna gani haya mawasilisho yalivyo mazuri na kama yataenda ipasavyo, basi tutafikia hiyo dira ambayo tunaitazamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna angalizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia hotuba yake aliyoitoa mwezi Novemba ambapo alisema, ninaomba ninukuu: “Watendaji msipobadilika kuendana na matarajio ya wananchi tutawabadilikia.” Kwa maana gani? Hii mipango tayari ni kifungo. Hii mipango tayari inatuweka katika mazingira ya uwajibikaji. Inaitaka Serikali iwajibike kwa kadiri ya namna tulivyopanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, Mheshimiwa Rais amesema, kama watendaji hawatabadilika kuanzia Mawaziri mpaka viongozi wa ngazi za kata na vijiji, kama hawatabadilika na hawataendana na kauli za Mheshimiwa Rais, ina maana hii mipango huenda isifanikiwe. Hata hivyo, tunategemea kwa namna Waziri wa Fedha alivyowasilisha na Waziri wa Mipango alivyowasilisha tunategemea haya mambo yataenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijikite nianze moja kwa moja kwenye sekta ya elimu. Tunafahamu kabisa ya kwamba katika maendeleo yoyote lazima uwezo wa watu uweze kujengwa. Watu wanatakiwa wajengwe kupitia elimu. Sasa je, elimu yetu kwa wakati huu ikoje? Tunaweza kuona kwamba mwaka 2007 tulikuja na Sera ya Elimu kila Kata, lakini hatujaendelea mbele zaidi ya hapo na tuna mpango wa maendeleo mpaka mwaka 2050.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa ninashauri, sasa twende mbele zaidi, tuwe na mawazo ya kujenga shule za sekondari kila kijiji, tuwe na mawazo ya kujenga shule za msingi kila kitongoji, ili hawa watu wapate elimu. Kwa sababu tukiangalia tu, tukibakiza hizi shule zetu za kata ambazo sasa hivi zinafanya vizuri; na ninamshukuru Mkuu wangu wa Shule Bwana Mtoi amefaulisha shule yetu ya Siuyu imefanya vizuri kwa mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama tutaishia kwenye kata, ina maana kuna watu wengi tutawaacha na tukumbuke kwenye elimu kuna watu wakimaliza Darasa la Saba tunawaacha pembeni. Kuna watu wakimaliza shule ya sekondari tunawaacha pembeni, na wengine wakimaliza Form Six tunawaacha pembeni, wale ambao hawabahatiki kuendelea. Sasa Mpango huu unatakiwa uje na mawazo ya kuhakikisha kwamba hakuna mtu hata mmoja anayeachwa nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mtu aingizwe kwenye Mpango. Yule anayeachwa darasa la nne, yule anayeachwa darasa la tano, yule anayeachwa form four, anayeachwa form six, anayeachwa chuo kikuu wote waingie kwenye Mpango, wahusishwe kama vile mpango unavyosema mpango jumuishi na ushirikishwaji… (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Thomas kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI).

TAARIFA

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na mpango wa kujenga shule za sekondari kwenye kila kata Tanzania nzima, maeneo yote ambayo kata hizo hazina shule za sekondari. Siyo hivyo tu, nchi hii ina vijiji 12,261, lakini tunazo shule za msingi zaidi ya 15,000 hiyo ni kumaanisha kwa uwiano ni karibia kila kijiji kina shule ya msingi na tunaendelea kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa, tunajenga shule ya msingi kila palipo na shule ya sekondari. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka shilingi trilioni 1.3 kupitia Mradi wa SEQUIP kwa shule za sekondari na ameweka zaidi ya shilingi trilioni 1.13 kupitia Mradi wa BOOST kwa shule za msingi. Kwa hiyo, mpango anaouelezea ndiyo tunaoendelea kuutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Thomas Taarifa unaipokea?

MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana, ninapokea taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba speed iwe kali ili maneno ya Mheshimiwa Rais ya kwamba watendaji wasipobadilika, basi watabadilishwa. Kwa hiyo, ni jambo zuri alilozungumza, lakini mimi nitilie mkazo kwamba kila kijiji ijengwe shule ya sekondari kwa sababu sasa hivi wanafunzi ni wengi. Hizo shule za msingi sasa hivi zielekezwe kwenye vitongoji, ndiyo hoja yangu ilikuwepo hapo, kwa sababu, sasa hivi wanafunzi ni wengi na shule sasa hivi zimeelemewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiangalia sasa hivi shule ambazo tuko nazo hata madawati hayatoshi kwa sababu wanafunzi ni wengi sana. Pia, hata madarasa na yenyewe hayatoshi. Kwa hiyo, kama Serikali itaelekeza elimu kwa kila kitongoji, shule za msingi zikajengwa na kila sekondari ikaenda kila Kijiji, tutakuwa tumesaidia sana kwenye suala la elimu na watu wetu watakuwa wamepata maarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni katika sekta ya ujenzi. Ninaomba nichangie hapo. Tunaona katika bajeti zetu za kila mwaka, sekta ya forodha huwa inachangia sehemu kubwa sana. Sasa ili sekta iendelee kuchangia vizuri na iweze kuleta pato kubwa la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi bado ninatilia mkazo yale ambayo yapo kwenye Mpango, kwamba zile bandari kavu, kwa mfano, Kwala ambayo tumeainisha, lakini kuna maeneo mengi hapa nchini Tanzania, hata mkoani Singida. Kuna shida gani kujenga bandari kavu Mkoa wa Singida? Kujenga bandari kavu karibu kila maeneo itasaidia kuondoa congestion pale Dar es Salaam. Zile bandari ambazo tunazijenga ya Bagamoyo, Tanga, na Mtwara, lakini bado hazipumui kwa sababu hatujatoa matoleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi ushauri wangu ni kwamba tujitahidi kadiri tuwezavyo tujenge bandari kavu maeneo mbalimbali, ili kuachia zile sehemu ambazo zinapokea mizigo ili papumue na mizigo mingine ipokelewe katikati mwa nchi hata hapa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni katika sekta ya kilimo na ufugaji. Mipango yote imetajwa vizuri, lakini kwenye sekta ya kilimo na ufugaji haijataja vizuri, na sijaona kipengele ambacho kimetiliwa mkazo kwenye ufugaji. Ukumbuke watu wetu hawa ni wakulima na wafugaji kwa asilimia kubwa na tumeona hapa kilimo ni almost 70%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ndivyo ilivyo, mimi nilikuwa ninafikiria masuala ya mifugo yawekwe katika namna ambayo hawa watu wanaweza wakafuga kisasa. Kwa mfano, tuna shida kubwa sana ya majosho kwenye maeneo yetu. Tuna shida kubwa sana ya mabwawa, ikifika miezi ya kiangazi hasa mikoa yetu, unakuta mifugo inaanza kufa kwa sababu ya kukosa malisho na kukosa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sekta hii ni muhimu kweli kweli. Ukitaja sekta ya kilimo, inaenda sambamba na sekta ya ufugaji, kwa sababu watu wetu ndio wakulima na wafugaji. Sasa nilikuwa ninaomba tuhakikishe ya kwamba pamoja na kwamba tuna dira nzuri, tuhakikishe ya kwamba hii sekta tunaipanua kuhakikisha kwamba watu wetu hawa wanajengewa mabwawa karibu na maeneo yao, wanasaidiwa katika masuala ya malisho ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakinii lingine la kumalizia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa, muda wako umeisha.

MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)