Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Asha Hussein Saleh (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ASHA HUSSEIN SALEH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia neema ya uhai kuweza kufika hapa tukiwa wazima wa afya. Pia, ninapenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuchaguliwa na wananchi kwa 98%, ili kuweza kuiongoza Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika wananchi wamefanya maamuzi sahihi, kwani wameamua maendeleo. Wamechagua maendeleo kwani Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni shupavu na mbobezi wa kuweza kuiletea maendeleo Nchi ya Tanzania. Kwa vile, ukiangalia, ameweza kumtua mama ndoo kichwani pamoja na mtoto, ameweza kuwekeza katika vituo vya afya pamoja na kuimarisha diplomasia ya uchumi ndani ya Tanzania na kuendeleza katika sekta ya usafirishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya haya kwa kujua kwamba, hili ndilo suala linaloweza kusababisha kukua uchumi wa Taifa letu, pamoja na kipato cha wananchi na kuwaondolea shida wananchi wake. Aidha, ninapenda pia, kumpongeza Dkt. Hussein Ali Mwinyi na yeye kwa jitihada zake za kuleta maendeleo ndani ya Nchi ya Zanzibar. Hakika amefanya mengi ndani ya Jimbo la Fuoni katika kutuletea elimu bora na shule za ghorofa, hospitali, pamoja na kutujengea barabara zinazopitika kwa kila kona ndani ya Jimbo la Fuoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuishukuru Kamati Kuu. Kwa vile ni mara ya kwanza kusimama katika Bunge hili Tukufu, ninapenda kuipongeza Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi kwa kupendekeza jina langu, ili kuweza kugombea na leo hii kuwa Mbunge wa Jimbo la Fuoni. Pia, bila kusahau, ninawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Fuoni kwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi na kusababisha leo hii kuwepo ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba nijelekeze katika mchango wangu kwa Ofisi hii ya Waziri Mkuu, nitachangia katika suala la mazingira. Jimbo la Fuoni limejaliwa kupata bahari na niliposoma wasilisho la Waziri Mkuu, amezungumza juu ya mazingira na tabianchi na sisi pale Fuoni tunayo bahari, lakini pia, Waziri Mkuu alisema ametoa mafunzo, pamoja na kuwanunulia boti wananchi ambao wanahusiana na idara ya mazingira. Kwa hiyo na sisi pale Fuoni kwa kuwa, tunayo bahari na pia, tunaathirika kwa kiasi fulani na mazingira, basi ninachukua fursa hii kumwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwapatia vijana pale wavuvi ambao wanajielekeza katika ufugaji wa kaa, awapatie mafunzo, pamoja na boti, kama alivyoelekeza ndani ya hotuba yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la mazingira pia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa Makamu wa Rais alitembelea ndani ya Jimbo la Fuoni kujionea hali halisi ya wafugaji wa kaa. Kwa hiyo, sasa ninamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa vile na yeye anatembelea Tanzania nzima kupokea changamoto, basi atembelee katika Jimbo la Fuoni. Aje kuwaona wananchi wa pale wanaofuga kaa, apokee changamoto zao na suala hili kwa vile lipo ndani ya ofisi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa hapo hapo katika hiyo idara ya mazingira, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aweze kutembelea katika Jimbo la Fuoni, katika Wadi ya Fuoni Mambosasa kwa sababu, kule tuna Bonde la Jangamizini, ambalo linajaa maji na wananchi wake wanahamahama. Wakati mwingine linasababisha hata watoto wadogo wanaweza kufariki kwa kupita katika eneo lile. Eneo lile ni sugu katika kujaa maji pale, basi ninaomba kupitia Bunge hili Tukufu, Mheshimiwa Waziri Mkuu afanye ziara mahususi ili aweze kututatulia changamoto zilizoko pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa busara na hekima zake za kuweza kutenga shilingi bilioni 200, kwa ajili ya vijana. Shilingi bilioni 200 hizi Mheshimiwa Rais alizielekeza ili kuweza kutatua changamoto za ajira, vijana pamoja na wanawake. Kutokana na vijana wenyewe kutojua au kuweza kuwa na ule uelewa wa kufanya katika kuomba yale maombi imefikia mpaka zoezi lile limefungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi ninaiomba Serikali kwa makusudi mazima kuweza kulifungua dirisha hili la maombi ya fedha zile za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu, ili waweze na wao kujitatua kiuchumi, kwani vijana hawana ajira, lakini fedha zile zimetegwa kwa ajili yao. Likifunguliwa dirisha hili, basi wananchi, vijana na wanawake, hususan vijana wa Jimbo la Fuoni watachangamkia fursa hizi za kuweza kuomba mikopo hii ili waweze kujinasua kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijielekeze kidogo katika eneo la usafiri yaani barabara. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria; tulipata fursa ya kutembelea Mkoa wa Geita katika Mji wa Nyang'hwale, tulikwenda pamoja na Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete. Katika ziara ile tulipokuwa tunalekea Mji wa Nyang'hwale, basi ilikuwa kusema kweli ni guburu guburu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, guburu guburu tangu tunaingia ndani ya Mji wa Nyang'hwale mpaka tumefika Nyang'hwale. Kama tunavyojua Mji wa Geita ni wa madini, ambapo wapo wawekezaji wadogo wadogo. Ripoti ya Waziri Mkuu imesema kwamba, sekta ya madini kwa Julai, 2025 mpaka Januari, 2026 imekusanya mapato ya 64.3%. Kwa hiyo, Mkoa wa Geita unachangia pato hili la Taifa. Basi ninaiomba Serikali kwa makusudi mazima iweze kuwajengea barabara Mji wa Nyang'hwale kwa sababu, barabara yake ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajielekeza katika suala la Muungano. Ninawapongeza kwanza Waheshimiwa Marais wetu wawili walioadhimisha suala hili. Ninampongeza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume kwa kuanzisha suala hili. Kwa kweli, suala hili ni zuri na kama wana wa Tanzania basi inatupasa kudumisha na kuuenzi Muungano huu kwa nguvu na hali zote. Zile kero za Muungano zilizobaki, basi ninamwomba Waziri Mkuu aweze kuchukua juhudi za makusudi, ili kuweza kumaliza kero hizi za Muungano. Baada ya hapo naomba nijielekeze kwenye Mfuko wa Jimbo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Asha, muda wako umekwisha.

MHE. ASHA HUSSEIN SALEH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalize kwa dakika moja. Katika Mfuko huu wa Jimbo, basi ninaomba idara zinazohusika watume kwa wakati, Wabunge tunapopeleka miradi yetu waweze kututekelezea kwa wakati, ili fedha hizi za Mfuko wa Jimbo zisiweze kukutana na fungu lingine linalokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Fuoni, ninaunga hoja kwa asilimia mia moja.