MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa mradi huu umechukua muda mrefu na mkandarasi ameshafanya kazi zaidi ya shilingi bilioni 4.5 na amelipwa shilingi bilioni 1.5, je, nini mkakati wa Serikali wa kupeleka fedha ili huyo mkandarasi arudi kazini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa kuna miradi ambayo imefikia 98%, Mheshimiwa Naibu Waziri anaifahamu, Mradi wa Iseni, Nyang’hanga, Mradi wa Mwarina – Mwamabanza – Salong’we, lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kumalizia hizo asilimia ambazo zimebaki ili wananchi waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Boniventura Kiswaga, Mbunge mahiri kutoka Mkoa wa Magu katika Jimbo la Magu, kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya ya kuwatetea hasa katika kumtua mama ndoo kichwani ambayo ni falsafa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikiri kwamba Mheshimiwa Mbunge ni mfuatiliaji mzuri sana na kwa mantiki hiyo, hivi sasa ninayo maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso kuhakikisha mradi huu na mkandarasi huyu ndani ya malipo ya mwezi huu tuhakikishe kwamba analipwa. Ndiyo mkakati wa kuhakikisha kwamba tutaendelea kumlipa mpaka pale ambapo fedha zote zitakuwa zimeshalipwa ili mradi uweze kukamilika. Hivi sasa mradi uko 65% na tunaamini kwamba akishalipwa atarudi site.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, mpaka sasa mkandarasi tumeshamwita hapa Dodoma, leo tutakuwa na mazungumzo naye ili tuhakikishe tutakapolipa hizi fedha, arudi site moja kwa moja ili tukaone sasa matunda ya kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi mingine ndani ya Jimbo la Magu ambapo ni matokeo ya kazi nzuri sana ya Mheshimiwa Mbunge. Tunayo miradi takribani sita, ukiwemo wa Lugeye. Miradi hii kwa jumla yake kuna uwekezaji mkubwa sana wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya shilingi 18,000,000,000 zimewekezwa pale, na pia miradi ya Nyang’hanga, Iseni, Sagani, Misungwi, Mahaha, Nsola, Bubinza yote hiyo iko katika hatua mbalimbali. Mmoja upo 90%, mwingine 98%, mwingine uko 65%, mwingine uko 50%. Tunaamini kwamba tukiendelea kupeleka fedha, miradi hii itatoa matokeo kwa haraka sana. Nakushukuru sana.