MHE. MARIRTA G. KIVUNGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Je, ni Serikali itakamilisha zoezi la kufikisha umeme kwenye vitongoji vilivyosalia katika Wilaya ya Longido na hasa kwenye vyanzo vya maji?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote ndani ya nchi yetu vinapata umeme. Nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali tutafika kwenu na tutakapopata fedha, tutahakikisha kwamba vitongoji hivyo alivyovitaja vianapata umeme na Mheshimiwa Mbunge atakuwa ni sehemu ya watu ambao tutakwenda kuzindua kuwasha umeme kwenye vitongoji hivyo. Ahsante.
MHE. MARIRTA G. KIVUNGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, je, ni lini barabara ya lami ya kutoka Elerai – Kamwanga, Wilayani Longido itaanza kujengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge na ninaomba tu nimhakikishie kwamba barabara zote za kimkakati ambazo zina umuhimu mkubwa wa shughuli za kiuchumi na kijamii katika halmashauri zetu kote nchini, ikiwemo Halmashauri ya Longido zinaendelea kutengewa fedha kwa awamu ili kuhakikisha kwamba zinajengwa aidha kiwango cha changarawe au kiwango cha lami kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Kwa hivyo, nimkuhakikishie kwamba hiyo barabara itaendelea pia kutengewa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, kumuelekeza meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Longido, kuifanyia tathmini barabara hiyo na kuwasilisha mpango kazi ambao wame-internalize ndani ya mkoa na sisi ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tuweze kuona namna ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.