Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kakulu Burchard Kakulu (1 total)

MHE. KAKULU B. KAKULU: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwanza kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pia nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbagala kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoiongoza kwa kutusaidia kujenga ile barabara. Kwa kweli ilikuwa ni changamoto kubwa, ilisababisha msongamano mkubwa na ajali nyingi katika Kilima kile cha Mto Kizinga. Kwa hiyo, tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu hayo mazuri, swali moja tu la nyongeza. Ninafahamu na wote tunajua umuhimu wa barabara inayounganisha pale Kongowe kutoka Kongowe kuelekea Kivukoni katika Jimbo la jirani la Kigamboni, na umuhimu wake hasa katika kulisha viwanda vilivyopo Kigamboni katika eneo la Kisarawe II na viwanda vilivyopo katika eneo la Mwandege pamoja na eneo la Mkuranga.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali inaona umuhimu pia wa kupanua hii barabara kutoka Kongowe kwenda Kigamboni ili kusaidia kuhudumia hivi viwanda na shughuli nyingine za wananchi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee pongezi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, kwa kutambua kazi kubwa ambayo anaifanya na hasa kuondoa changamoto ya msongamano wa barabara kwenye eneo hilo ikiwa ni pamoja na kulijenga hilo daraja la Mzinga ambalo muda siyo mrefu tunaanza kulijenga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, hii barabara ya Kongowe kwenda Kivukoni ipo kwenye mpango wa kuondoa misongamano (decongestion) ya miji ikiwepo Mji wa Dar es Salaam ikiwepo pamoja na hiyo barabara ya Kongowe – Kivukoni.