Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Timoth Geofrey Anyosisye (2 total)

MHE. TIMOTH G. ANYOSISYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tarehe 29 Oktoba, 2025 Jimboni Kawe vilichomwa Vituo vya Polisi vitatu. Kwetu sisi Wanakawe jambo hili tunalichukulia kama jambo la dharura. Je, ni lini Serikali itajenga vituo hivi ili kurejesha hali ya huduma ya kipolisi katika maeneo husika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninaomba nimjibu swali lake Mheshimiwa Timoth kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tarehe 29 Oktoba, 2025 kulitokea uharibifu wa mali mbalimbali za Serikali ikiwepo baadhi ya Vituo vya Polisi katika baadhi ya maeneo. Ninaomba nimwambie Mheshimiwa Timothy kwamba Serikali inaendelea kukamilisha kazi ya tathmini na kuja na mpango wa dharura wa kuona namna gani ya kuweza kurejesha huduma kwenye maeneo husika. (Makofi)
MHE. TIMOTH G. ANYOSISYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi, Jimbo la Kawe changamoto yetu kubwa ni miundombinu ya barabara. Barabara ya Ukwamani - Kwa Mapupu - Kanisani KKKT, Kata ya Kawe, lakini pia barabara ya Kwa Shokoronda na Mongela inayounganisha kata mbili; Kata ya Makongo na Mbezi Juu, na pia barabara inayotoka Bunju A inayopita Kata ya Mabwepande pamoja na Bunju ambayo inaenda hadi Kata ya Wazo pamoja na Kata ya Goba zimekuwepo kwenye mpango wa kujengwa muda mrefu, lakini zimekuwa zikiahirishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanakawe wanataka kujua je, ni lini barabara hizi zitajengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zote ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam likiwemo Jimbo la Kawe, barabara za Mheshimiwa Timoth ambazo ameziongelea miundombinu yote hii tutaitekeleza chini ya Mradi wa DMDP2. Tulianza na DMDP1 tukajenga barabara nyingi sana, na hivi sasa tunakwenda kujenga mtandao wa barabara wa karibia kilometa 257 chini ya Mradi huu wa DMDP2 na barabara hizo anazotaja kwa hakika zitafikiwa.