Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii tena. Awali ya yote nitoe shukrani kwa Mwenyezi Mungu aliyenijaalia afya njema na leo nipo hapa. Pia nitoe shukrani kwa wananchi wangu wa Jimbo la Ukonga kwa maamuzi sahihi ya kunichagua kuwa mwakilishi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kupongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais, ni hotuba nzuri ya kiutu uzima yenye kujali yenye kuthamini watu wake. Hakika ni hotuba ambayo inatoka kwa mama mwenye kuwa na sifa ya kuwa mzazi na mzazi ana sifa ya ulezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uzuri wa hotuba hiyo, Mheshimiwa Rais siyo mtendaji wa kila eneo. Ili Mheshimiwa Rais vazi ambalo amelivaa kwenye hotuba hii, vazi ambalo limempendeza liweze kuendelea kuwa vazi zuri mbele ya macho ya Watanzania, ninawaomba wasaidizi hasa Mawaziri, Manaibu wao, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na watendaji wengine waweze kuendelea kumvisha vazi hili Mheshimiwa Rais kwa kutekeleza haya ambayo Mheshimiwa Rais amewaahidi Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa watachukua vyeo hivyo kama sehemu ya show, maana halisi ya hotuba ya Mheshimiwa Rais haitaonekana na tutajikuta na mwaka kesho tunakuja tukiwa tunarudi kwenye changamoto hizi hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninatoa wito sana huo na ninampongeza tena Mheshimiwa Rais. Nimeona Mawaziri wengi ni vijana; pia Mawaziri wengine wengi ni akinamama. Ninaomba watambue Mawaziri na Manaibu wao kwamba huko mitaani kuna wananchi wengi wamekaa wanaishi kwa matumaini kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, ninaomba wanapokaa kwenye vikao wafikirie kwamba huko watu wanasubiri matarajio ya Mheshimiwa Rais, wakiishi kwa imani. Kwa hiyo, ni vizuri waangalie hapo. Vinginevyo tutarudi hapa kuulizana mara mbili mbili wapi wametekeleza kama Mheshimiwa Rais alivyotuletea wito wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo na kuwaomba ndugu zangu hao Mawaziri na Manaibu na Makatibu Wakuu, ninaomba nijikite kwenye sehemu mbili:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya kwanza ni katika kitabu hiki cha hotuba ya Rais ukurasa ule wa 23 unaozungumzia habari ya urasimishaji maeneo ya makazi. Katika Jimbo langu la Ukonga, hasa Kata ya Zingiziwa, Chanika, Buyuni, Pugu na Pugu Stesheni, kumekuwa na changamoto zisizoisha zinazotokana na mkwamo wa Mradi wa Urasimishaji Ardhi, mradi ambao ukiongea na baadhi ya wazabuni wanazungumza kwamba unatokana na migogoro ya mipaka baina ya Halmashauri ya Wilaya ya Ilala na Wilaya ya Kisarawe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hapa ni kama watu tunagombea fito moja na huu mradi unavyochelewa pia Serikali inachelewa kupata mapato kutokana na urasimishaji ardhi. Ninaomba kwa sababu Kisarawe ni Tanzania, Ilala ni Tanzania, mamlaka inayotawala ni moja hebu watuondolee huu mvutano usiokuwa wa lazima kwetu ili wananchi waweze kupata hii huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili liwezekane, ni viongozi niliowataja miongoni mwao wenye dhamana ya hii kitu waweze kukaa kumaliza hili tatizo ambalo ni la muda mrefu. Nami pia ni mhanga wa matatizo haya ya mipaka kati ya Kisarawe na Ilala. Eneo ninaloishi Pugu Kajiungeni mguu mmoja upo Ilala mguu mwingine upo Kisarawe, lakini unapofika kwenye utendaji wa Kiserikali wao kwa wao wanavutana, Kisarawe wanavuta, Ilala wanavuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana tuangalie namna ya kuondokana na hiyo hali ili kweli tuweze kuishi kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais nina hakika Rais wote tunampenda ni Rais wetu wa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua inayofuata ni Kifungu ukurasa wa tisa: ukurasa wa tisa unazungumzia Sheria ya Uchaguzi wa Wabunge inayoeleza kuwa mashauri yote ya uchaguzi yatafunguliwa kwenye Masjala ya Mahakama Kuu ambapo jimbo husika la uchaguzi lilipo. Kwa maana ya kwamba ukiwa unapinga matokeo, basi utachagua unafungua kwenye Masjala ya Mahakama Kuu katika Jimbo lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kwa upande wa Zanzibar Mahakama Kuu ya Tanzania haina Masjala. Hivyo basi, hali hiyo hutoona kuwa hilo nalo ni sehemu ya kero ya Muungano na inafifisha upatikanaji wa haki hasa suala zima la uchaguzi, ukizingatia kwamba sheria ama miongozo inasema tufungue kesi mahali ambapo Masjala Kuu ilipo na kule Zanzibar Mahakama yetu ya Tanzania haina masjala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kinachofuatia hapo ni kwamba wananchi ambao wanakuwa na haki ya Kikatiba ya kukata rufaa kwenye vyombo vyetu vya kisheria wanashindwa kuitekeleza kwa sababu huo mlango wako umefungwa. Hivyo basi, ninavyoona kwa maslahi mapana ya Taifa letu na tumeona habari ya Muungano unavyosifiwa na kadhalika. Hili nalo tulione ni sehemu ya kero. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba pia watu wenye dhamana ya jambo hili waliangalie kwa mapana yake, kwamba kuna mlango watu wanakosa sehemu ya kupumulia. Kama unavyojua Waswahili wanavyosema, paka ni mnyama dhaifu sana, lakini ukimfungia kwenye chumba na wewe ukajifungia humo ndani ukafunga mlango, paka anageuka kuwa adui mkubwa sana wa mwanadamu. Ninaomba tufungue milango ili hiyo ahadi iweze kukaa sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo ninashauri kwa umuhimu wa pekee wakati tunasubiri mchakato wa Katiba Mpya kama Mheshimiwa Katibu Mkuu wetu alivyosema hapa, ni vizuri hili jambo liingizwe makusudi kwenye mchakato wa Katiba marekebisho madogo ili tuweze kuwapa haki Wazanzibari ambao imenyimwa ama imefungwa kwa mujibu wa miongozo ya makao makuu yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeweka nia ya kuleta hoja binafsi juu ya jambo hili ili tufikie mustakabli mzuri wa Taifa letu, kwa nia ile ile ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais juu ya uendeshaji wetu wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze pia sehemu ndogo. Hapa nilipokuwa nimekaa wananchi wangu wamenikumbusha na nilikuwa ninaongea na Naibu Waziri wa Ujenzi, lakini nimeongea na Naibu Waziri upande wa DAWASA na kadhalika, suala la Barabara yetu moja ya kutoka Pugu Kajiungeni – Pugu Kirumba – SGR.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile ni ya vumbi japo Naibu Waziri ametwambia kwamba ina mpango wa kutengenezwa kwa lami. Katika kipindi hiki ambacho tunasubiri barabra hiyo ya lami, pale yanapita magari makubwa malori, yanapita na mizigo na ile barabara ni ya vumbi na ni katikati ya makazi. Tumekuwa na shida ya vumbi, nyumba za pale zimechoka. Wakazi wa pale wako hatarini kupata TB. Hali yao si nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa makusudi kabisa, wakati Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana wanaendelea kuchakata mpango wa kupitisha lami, basi upatikane mpango mahsusi wa makusudi. Aidha, pawe panamwagiwa maji kila siku ili vumbi liwe halipo, ama malori yale ya mradi yahamishwe badala ya kupita njia ile basi yazungukie Kilitex kutokea kwenye barabara ya lami ya Nyerere kuja huku yanakoelekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha, lakini mwisho wa yote nifunge kwa kusema Taifa letu amani yetu. Ninaomba wote kwa pamoja tuishi katika maneno kama hayo. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi hii. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia afya njema. Pia nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uteuzi mzuri wa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Niseme wazi kwamba, mimi ni muumini wa utendaji na ziara; watanisamehe Waheshimiwa, ninakohoa kidogo; za Mheshimiwa Waziri Mkuu na maelekezo anayoyatoa; na ananikumbusha enzi na Mheshimiwa Waziri aliyepita muda wake juu ya maagizo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri; ili nchi yetu iweze Kwenda Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mmoja katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania na wasaidizi wake wa karibu ni Waheshimiwa Mawaziri na Waheshimiwa Manaibu wao wakisaidiwa na watendaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haipendezi na haileti sura nzuri kwamba mambo ambayo yanaweza yakamalizwa na Waheshimiwa Mawaziri yanaweza yakamalizwa na Makatibu Wakuu, yanaweza ya kamalizwa na Wakurugenzi, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya yanasubiri hadi Mheshimiwa Waziri Mkuu afanye ziara ndipo wananchi waende wakalalamike kwake. Ili tuweze kuvuka ni lazima tuambiane ukweli, tusimchoche Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu ni binadamu kama tulivyo sisi. Sasa tumpunguzie hizi ziara kwa kumwekea wepesi wa watendaji chini kutenda haki. Nina hakika tukifanya vizuri Mheshimiwa Waziri Mkuu atapata nafasi nzuri ya kufanya tathmini kwa vyombo vyake. Pia itampa nafasi Mheshimiwa Rais kuona kwamba alifanya chaguo sahihi na hivyo kwenye Serikali inayojali wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi hapa nilimsikia Mheshimiwa Waziri wa Maliasili akizunguka mambo mbalimbali. Niweze kusema tu kwamba nilipata nafasi ya kuteta naye kidogo na amenihakikishia kwamba changamoto zilizopo kwenye Jimbo langu la Ukonga, hasa Kata za Buyuni, Chanika na Zingiziwa inayotokana na mipaka ya Hifadhi ya Kazimzumbwi, Mheshimiwa Waziri amenipa uhakika kwamba tunaenda kulimaliza baada ya kuwa limejadiliwa kwa muda mrefu sana, kwa zaidi ya miaka mitatu kwenda nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nitoe shukrani kwa Mheshimiwa Spika wetu kwa kuonesha msimamo katika jambo letu hili na wajibu wetu kama Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kutokana na hali ya polisi wetu nilipata nafasi ya kutembelea Jimbo langu la Ukonga hizi siku chache za mapumziko na kufanya ziara kwenye Kituo cha Polisi cha Wilaya Chanika. Kituo cha Polisi cha Wilaya Chanika kinahudumia zaidi ya kata nane kwenye jimbo langu kinahudumia kata tatu. Kwa kweli kituo kile kina uhaba mkubwa wa magari kwa ajili ya kutuhudumia sisi wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kile kina gari moja maalum kwa ajili ya doria na gari moja ya kiutawala; na hiyo gari moja lililobaki ni bovu, ambapo kwa maelezo ya kaimu OCD ambaye nilimkuta pale ofisini, imekuwa ikitengenezwa mara kwa mara, kwa hiyo imekuwa inapoteza ufanisi katika kutekeleza majukumu yake. Kwa hiyo ningeomba tu kwamba Serikali iangalie kwa jicho la pili umuhimu wa kuongezea gari mpya kile Kituo cha Wilaya cha Polisi pale Chanika. Kituo hiki ni muhimu sana kwa watu wa huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la huduma za afya. Nimekuwa ninalirudia, hii ni mara ya pili. Ninalirudia hili kwa sababu inawezekana, au ninaamini kuwa Serikali ilifanya uamuzi sahihi kuweka au kufuta tozo ama gharama za kuchangia matibabu kwa watoto wa miaka zero hadi mitano na akinamama wajawazito. Ninaamini imefanya uamuzi sahihi. Hata hivyo, huko chini hicho sicho kinachotekelezeka. Nimeuliza hili kwa sababu katika ziara yangu siku chache hizi nilitembelea hospitali mbili zipo katika jimbo langu na nimekuta matendo haya bado yanaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia katika ziara zangu tulimtembelea mzazi mmoja, alikuwa na mtoto mdogo mwenye miaka mitatu akiwa na kadi ya kliniki. Alivyofika hospitali bado alichajiwa fedha shilingi 10,000 kwa ajili ya vipimo. Hadi nilipoingilia kati ndipo ikaonekana kwamba hatakiwi kulipia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea pia na kituo kingine cha afya pale kwetu, changamoto hizi zipo. Nimekuwa nikizungumza hapa mara kwa mara, kwamba wakati mwingine Serikali inaweza ikawa inachelewa kuweka fedha, lakini wakati mwingine watendaji wetu huko chini wanakuwa changamoto. Sasa sielewi, kwamba hawa watendaji; baadhi yao, si wote; vichwa ni vigumu ama tunakwama wapi? Kwa sababu Serikali ni ya umma, hospitali ni ya umma, kodi ni za umma, Serikali yetu inaiongozwa na Chama Cha Mapinduzi ama iliyoundwa na Chama Cha Mapinduzi imeweka Ilani ipo wazi, watu watibiwe bure, shida iko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule chini kuna Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wa Kata, wa Jimbo, wa Wilaya na wa Mkoa. Viongozi wa vyama vyetu ndiyo viwanja wetu, wanashindwa nini? Sasa ningeomba tufikie mahali sasa, Bunge litamke ama Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu itueleze wazi, kwamba tunadanganywa? Kama Serikali imeamua, tunakwama wapi ilihali sisi ni wawakilishi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa sitegemei na wala hakuna Mheshimiwa Mbunge atategemewa kuleta taarifa za uongo hapa, tunatoa tarifa za ukweli na tuna ushahidi nazo. Sasa ninaomba hili nalo lifikie mwisho. Ni aibu kwa Tanzania yetu, tunazungumzia habari ya afya kwa akinamama wajawazito, habari ya afya kwa watoto wetu, bado tukienda huko chini wanatozwa, hii ni aibu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili pia la watu wazima wenye miaka 60 na kuendelea; hivi bado tunahitaji mganga wa kienyeji kupiga ramli kwamba huyu mzee anakuja mezani kwako daktari akiwa na kadi yake ya NIDA inaonyesha umri wake ni miaka 60 plus, unamwambia bado aje na barua ya msamaha? Hapana, ninaomba tubadilike, twende kwenye kutafsiri matendo yetu. Tukifanya hivi hata kelele mitaani zitapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendea haya mambo tunayoyazungumza humu Bungeni, watendaji huko chini wakiya-support tutakaa raha mustarehe na majimbo yatakuwa mazuri na hakika mitaani utapita utaona nyuso za wananchi zikiwa zimekunjuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ningependa nizungumze suala la mafuta, ambalo ni issue kubwa sana. Suala la mafuta katika nchi yetu limekuwa ni changamoto na hii si changamoto ya kujiitegemezea na hatuwezi kuwalaumu wanasiasa ama watendaji wetu; ni kulingana na mazingira ya dunia tuliyonayo kwa sasa wababe huko wanaonyeshana nguvu. Waswahili wanasema wapambanapo fahari wawili ziumiazo ni nyika. Kwa hiyo nafikiri sisi kama nyika tunaumia. Ningeomba tu, kwanza ninakubaliana na hatua ambayo inachukuliwa na Serikali katika kuhakikisha kwamba mafuta yanapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mabadiliko ya bei kuongezeka ya wastani kati ya shilingi 800 hadi shilingi 1,000 ningeiomba sasa Serikali ihakikishe kuwa inakazia mkazo hapo, mafuta yasiongezeke tena; na badala yake Serikali iondoe kodi, baadhi ya kodi ifute ili bei ya mafuta isimame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hivyo tunapozungumzia habari kidogo ya fedha iliyopanda kwenye price ya lita moja ya mafuta, tukubaliane kimsingi kwamba tunaenda kuongeza pia mfumuko wa bei. Si mfumuko wa bei bidhaa zetu tu, ni pamoja na mfumuko wa bei wa gharama zingine zote za binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira hayo, kama Taifa na nchi kwa ujumla, tunaomba Serikali iweze kuongeza pia posho kwa wastaafu wetu, wafanyakazi wetu ili kwenda sambamba na hali halisi ilivyo. Tukiacha bei imesimama kama ilivyo na wafanyakazi wetu ama wafanyakazi wa Serikali na kwenye viwanda binafsi na mishahara ile tunatengeneza kundi lingine la wahalifu kutafuta namna ya kumwibia mwajiri. Ninaomba sana Serikali iangalie hapo upande wa pili pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. (Makofi)