Supplementary Questions from Hon. Charles Mhando Njama (3 total)
MHE. CHARLES M. NJAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Kwanza naanza kwa kumshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuletea pesa wiki iliyopita shilingi bilioni 1.4, kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali yetu ya Magunga. Hospitali ya Magunga imezeeka sana, imechakaa na ina umri karibu miaka 73 sasa. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari twende pamoja katika hospitali ile, kwa ajili ya kufanya tathmini, ili ikiwezekana tufikirie kujenga majengo mapya badala ya kuendelea kuweka viraka katika hospitali ile, ambayo inakuwa ni gharama kubwa zaidi kwa Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Charles, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi pamoja na timu ya wataalam tutaongozana pamoja na Mheshimiwa Mbunge kwenda kwenye hospitali hiyo kufanya tathmini na kuendelea kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo. (Makofi)
MHE. CHARLES M. NJAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, Ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza. Je, kilomita 2.45 za kutoka Korogwe Girls – Stesheni zitafanyiwa upanuzi ili kuendana na ujenzi wa barabara mpya kutoka Old Korogwe – Kwamndolwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoanza hii barabara ni kuanzia Old Korogwe – Kwamndolwa. Nimwelekeze Meneja wa Mkoa wa Tanga kwamba kwa kuwa hii barabara inaenda Korogwe Girls waende wakaiangalie na kuona kama imefanyiwa usanifu ama kama haijafanyiwa usanifu iweze kufanyiwa usanifu ili tuweze kuunga hizo kilometa 2.5 kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. CHARLES M. NJAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa namna ambavyo wameendelea kutoa jicho lao kwa ajili ya ukarabati wa majengo yale, lakini kwa kuwa hali ya majengo yale ni chakavu mno na hayaridhishi kabisa, tunaomba aweze kupanga safari yeye pamoja na wataalam wake ili twende tukaone hali halisi kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, ninaamini baada ya kuiona tunaweza tukawa na mpango wa pamoja ambao utatufanya tuharakishe zaidi kufanya matengenezo, kwa kuwa kiasi cha milioni 600,000,000 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bado ni kidogo mno ukilinganisha na hali ya uhitaji uliokuwepo katika majengo yale.
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je ni lini ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Kwamndolwa utaanza, kwa kuwa imekuwa ahadi ya muda mrefu kwa wananchi wa Kwamndolwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, pongezi ambazo amezitoa Mheshimiwa Mbunge zinaelekea moja kwa moja kwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu yeye alifanya ziara na aliahidi fedha hizi ziende kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ambayo imetajwa.
Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge lako Tukufu, tutapanga ratiba ili twende ziara katika hospitali yetu hii kujionea uchakavu wa miundobinu na pia thamani ya fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya kukamilisha miundobinu hiyo.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba katika swali lake la pili la nyongeza kuhusu kituo cha afya, tukiwa katika ziara hii tutapita kwenye kituo cha afya alichokitaja ili tuone namna gani ya kuendelea kutenga fedha ili kukamilisha miundobinu ya ujenzi wa kituo hicho.