Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Charles Mhando Njama (2 total)

MHE. CHARLES M. NJAMA aliuliza:-

Je, lini barabara ya Old Korogwe – Kwamndolwa kilomita 10 itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Charles Mhando Njama, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Old Korogwe ni sehemu ya barabara ya Mkoa ya Old Korogwe – Kwamndolwa – Magoma – Mashewa – Bombomtoni – Mabokweni yenye urefu wa kilometa 127.69. Mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu ya Old Korogwe – Kwamndolwa yenye urefu wa kilomita 10 upo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kumpata Mkandarasi. Mara baada ya kumpata Mkandarasi ujenzi kwa kiwango cha lami utaanza. Ahsante.
MHE. CHARLES M. NJAMA aliuliza:-

Je, Serikali haioni kuwa ipo haja ya kujenga majengo mapya katika Hospitali ya Magunga badala ya kuendelea kuweka viraka kila mwaka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles Mhando Njama, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hospitali ya Magunga ni moja ya hospitali kongwe nchini ambayo imejengwa mwaka 1952 na inahitaji ukarabati mkubwa. Katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 Serikali imetoa jumla shilingi bilioni 1.06 kwa ajili ya ujenzi wa jengo jumuishi la huduma za uzazi Maternity Complex kwa muundo wa ghorofa. Taratibu za kibali na michoro zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imetenga fedha shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa theatre pamoja na ukarabati wa jengo la kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Magunga. Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mipya inayohitajika katika Hospitali ya Magunga ili iweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.