Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dougras Didas Massaburi (2 total)

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. DOUGRAS D. MASSABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, leo kwa mara ya kwanza ninasimama ndani ya Bunge hili Tukufu kwa ridhaa ya wananchi ya Jimbo la Kivule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwanadiplomasia nguli Afrika na dunia ambaye alichaguliwa na Watanzania kwa zaidi ya 97%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchaguzi ule ulitafsiriwa na kazi kubwa aliyoifanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miaka yake minne ya uongozi, lakini alionekana kwenye mikutano mbalimbali ya wananchi kwa namna ambavyo wananchi walifurika kadiri ambavyo alikuwa akitembea katika mikoa yote takribani 32.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuzunguka kwake, ahadi zake zilisheheni matarajio ya Watanzania, na ahadi zake zilimgusa Mtanzania mmoja mmoja. Wakati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, alikuja na falsafa ya 4R.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika falsafa yake ya 4R ilimfanya kutambulika duniani na Mataifa ya nje na kupelekea kuwa kinara kwenye masuala ya haki za binadamu, uhuru wa habari, uhuru wa dini na kadhalika. Kiongozi ni lazima uwe na ngozi ya mamba. Hata nyakati ambazo zilikuwa ngumu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alituvusha salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtakumbuka tulipata fedha za IMF kwa ajili ya kuzuia na kujikinga kipindi kile cha Covid. Tunao Ushahidi wananchi wa Jimbo la Kivule tulipata takribani shilingi bilioni 4.6. Dkt. Samia Suluhu Hassan aligeuza kuwa fursa na tukapata zaidi ya madarasa 232, wananchi wa Jimbo la Kivule wanapata elimu iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tukasema ya kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kazi kubwa aliyoifanya na mageuzi makubwa aliyoyaleta katika mashirika ya umma ilikuwa ni chachu ya kuwaletea maendeleo kwa wananchi wa chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitasoma kwa haraka haraka mambo makubwa na mageuzi aliyoyafanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka yake minne. Kwanza aliongeza Government Investment Value kukutoka shilingi trilioni 67 hadi shilingi trilioni 92, sawa na 36% ya ongezeko la mitaji katika mashirika ya umma. Kwa maarifa hayo ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilimpelekea kuvuna fedha nyingi za gawio la Serikali kutoka shilingi bilioni 637 hadi shilingi trilioni 1.028 mwaka 2020/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa imefanyika kwenye mageuzi. Tumeona namna ambavyo Serikali imewekeza katika mashirika yasiyokuwa ya kiserikali. Tumepata ongezeko kutoka shilingi bilioni 153 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 263 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la 72%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameendelea kuimarisha mashirika ya kimkakati. Shirika la TANESCO lilikuwa linajiendesha kwa hasara, lakini leo hii faida imeongezeka kutoka shilingi bilioni 8.9 hadi shilingi bilioni 21.9 yenye capital ya shilingi trilioni 2.4. Tumeona mashirika mengine kama TPDC ambao wametoka profit ya shilingi bilioni 159 hadi shilingi bilioni 306 kwenye mtaji wa shilingi trilioni 2.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mashirika ambayo yalikuwa hayatoi gawio, mfano TAZAMA Pipeline leo hii imeendelea na Serikali inapata faida kutoka kwenye magawio na maeneo hayo. Pia tumeona namna gani tumeendelea kuongeza hisa katika kampuni za madini ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2017. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mageuzi makubwa, lakini hayakuishia tu kwenye Kitaifa, mageuzi haya yameshuka chini na kumgusa mwananchi mmoja mmoja. Hivi leo mimi ninavyozungumza hapa Jimbo letu jipya la Kivule halikuwa na maji, kwa maana maji yalikuwa ni asilimia sifuri. Leo tunapozungumza ndani ya miaka yake minne maji yamefika 48%. Amejenga tenki kubwa la maji la lita milioni tisa lenye thamani zaidi ya shilingi bilioni thelathini. Maji yale yanatembea Ilala nzima, kwa maana Jimbo la Segerea, Jimbo la Ukonga zamani, pamoja na Jimbo letu jipya la Kivule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mitambo ile ya maji aliyoinunua kwa kila mkoa takribani mwezi mmoja uliopita, kaka yangu Mheshimiwa Juma Aweso alikuja Jimbo la Kivule na watu wa Kivule tukapata mitambo ile, na sasa visima takribani 10 vinaendelea kuchimbwa ndani ya Jimbo letu Jipya la Kivule (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha masuala ya maji, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa katika sekta ya elimu. Leo hii sisi wananchi wa Kivule tulikuwa hatuna kidato cha tano na cha sita, lakini sasa zimejengwa shule za sekondari mpya za kutosha, tena nyingine zenye hadhi ya gorofa. Tunayo Shule ya Sekondari ya Kitunda Relini, tunayo Shule ya Sekondari ya Kipunguni zenye hadhi ya ghorofa ndani ya Jimbo leu jipya la Kivule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye sekta ya afya, jimbo lile ni jipya, wakati Mheshimiwa Rais anaingia madarakani hakukuwa na kituo cha afya hata kimoja, leo tunapozungumza kwenye kata zetu zote sita tuna kituo cha afya kimoja kikubwa kwenye Kata ya Kivule chenye mfano wa hospitali ya Kiwilaya, na kingine kikubwa zaidi Kata ya Mzinga zenye thamani ya shilingi bilioni 4.9 chenye thamani hiyo, na vifaa vya kutosha. Wananchi wa Kata ya Mzinga na Jimbo la Kivule wanapata huduma ya afya kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite sasa, kwenye mpango ambao tumeuona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 14 Novemba, Mheshimiwa Rais ametoa dira lakini pia ametupatia hotuba. Hotuba yake ilisheheni mahitaji ya Watanzania hasa vijana na akina mama. Utaona namna gani alikuwa anajaribu kuunganisha ujenzi wa vyuo vya VETA pamoja na mikopo ya 10% ya akina mama na vijana ili kuweza kutengenza matajiri wa baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie fursa hii kumshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, baada ya kuona congestion kubwa kwenye Chuo cha VETA cha pale Chang’ombe ambacho kipo Wilaya ya Temeke, nasi watu wa Ilala sasa tunakwenda kupata Chuo chetu cha VETA ndani ya Wilaya ya Ilala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumepata fedha kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kaka yangu Elihuruma, tumenunua eneo kubwa la hekari tisa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA ili kuweza kuwanyanyua na kuwasaidia vijana wanaoishi ndani ya Wilaya yetu ya Ilala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tunaomsaidia Mheshimiwa Rais, tunapaswa ku-walk the talk; yaani kutembea mle ambapo Mheshimiwa Rais anatarajia. Hapa imetajwa sekta yetu ya ujenzi, amesema anakwenda kuongeza bajeti TARURA na kuongeza bajeti kwenye Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu pale, Mheshimiwa Chaurembo aliuliza swali, Barabara ya Msongola kuelekea Mbande mpaka Chamazi, tukapata majibu ya Naibu Waziri kuwa ni kusuasua na uwezo wa mkandarasi. Sisi watendaji tunapaswa kupata wakandarasi watakaotusaidia kupata value for money na ku-achieve zile 5R of procurement ili miradi yetu iweze kukamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Rais, katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi Barabara yetu ya kutoka Banana – Kitunda – Kivule – Msongola tayari mkandarasi anaifanyia kazi, na tumeahidiwa kufikia mwezi wa Nne lami ile itakuwa imekamilika na wananchi watakuwa wanaitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wetu wa Kiserikali, Waheshimiwa Mawaziri, waendelee kuliangalia kwa jicho la kipekee Jimbo letu Jipya la Kivule. Barabara ya kutoka Pugu kuelekea Majohe kuelekea mpaka Mbondole; Barabara ya kutokea pale Kitunda kuelekea Magole kupitia Nyangasa; Barabara hiyo hiyo kutokea Kitunda kuelekea Mwanagati ni takribani kilomita thelathini na nane, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameziorodhesha kwenye Ilani ya Chama cha mapinduzi. Kazi yetu sisi ni moja tu, kusimamaia mradi ule wa DMDP uweze kukamilika kwa wakati na barabara nyingine zilizobakia takribani kilomita 50 ndani ya Jimbo letu Jipya la Kivule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, itoshe kusema ya kwamba, sisi wananchi wa Kivule tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupatia jimbo letu jipya, na kutupatia mwakilishi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nasi tupo tayari kumsaidia Mheshimiwa Rais kuisimamaia Serikali kutekeleza wajibu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DOUGRAS D. MASSABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza nachangia hotuba ya Mapato na Matumizi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana tumetoka kwenye Mwenge Ilala na tumezindua miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 54 na sehemu kidogo. Nasi watu wa Kivule pia tulipata shule za sekondari na nyingine za ghorofa ndani ya Jimbo letu la Kivule, ikiwemo Shule ya Sekondari ya Kitunda Relini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa ndani ya jimbo letu. Tunavyo vituo vya afya vya kutosha. Tunazo kata sita, na ndani ya kata sita tayari kata tano zote zina vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kupitia Wizara ya Maji, pale kwenye Kata ya Kivule ndugu yetu Mheshimiwa Aweso alitutembelea na akatuahidi visima takribani 10 vya maji, na tayari tunacho kisima juzi vimeshaanza kutoa maji kwenye kata ile ya Kivule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, najikita kwenye changamoto za Jimbo la Kivule. Juzi dada yangu Mheshimiwa Bonnah alizungumza hapa masuala ya AFCON; na kimsingi Jimbo la Kivule ni Jimbo linaloendesha uchumi wa eneo lile. Lipo Katikati, yaani ukitoka Mbezi ukapita Segerea ni lazima upite Jimbo la Kivule ndipo utokee Chamazi ambako watu wa AFCON watakapokuwa wanafanya mazoezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza, Jimbo hili la Kivule halina barabara ya lami hata moja. Wenzangu hapa wamekuwa wakililia kukarabatiwa barabara zao za lami, ni sawasawa na mtoto analilia kiatu kizuri wakati mimi familia yangu mtoto wangu hana hata mguu. Kwa hiyo, naomba sana nifikishie salamu za wananchi wa Jimbo la Kivule, wanalia na barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata juzi Mheshimiwa Kwagilwa alikuja pale akiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI na mkandarasi wa Barabara ya kutoka Banana – Kitunda – Msongola, barabara hiyo hiyo kuelekea Nyantira na Mwangati, inapita njia nne kutoka Majohe mpaka Pugu Sekondari. Ziliahidiwa kufika tarehe 30 Aprili, 2026 zitakabidhiwa kwa wananchi, lakini cha kustaajabisha, kama anavyoongea kaka yangu Baba Levo, bado ni matope yasiyokuwa na mwisho. Sasa hivi zimebaki siku 16 peke yake kutimiza siku hiyo ya tarehe 30 Aprili, 2026, lakini sioni jitihada yoyote inayofanyika ili kuhakikisha barabara hizo zinapitika kiangazi na masika, na vilevile madaraja pamoja na vivuko kwenye maeneo ya Mto Mzinga

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, 70% ya mayai yanayokwenda Dar es Salaam yanatoka ndani ya Jimbo la Kivule. Vilevile tunalima mbogamboga kama mchicha, na spinach, maana pale tunapitiwa na Bonde la Mto Mzinga. Akina mama wanafanya shughuli zao za kiuchumi ili kuweza kulisha Mkoa wa Dar es Salaam na Serikali kupata kodi kwenye malisho hayo. Sasa inafika mahali, wanazalisha lakini hawapati nafasi ya kusafiri umbali mrefu kupeleka mazao yao huko mjini kwa ajili ya ubovu wa barabara na kupanda kwa gharama za usafirishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimeona niwasilishe changamoto hizo kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamewasilisha. Nami nina kilio kikubwa sana cha Jimbo letu jipya la Kivule. Kwa hakika mtufikirie, tuone namna gani tunakwenda kulikomboa jimbo lile kwa miundombinu ya barabara ili wananchi wetu waendelee kufanya shughuli zao za ufugaji na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na Mpango, Dira 2050 na Mapato na Matumizi ya Mwaka 2026/2027. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye Rais pekee ambaye baada ya sisi Bunge kutunga Sera mwaka 2009, mwaka 2010 tukatunga Sheria ya PPP, halafu mwaka 2014 tuka-review Sheria ya PPP tukaelekeza tuanzishe kituo cha PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, tangu 2014 hadi 2024 kituo hicho cha PPP hakikuwahi kuanzishwa isipokuwa alipokuja Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, akakianzisha, na akamkabidhi kaka yetu Mheshimiwa Kafulila kama sehemu ya kuwa Mkurugenzi wa Kituo kile. Ninampongeza Mheshimiwa Kafulila, na hivi juzi kwenye gazeti la AgMP Tanzania tumetambuliwa kuwa nafasi ya tisa duniani kama watu ambao tunao professionals wa kutosha kwenye kitengo hicho cha PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wetu huu ukiuangalia unaelekeza kuwa 70% utokana na vyanzo mbadala kwa maana ya PPP, shares, na bond. Hizo ndizo alternative financing. Hata hivyo, katika sheria yetu hakuna mahali ambapo inazungumzia bonds na shares zinakuwa managed vipi? Isipokuwa PPP peke yake ambayo ina dedicated center na ina policy pale, ambayo sisi tuliitunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado PPP yenyewe hii tunayoisema hapa hatuipi meno ya kutosha. Tunazungumza kuwa miradi mingi itokane na vyanzo mbadala (alternative financing). Lengo letu ni kwamba, kiasi kinachobaki Serikali ikiwekezee nguvu kwenye primary objective ya kusaidia wananchi katika kupata afya bora, elimu bora, na barabara bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia bajeti ile ya PPP tumeona imepitishwa shilingi bilioni moja kila mwaka. PPP maana yake ni maandalizi ya mradi. Sasa kama tunafikiria kuanzisha mradi wenye thamani ya shilingi trilioni kumi, kwa mfano mradi ule Mbambabay kwenda Mtwara wenye thamani siyo chini ya shilingi trilioni 10, au 15, lakini feasibility study yake inahitajika siyo chini ya dola 2,500,000. Eti Serikali inasubiri SADC watoe fedha hiyo kwa ajili ya kufanya feasibility study kwenye mradi ambao unaweza kuwa na tija kwa Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo haja ya kushikamana ili tuweze kukipa nguvu kitengo cha PPP ili miradi hiyo iende kwenye hizo alternative financing na fedha nyingi ibaki kuweza kuwahudumia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona wenzetu wa Kenya pale nchi jirani, samahani, wao wanatumia siyo chini ya dola milioni 60 kwenye uandaaji wa miradi, lakini sisi tunatumia bilioni moja kwenye uandaaji wa miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hapa Wizara ya TAMISEMI wameorodhesha miradi zaidi ya 400 kwa ajili ya alternative financing. Sasa tujiulize, je, wanazo feasibility study? Je, miradi hiyo are they bankable projects? Ni kwamba tunayo list, tunayo majina ya miradi, lakini hatuna list ya miradi. Kwa hiyo ipo haja ya kuona namna gani bora tunaweza tukawashikilia ndugu zetu wa PPP, tukawapa nguvu, na tuka-coordinate hizi alternative financing kama ndugu zetu wa Rwanda wanavyofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rwanda wana kitu kinaitwa Rwanda Board of Directors. Kwamba mtu akienda pale, ana jambo la PPP, au shares, ama bonds, kila kitu kinamalizikia pale. Ningeshauri, hiyo iwe chini ya Ofisi ya Rais ama Waziri Mkuu ili kuweza kupunguza miluzi mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakubaliana kwamba uchumi wa nchi yetu upo kwenye mashirika, na ndiyo maana Mheshimiwa Rais aliweka zaidi ya shilingi trilioni 92.5 kwa ajili ya kunyanyua mitaji ya mashirika. Hata hivyo, bado kuna changamoto katika kufanya maamuzi. Yaani kuna multi approvals centers nyingi. Unakuta mtu anakuja, anataka kufanya uwekezaji, ni lazima aende kwa TR halafu arudi kwa PPP. TR yuko Wizara ya Mipango, PPP tuko Wizara ya Fedha, Waheshimiwa Mawaziri tofauti, hakuna coordination of the Government.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuone kuwa kuna haja ya kuichukua PPP yenyewe iunganishwe na watu wa TR ili kusudi waweze kuleta ufanisi wa mashirika, kwa sababu lengo la TR na PPP ni kuleta ufanisi kwenye mashirika ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona nishauri hilo ili kuweza kuona namna bora ya kuweza kuyashirikisha mambo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tunalenga kujenga uchumi. Serikali yetu hii inazo assets nyingi. Ipo haja ya kufanya tathmini ya assets za Serikali. Zile ambazo hazizalishi na tunaona zitahitaji capital ambayo inaweza ikatoka ama foreign ama kwenye private sector, tuingize ili kuweza kuongeza ajira, kuchangia uchumi na kufanya mnyororo mpana wa kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana nami kwamba, yapo mashirika mengine lakini hayazalishi. Ipo sababu sasa ya ofisi za Serikali kufanya evaluation ya maeneo hayo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Massaburi, muda wako umeisha, ninaomba uunge mkono hoja. Unaweza ukachangia kwa maandishi, haina tatizo.

MHE. DOUGRAS D. MASSABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)