Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kija Limbu Ntemi (5 total)

MHE. ENG. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Spika, ninamshukuru kwa majibu ya Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ninapenda kufahamu huu mkataba utaanza lini, kwa sababu watu wameshaumizwa na wameshafungiwa mikataba ambayo inaonesha ni mkataba wa miezi minne, hauna malipo, lakini watu wamelipa fedha nyingi kwa ajili ya hii mikataba. Unafungiwa mkataba wa miezi minne kila duara moja inalipa shilingi milioni kumi kumi, zaidi ya maduara 100 watu wamelipa fedha.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, hawa watu waliolipishwa hizi fedha ndani ya miezi minne na miezi mitatu kuna uwezekano wa kurudishiwa fedha zao ili huu utaratibu utakapoenda kuanza, hawa watu wawe wamesharudishiwa fedha zao na utaratibu ufuatwe vizuri kwa sababu wameonewa na zile fedha wamelipa pasipo na utaratibu na hazina mfumo wowote.

SPIKA: Mheshimiwa maswali yako ni mawili tu.

MHE. ENG. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la kwanza Engineer Kija, ninapenda kukujulisha kwamba kanuni hizi zilipotungwa au zilipofanyiwa marekebisho mwaka jana tukaweka kipengele kinachohakikisha kwamba hakuna mwenye leseni anayempangisha mchimbaji mdogo eneo bila kusainiana mkataba. Kwa hiyo, kwa sababu sheria haina tabia ya kurudi nyuma, siyo retrospective, kuanzia kanuni hii iliporekebishwa wote wanaoingia katika makubaliano mwenye leseni na anayetaka kupanga eneo lazima wa-comply.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, kiwango wanachowekeana ni maridhiano yao na sisi kama Wizara wakishasajili mkataba tunausimamia, yale yaliyopita wahenga wanasema si ndwele tugange yaliyopo na yajayo.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante na nina swali moja kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Ni lini Barabara ya STAMICO – CCM – Ushirombo itajengwa kwa kiwango cha lami ili kuondoa adha ya wananchi kwa sababu barabara ilishaandaliwa katika mfumo wa kuwekewa lami, lakini sasa hadi leo haijawahi kujengewa lami na watu walibomolewa nyumba kusogea ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami? Ni lini Serikali itaamua kujenga kutoka STAMICO – CCM – Ushirombo kwa kiwango cha lami ili kuondoa vumbi na kero inayowapata wananchi wa Jimbo la Katoro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutashirikiana na wenzetu wa TARURA kama Serikali kuhakikisha kwamba kama tayari wameshabomolewa watu, basi mpango upo. Hata hivyo, tutashirikiana na wenzetu wa TARURA kuhakikisha kwamba hiyo barabara inajengwa. Kwa sisi TANROADS, barabara yetu ni kutokea Ushirombo kuja Katoro (ile barabara kubwa ambayo ndiyo tunashughulikia).

Mheshimiwa Spika, hiyo barabara nyingine, tutaongea na wenzetu wa TAMISEMI kupitia TARURA tuone wamefikia hatua gani ama baada ya hapa nimwombe Mheshimiwa Mbunge tuje tukae tuone ni barabara ipi hasa anayoisemea.
MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea maji katika Mji wa Katoro akiyatoa eneo moja linaitwa Chankorongo. Tangu dunia iumbwe maji hayajawai kufika Katoro, lakini sasa yamefika Katoro kwa gharama ya shilingi bilioni nane.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kufahamu maji yameshaletwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, je, ni lini sasa Serikali itakuja kusambaza maji hayo ili wananchi waweze kunufaika na maji kuliko kubaki tu na historia ya kwamba maji yamefika Katoro na hayajasambazwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe pia Mheshimiwa Waziri…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, swali la nyongeza ni moja.

MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ntemi Kija, Mbunge wa Katoro, hakika ameanza kazi yake vizuri na anafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha kwanza tunachohitaji katika utekelezaji wa miradi hii ni kupata ama kubainisha chanzo cha maji na baada ya hapo kujenga miundombinu (transmition line main) na baada ya hapo sasa tunakuja kwenye usambazaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimtoe hofu kwa sababu kazi ya kupata chanzo imekamilika, kazi ya kujenga miundombinu ya kufikisha maji katika eneo la Katoro imekamilika. Sasa kazi iliyobaki ni ndogo sana kwa Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, usambazaji wa maji katika Mji wa Katoro unaenda kufanyika kwa haraka sana. (Makofi)
MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Katika Hospitali ya Wilaya ya Katoro, tuna changamoto ya jenereta, limeharibika kwa muda mrefu, na huduma zimesimama. Lini sasa Serikali itapata jenereta ili kutimiza mahitaji ya wananchi katika Hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali hii ya wilaya inaendelea kutoa huduma kwa kutumia umeme wetu, lakini sasa huwa tuna yale majereta ya dharura ambapo sasa nimwelekeze Mkurugenzi afike eneo la tukio na aone kwanza namna gani ya kuweza kulirudisha jenereta lililokuwa linafanya kazi pale ili liendelee kuwa la dharura na kutoa huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)
MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii ili na mimi niulize swali. Kituo cha Afya cha Katoro kinapokea wagonjwa wengi sana kuliko Hospitali ya Wilaya ya Katoro. Je, ni lini Kituo cha Afya cha Katoro kitapata jengo la emergence ili kuongeza ufanisi kuhudumia wananchi wa Katoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, ni kweli pale Katoro kuna ongezeko kubwa sana la watu ndiyo maana wananchi wetu wanaona bora waende kwanza wakapate huduma katika kituo cha afya, lakini tayari Katoro wanayo hospitali ya wilaya inayotoa huduma za msingi, na wana jengo bora kabisa la emergency.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunawaomba wananchi waendelee kwenda kupata huduma hizo katika jengo la dharura la hospitali yetu ya Wilaya huku tukiendelea kujielekeza kuboresha miundobinu rafiki na miundobinu ya dharura katika kituo chetu cha Afya cha Katoro.