Supplementary Questions from Hon. Ado Shaibu Ado (5 total)
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kuniona. Kwa vile tatizo hili la tembo kuvamia vijiji na kuharibu mazao, kuuwa binadamu ni tatizo kubwa sana katika Jimbo la Tunduru Kaskazini na Wilaya ya Tunduru kwa ujumla wake. Ambapo kwa msimu wa kilimo wa 2025/2026 peke yake jumla ya waathirika 1791 wameharibiwa mazao yao na askari wa vijiji mpaka sasa wako 23 tu. Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa waathirika wote na kuongeza idadi ya askari wanyamapori wa vijiji (VGS)?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tayari Serikali imeshaweka fedha na zimeshaingia na sasa tunafanya utaratibu wa kulipa kupitia mfumo. Kilichochelewesha ilikuwa tunalipa manual, unaenda kijijini unaenda kulipa, pengine unaenda kulipa milioni tano unatumia gharama ya milioni nne, lakini kwa sasa tunatumia mfumo na mfumo huu umetuwezesha. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira hawa watu wetu watapata malipo yao.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona ili niulize swali dogo la nyongeza. Mbunge wa Tunduru Kusini Mhandisi Fadhili Chilombe, ninafahamu kwamba ameleta hoja na kufuatilia mara nyingi Wizara ya TAMISEMI juu ya haja ya kuigawanya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kupata Halmashauri mbili na mchakato wetu ulifika mpaka RCC, tuna watu zaidi 400,000 na tuna kilometa za mraba 18,000.
Mheshimiwa Spika, tunataka kauli ya TAMISEMI ili Watanzania wanaoishi Tunduru wapate kauli ya Serikali ndani ya Bunge. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kujibu kwenye jibu la msingi, uanzishwaji wa mamlaka za kiutawala ikiwemo hili analoliongelea Mheshimiwa Mbunge, Ado Shaibu, Mwenyekiti wetu wa Kamati ya LAAC unazingatia Sheria ile ya Uanzishwaji ya Mamlaka za Wilaya, Sura Na. 287 pamoja na Sheria ya Uanzishwaji wa Mamlaka za Miji, Sura 288.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimetoa maelekezo na ushauri kwa Halmashauri ya Kibaha, vivyo hivyo wananchi wa Tunduru wafuate utaratibu huo na TAMISEMI kazi yetu ni moja tu kufanya tathmini na mapitio kama vigezo vimezingatiwa. (Makofi)
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Tunduru Kaskazini ni moja kati ya majimbo ambayo hayana kituo cha afya kwa kila tarafa, na kwa kuwa Tarafa ya Nampungu ni tarafa pekee ambayo haina kituo cha afya na haijapata bajeti ya kutosha katika ukamilishaji wa ujenzi wa kituo hicho cha afya, je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Mpungu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pia Jimbo la Tunduru Kaskazini lipo katika mpango wa kupata kituo cha afya cha kimkakati; na kwenye yale maombi tuliyowasilisha Hazina kimo kituo hiki cha afya cha Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kukamilisha baadhi ya majengo katika vituo vya afya ambavyo bado havijakamilika ili kuendelea kutoa huduma kwa watu wetu wa Jimbo la Tunduru kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa, Kituo Kikukuu cha Polisi cha Wilaya ya Tunduru ni kikongwe na kidogo, katika mazingira ambayo yanalazimisha sisi akina Ado ambao huitwa mara kwa mara pale kuhojiwa, tumewashuhudia makamanda wetu wakiwa wanaendesha mahojiano ndani ya chumba kimoja kwa watuhumiwa zaidi ya mmoja, hali ambayo inaondoa kabisa weledi, je, ni lini, Serikali itafikiria kujenga kituo kipya cha Wilaya ya Tunduru ili makamanda wetu wafanye kazi kwa weledi na utaratibu unaohitajika, ikiwemo faragha?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru na kumpomgeza sana Mheshimiwa Ado Shaibu, lakini ninaomba nimkumbushe tu kwamba kituo cha Polisi alichokitaja na vituo vyote vya Polisi nchini, uwepo wake siyo kwa ajili ya akina Ado Shaibu, ni kwa ajili ya wale wote ambao watakuwa wanahalifu sheria za nchi hii. kwa hiyo, Serikali inaendelea na hatua mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vituo vya Polisi vya ngazi ya wilaya, ambavyo kwa taarifa yetu ya awali tulisema kwamba tuna vituo vya Polisi 75 vya ngazi ya wilaya, ambavyo ama vinahitaji ukarabati au vinahitaji kujengwa upya kwa lengo la kufikisha hadhi ya daraja B, kwa maana ya kituo cha wilaya, kwa hiyo, na kituo cha wilaya ambayo Mheshimiwa Ado Shaibu amekitamka, nacho kipo kwenye mpango huo. Kadiri ya hali ya upatikanaji wa fedha tutaendelea kujenga vituo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika Wilaya ya Tunduru, Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa Mahakama ya kisasa ya ngazi ya wilaya. Kwa miezi mitano hivi sasa ujenzi ule umesimama. Swali langu ni kutaka kujua, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Mahakama ile ili tuweze kupata huduma inayokusudiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Ado Shaibu Ado, Wakili Msomi, kwa swali lake zuri lenye lengo la kufuatilia upatikanaji wa haki katika jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, ninaomba niendelee tu kumsisitiza Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza mradi wa kimkakati kabisa ambao unatokana na mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama na kwa sasa Mahakama inatekeleza mpango huu wa pili na imetumia wastani wa shilingi bilioni 524.9 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Mahakama kuanzia katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo mpaka Makao Makuu ya Mahakama kama tunavyoliona jengo letu la Judiciary Square.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa Mahakama ya Wilaya ya Tunduru aliyoitaja tayari imeshafikiwa na mpango huu wa pili, na tayari mkandarasi yupo site anaendelea na ujenzi wa Mahakama hiyo, nimhakikishie kwamba ni dhamira ya Mahakama kuhakikisha wananchi wanapata majengo bora ya kisasa kwa ajili ya upatikanaji wa haki. Kwa hiyo, jengo hilo litajengwa na litakamilishwa ili wananchi wake waweze kupata huduma bora kabisa za upatikanaji wa haki katika jimbo lake.