Contributions by Hon. Ado Shaibu Ado (3 total)
Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Zima ninashukuru sana kwa kuniona ili na mimi nitoe mchango wangu juu ya mipango iliyowasilishwa mbele ya Kamati yetu ya Bunge Zima. Ni lazima nikiri kwamba, leo ni moja ya kati ya siku za kipekee sana kwangu. Hii ni kwa sababu, zaidi ya mwongo mmoja uliopita, nikiwa nafanya kazi ya kujitolea katika Kigoda cha Mwalimu Nyerere juu ya umajumui wa Afrika. Yuko bwana mmoja aliniita katika moja ya migahawa ya Jiji la Dar es Salaam. Bwana huyo alinipa mawazo yake kwamba, kwa kadiri anavyonifahamu anadhani ninaweza kutoa mchango fulani kwenye jamii iwapo nitajiunga na siasa ya vyama vya siasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakiri kwamba, nilimkatalia kwa sababu zangu binafsi, lakini baadaye kutokana na bidii yake juu ya jambo hili, na tafakuri yangu ya binafsi, niliamua kumkubalia. Bwana huyo ndiye ambaye leo Wizara yake imeandaa mipango tutakayoijadili hapa sambamba na ile ya Wizara ya Fedha. Bwana huyo ni Mheshimiwa Prof. Kitila Alexander Mkumbo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasimama hapa kwa kujiamini sana kwamba, licha ya utofauti wetu wa kiitikadi Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo hatarajii hata kidogo kwamba, mimi nitasimama mbele ya Kamati hii nikajikita kumsifia peke yake. Ninafahamu kwamba, Mheshimiwa Prof. atafadhaika iwapo mimi nitajikita katika kuonesha changamoto bila kuonesha majawabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ndiyo siasa ninayoifahamu, hiyo ndiyo siasa ninayoitamani, na hiyo ndiyo siasa ninayoiota. Siasa ya kupingana kwa hoja bila kugombana, siasa ya kupishana bila kuumizana, siasa ambayo ninaamini siku moja isiyo ya mbali, siasa ya namna hiyo itakita mizizi tena katika duru za kisiasa za nchi yetu, ili kwa pamoja tuweze kutoa mchango wetu wa kuijenga nchi kwa upendo na mshikamano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza juu ya mipango yetu, kwa sababu, mawazo mengi yametolewa hapa na sitaki kurudia; la kwanza, ni mpango wowote ni lazima pia, utazame vihatarishi vya utekelezaji wa mpango ule. Mimi ninaona mpango haujatazama kwa kina vihatarishi vya Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifuatilia siasa ya dunia hivi sasa mwenendo wa mambo katika siasa za Kimataifa unakuonesha kwamba, kuna mabadiliko ya kasi sana miongoni mwa Mataifa, hasa juu ya sera zao za mahusiano ya kimaendeleo na kudorora kwa nafasi na ushawishi wa majukwaa ya Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo linatutaka tuchukue tahadhari hasa katika kuhakikisha tunaweka vizuri masuala yetu ya ndani. Kama hatuweki vizuri masuala yetu ya ndani yatakayotufanya tuzalishe vizuri kwa utulivu, tukawa focused, tunaweza kujikuta tunapata changamoto katika financing ya mipango yetu na tukajikuta tunajikita katika kuwaumiza Watanzania kwa kuwabebesha mzigo mkubwa wa kodi ama kuingia katika mikopo ya kibiashara yenye masharti magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninarudia rai yangu, tutengeneze nyumba yetu vizuri, tujenge mshikamano wa Kitaifa, tuweke mazingira mazuri ya kisheria, kikatiba na muafaka wa Kitaifa utakaotufanya mipango yetu ya uzalishaji. Kimakusanyo inabaki kama ambavyo tumeipanga, hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili. Mipango yetu inasema kwamba, sekta binafsi itakuwa ndiyo engine ya utekelezaji wa mipango ile. Kwenye financing ya mipango yetu inasema kwamba, 70% itakuwa kwa sekta binafsi na 30% kwa sekta ya umma. Ninaunga mkono rai iliyotolewa na Wabunge wengi kwamba, ni lazima tuendelee kuweka mazingira wezeshi yatakayoifanya sekta binafsi iweze kushamiri na itoe mchango wake katika uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi bado ninadhani hatuja-define na hatujaipambanua sekta binafsi tunayoitaka. Ni lazima tujiulize maswali magumu, sekta binafsi tunayoitaka sisi ni sekta gani? Je, ni sekta ya wachuuzi wa kigeni wanaopambana na wajasiriamali Kariakoo? Au ni sekta binafsi isiyozingatia utu, mazingira na maslahi mapana ya Tanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu, ni lazima tuiongoze sekta binafsi. Sekta binafsi isiyopangiliwa, sekta binafsi isiyoongozwa, haiwezi kuwa engine ya uchumi, itakuwa ni bomu linaloangamiza uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu, nimesoma Mipango hii, nimeangalia maeneo ya kielelezo, programu za kielelezo, ziko programu 14 na nikajaribu kuchambua. Nimeona katika kila programu tuna miradi ya kimkakati, kwa maana ya flagship projects. Tuna hatua kadhaa za kuchukuliwa na tuna Mipango mbalimbali. Hii maana yake ni kwamba tuna makumi na makumi ya masuala ya kuyafanyia kazi. Nimeangalia katika mpango wa muda wa kati, nimeona tuna miradi saba ya kielelezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni kwamba Tanzania haijawahi kuwa na uhaba wa mipango tangu tupate uhuru, kwa maana ya Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar. Changamoto yetu kubwa ni utekelezaji wa mipango tunayojiwekea. Nina wasiwasi tukipata shock yoyote katika Mipango, baadhi ya Mipango hii itapewa kipaumbele na baadhi itawekwa kapuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuwe na Mpango fulani ambao tutauita, Mpango wa Kufa na Kupona. Kwamba, hata tukipata shida yoyote, kama Taifa, hili eneo ndiyo kipaumbele chetu namba moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo mchumi, lakini maoni yangu ninaomba Mradi wa Mchuchuma na Liganga ndiyo uwe wa kufa na kupona kwa sababu, Mchuchuma na Liganga ndiyo drive ya mapinduzi ya viwanda vya Tanzania kama tunataka kuhama kutoka katika maendeleo bandia ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunasema tuna maendeleo ya viwanda vya kuunganisha magari. Kwa maoni yangu, yale siyo maendeleo halisi ya viwanda, tena tusipokuwa makini unaweza kukuta ule ni uchochoro wa watu kuikosesha mapato Serikali. Yaani unakuta mtu vipuri vyote 100% anaagiza kutoka nje, anapata misamaha ya kodi, halafu akishaunganisha bila kujali ajira gani anazalisha sisi tunasema hayo ni mapinduzi ya viwanda. Mapinduzi ya kweli ya viwanda yataletwa na uzalishaji wa chuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Mwenyezi Mungu ametupa chuma na makaa ya mawe hapo hapo, Mchuchuma na Liganga. Suala lisilosemwa sana ni palepale Mchuchuma na Liganga kuna madini ya kimkakati ya titanium na vanadium, ambayo yana thamani kubwa zaidi kuliko hata hicho chuma. Kwa hiyo, Mradi wa Mchuchuma na Liganga na Mradi wake shikizi wa Reli ya Kusini, kwa maana ya Reli ya Mtwara mpaka Bandari ya Mbamba Bay, ambao utakuwa na Tawi lake la Mchuchuma na Liganga uwe ndiyo mradi wa kufa na kupona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika neno langu la kuhitimisha, nimejipa homework ya kwamba, kila nikisimama nitakuwa ninakumbusha juu ya Katiba Mpya. Leo ninakumbusha tena kwamba, Katiba Mpya ndiyo funguo ya muafaka wa Kitaifa. Mchakato wake uanze mara moja, uwe wazi, ili wadau wote waweze kushiriki.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. (Makofi)
Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu juu ya hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo aliitoa katika Bunge hili Tukufu. Kwa sababu, hii ni mara yangu ya kwanza kusimama rasmi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchangia hoja, ninaomba nitumie fursa hii kwanza kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Tunduru Kaskazini ambao kwa muda mrefu sana wamekuwa wakiniunga mkono kisiasa na leo ninasimama katika Bunge hili kama mwakilishi wao, ahsanteni sana Wanatunduru. Ahadi yangu kwa Wanatunduru, nitasimama imara, kwa ajili yao, kwa ajili ya kutetea maslahi yao bila kuchoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuchukua fursa hii kukishukuru Chama changu cha ACT-Wazalendo ambacho kimefanya uamuzi wa kuniruhusu mimi na Wabunge wenzangu nane wa ACT-Wazalendo, ili tuweze kushiriki katika Bunge hili la Kumi na Tatu. Kwa mazingira ya Uchaguzi wa Mwaka 2020 uamuzi huo haukuwa mwepesi, lakini kama inavyofahamika siasa ni hesabu na uwepo wetu ndani ya Bunge hili ni hesabu za kulitumikia Bunge hili, kama chombo cha mapambano ya kupaza hoja na kuwasilisha sera mbadala. Historia itatuhukumu kama uamuzi huo wa kimkakati ulikuwa ni uamuzi sahihi ama la.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi yangu na wenzangu ni kwamba, sisi tutatekeleza wajibu huo ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila hofu wala kusita, lakini pia tutatoa michango yetu kwa hoja badala ya vioja. Hiyo ndiyo ahadi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amezungumzia mambo mengi katika hotuba yake, mimi nitajikita katika maeneo makubwa matatu, la kwanza nitazungumzia juu ya mwelekeo wa kisiasa wa nchi yetu. Tangu tulivyoanza kutoa mawazo yetu ndani ya Bunge hili, Wabunge wengi wamezungumza kwa haki kabisa juu ya umuhimu wa amani na juu ya umuhimu wa vijana kupenda Taifa lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nukta moja ambayo imeachwa katika mijadala yetu na mimi ninaisema ni juu ya umuhimu wa haki, ili kupata amani ya kweli. Amani ni zao la haki na demokrasia, bila demokrasia hakuna haki, bila haki hakuna amani, bila amani hakuna maendeleo. Hiyo ndiyo principle. Kwa hiyo, ukiwa unazungumza juu ya amani hata kama utakesha kusisitiza watu wapende amani na watu waipende nchi yao, kama husisitizi juu ya haki huwezi kupata amani ya kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefarijika ndani ya hotuba ya Mheshimiwa Rais, ukiacha zile hatua za kutibu majeraha ya uchaguzi wa 2025 amezungumza juu ya ahadi ya Serikali kufufua mchakato wa Katiba mpya. Hilo ni jambo jema kabisa, lakini nakisi ambayo sisi tunaiona, huwezi kuwa na mchakato bora wa Katiba mpya kwa kutaja ahadi ya Katiba mpya peke yake. Sisi tunaona kwamba, Katiba mpya inashughulikiwa kwa vipandevipande; kipande ambacho tumepewa sasa ni kwamba, kutakuwa na Tume ya Usuluhishi ndani ya siku 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yetu sisi ni mchakato huu ushughulikiwe comprehensively. Tunataka Serikali ije na ratiba kamili ndani ya Bunge hili ya namna mchakato wa Katiba mpya utakavyoendeshwa. Pia, tunataka Serikali itueleze juu ya approach au mtindo ambao itautumia kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujipatia katiba yake na sisi tumekuja na mapendekezo. Hatua ambazo tunazipendekeza ni za muhimu sana katika mchakato huo na ni vizuri mapema sana Serikali inapotoa ahadi itueleze, kama hiyo ndiyo route ambayo itaipitia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, tunahitaji kuzifanyia mapitio Sheria zinazosimamia mchakato wa Katiba mpya, kwa maana ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya pamoja na Sheria ya Kura ya Maoni; hiyo ni hatua ya kwanza muhimu sana. Ya pili ni tunahitaji kuwa na Mkutano wa Kitaifa, kwa maana ya National Sovereign Conference, kwa ajili ya kupata muafaka wa pamoja juu ya masuala ya Kikatiba, ambayo mpaka sasa hayajapata muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya tatu ya muhimu ni lazima tuwe na timu ya wataalam, kwa maana ya Committee of Experts, ambao wataandaa Rasimu ya Katiba Mpya na hatua ya mwisho ni tunahitaji kuwa na kura ya maoni. Kwa hiyo, tunavyoitamka Katiba mpya tusiishie kuitaja kwa ujumla wake, tuwe na road map ambayo itawafanya wadau wote wa Katiba Mpya wajue mchakato utakwenda namna hii. Hilo ni la kwanza ninataka kulisisitiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, jana limezungumzwa kidogo na ninaheshimu taratibu. Ninafahamu kwa mujibu wa Kanuni ya 81, Mwongozo wa Spika ni wa mwisho juu ya suala. Kwa hiyo, sitoliibua tena suala hilo, isipokuwa nina rai kwamba, ahadi ambayo Mheshimiwa Rais ameitoa ya kuachiwa huru kwa wale ambao walikamatwa katika matukio ya tarehe 29 ni ahadi njema. Vyombo ambavyo vinahusika, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Katiba na Sheria, zifanye uchunguzi wa kina, zijiridhishe kama watu wote wameachiwa huru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapofungua ukurasa mpya wa kisiasa ukiwa na mtu mmoja umemwachia huru, siyo yeye peke yake, unakuwa umeigusa roho yake, familia yake na ukoo wake. Unawatoa kwenye masononeko, unaifanya nchi iwe na furaha na kinyume chake ukiwa na mtu mmoja amewekwa ndani, ametekwa au amepotezwa, siyo yeye peke yake bali ukoo mzima unakuwa kwenye masikitiko na unatengeneza Taifa lenye huzuni. Huo ni mchango wangu wa pili niliotaka kuusema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu na la mwisho, ninawakumbusha mabosi wangu, wananchi wa Tunduru, kwanza imesemwa juu ya kuboresha huduma za maji; Tunduru tuna mradi mkubwa sana wa maji. Pale Tunduru Mjini usambazaji wa maji hivi sasa upo kwa wastani wa kilomita 3.3, hivi mtandao wake. Tuna mradi mkubwa wa maji wa shilingi bilioni 3.4 ambao ungeweza kusaidia mtandao wa usambazaji wa maji Tunduru ufikie kilomita 92, lakini ule mradi mpaka sasa unasuasua. Tunaitaka Serikali ilitazame hili kwa sababu, tunaamini ni game changer katika kuboresha maisha ya Wanatunduru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine linalowahusu mabosi wangu, Wanatunduru, ni suala la umeme. Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Chilombe yupo hapa na tunashirikiana vizuri, ataendelea, ni mtaalam wa umeme, lakini niseme hivi kwamba, pale Tunduru tuna mradi mkubwa sana wa umeme ambao ukikamilika utatupa megawatts 120 wakati mahitaji yetu ni megawatts nne. Maana yake ni Tunduru tutakuwa na umeme mwingi sana wa ziada, tunasubiri kwa hamu mradi huo uweze kukamilishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa ukitazama mradi unasuasua kwa sababu, mkandarasi hajapata fedha za kuendelea na mradi. Vifaa viko site amekwishapeleka vifaa vingi pale, lakini umeme wa uhakika hujapatikana, ndiyo maana hivi sasa ukienda Tunduru, mimi nina hakika, tutakuta eneo ambalo linaweza kuingia katika kitabu cha historia ya maajabu ya kukatikakatika kwa umeme. Tunduru inaweza ikawa namba moja kwa sababu, umeme unakatika mara 20 kwa siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wataalam wanatwambia ni kwa sababu, njia ya umeme inapita katika miji mingi. Haya ni maelezo ya kitaalam, mwananchi wa kawaida hayaelewi hayo, yeye anadhani Serikali imelala na imefeli. Kwa hiyo, tunaomba mkandarasi yule apewe fedha.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. ADO S. ADO: ...ili mradi uendelee. Ahsante sana.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninampongeza anayetoa hoja, lakini ninatokea Tunduru, umeme haukatiki mara 20 kwa siku. Ahsante. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Unaipokea hiyo Taarifa?
Muda wako pia, umeisha.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, muda wangu umeisha watakaotuhukumu kama umeme unakatika mara 20 ama la, siyo Bunge hili ni Wanatunduru, tukutane site. Ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kuniona, ili niweze kutoa mchango wangu katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nina imani kwamba, kutokana na nafasi yetu tumekuwa tunapewa hapa uwiano wa kuchangia; kwa siku sisi ACT tumeambiwa, kwa nafasi yetu ya Waheshimiwa Wabunge tisa, tuna nafasi ya kuchangia angalau mchangiaji mmoja kwa siku, huwa tunapewa hivi kutoka Ofisi ya Katibu pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naona hizi ni dakika za jioni, isije ikahesabiwa dakika za jioni tukakatwa juu kwa juu tukashindwa kujipambanua. Ule msingi wa kwamba, nafasi yetu ya kuchangia mchangiaji mmoja izingatiwe, ili Bunge lipate kusikia mawazo yetu pia. Nimepata faida ya kuwasikia wachangiaji wenzangu, Waheshimiwa Wabunge na wengi wamejikita katika kuchambua hoja mbalimbali ambazo zipo katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini mimi nitachukua njia tofauti nikitambua kwamba, Hotuba ya Waziri Mkuu katika Bunge la Bajeti siyo hotuba ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo hotuba ya kisekta, hii siyo hotuba itayojikita kwenye maduhuli tu ya Serikali na namna ya kuyatumia. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ndani yake inabeba tafakuri ya mwaka uliopita wa fedha. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inabeba maono ya Serikali katika mwaka ujao wa fedha kwa hiyo, mimi nitajielekeza katika maeneo ambayo kwa maoni yangu yamebeba ukimya mkubwa sana katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Yako maoni, yako maeneo, mimi ninaona yalipaswa kuwemo kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu au yalipaswa kupewa uzito wa kipekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona hotuba hii imebeba ukimya katika maeneo hayo na kwa ajili ya muda nitayataja machache. Eneo la kwanza, nimesoma Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kurasa zote 122; sijaona kwenye ukurasa wowote, sijaona kwenye aya yoyote, sijaona kwenye sentensi yoyote, kuhusu Katiba Mpya, Tume Huru ya Uchaguzi na mageuzi ya kisiasa nchini kwetu. Hatua hii ya Hotuba ya Waziri Mkuu kukaa kimya juu ya jambo hili muhimu sana sisi tunaipa tafsiri kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hitimisho ninalolijenga mimi, mpaka nitapokuwa proved wrong wakati ujao, hii inanipa ishara kwamba, Serikali imeipuuza, hailipi uzito na haitaki ajenda ya Katiba Mpya, huo ndiyo msimamo wangu. Sasa ninatoa ujumbe kwa Serikali na Chama Cha Mapinduzi, ujumbe wa kwanza ni Watanzania si wajinga wanaelewa hali halisi ya kisiasa ya nchi yetu na wanajua bila Katiba Mpya, bila Tume ya Uchaguzi na bila mageuzi ya kisiasa ndani ya nchi yetu…
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ado, kuna Taarifa.
Mheshimiwa Ester Bulaya.
TAARIFA
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru tu kwa mchango wake, Mheshimiwa Ado, mdogo wangu na mimi nilikaa sana hapo. Ninaomba nimpe Taarifa kwamba, kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumedhamiria ndani ya miaka hii mitano ya Awamu ya Sita Watanzania watapata Katiba Mpya. Ukimuangalia anavyozungumzia suala la Katiba Mpya amemaanisha, ndiyo maana kwenye ilani ya chama chetu tumeiweka. Ninaomba nimpe hiyo Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa unaipokea Taarifa hii?
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa nyingine.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa mwenyekiti, Taarifa ya Mheshimiwa Bulaya siipokei. Siipokei kupitia hoja yangu namba mbili, ambayo ninaelekea kuitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujumbe wangu kwa Serikali na Chama Cha Mapinduzi, ujumbe namba mbili, Katiba Mpya sio ajenda ya CCM, Katiba Mpya sio ajenda ya Serikali, Katiba Mpya ni ajenda na mali ya Watanzania. Ukimya huu katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu unamaanisha Serikali imeihodhi ajenda hii.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ado, kuna Taarifa. Mtoa Taarifa yuko wapi? Sawa, Naibu Waziri.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumpa Taarifa Mheshimiwa Ado kwamba, Serikali iliyopo madarakani ni ya Chama Cha Mapinduzi na inatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa hiyo, hakuna namna utatofautisha Chama Cha Mapinduzi na Serikali iliyoko madarakani na Watanzania. Ahsante.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ado, unaipokea Taarifa hiyo?
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa mwenyekiti, siipokei Taarifa hiyo. Sijasema Serikali ni mali ya nani, hilo ni somo lingine la Katiba, mkufunzi yuko pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema Katiba Mpya ni mali ya Watanzania. Watanzania wana haki kwenye hotuba kama hizi zinazobeba maono, kujua mchakato wao wa Katiba Mpya unakwenda wapi.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Inatoka wapi Taarifa. Ndiyo, Mheshimiwa Kihenzile.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninakubaliana na Mheshimiwa mchangiaji kwamba, Katiba Mpya ni mali ya Watanzania, lakini pia ninamkumbusha mali za Watanzania ni pamoja na ardhi, fedha na vinginevyo. Kwa sasa mwenye mkataba wa kuvisimamia ni Serikali na Serikali ya sasa ni ya CCM kwa hiyo, huwezi kuvitenganisha.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ado unaipokea taarifa hiyo?
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa hiyo. Kwa sababu ninaona nakwamishwa kwamishwa hapa, gari lina nasanasa niiache ajenda hiyo ujumbe umefika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ajenda ya pili ambayo ninaona ni ukimya kwenye hotuba ya Waziri Mkuu ni vita dhidi ya ufisadi, rushwa na ubadhirifu. Sijaona kama imepewa kishindo kinachostahili. Ninaamini Hayati Sokoine angefufuka leo wala nisingepata shida kujua ajenda yake namba moja ingekuwa ni ajenda gani. Ninafahamu... (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa, niko hapa taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kumpa taarifa Mheshimiwa Ado kwamba, unapozungumzia mtu ambaye tangu ameapa, tangu tumemdhibitisha kwenye Bunge hili kwa kinywa chake, kwa vitendo kuzungumzia masuala ya ufisadi na kukemea ubadhirifu na kukemea uzembe ni Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba. Kwenye hotuba yake Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini yake yeye, kama Msimamizi Mkuu wa Serikali atahakikisha wazembe, wabadhirifu watachukuliwa hatua na wananchi wa Tanzania waweze kupata maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana mdogo wangu leo alikuwa hajajiandaa kuchangia. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ado unaipokea taarifa hiyo?
MHE. ADO S. ADO: Siipokei taarifa hiyo. Mimi ninafahamu rejea ya uchambuzi, ni hotuba ya Waziri Mkuu. Ninaweza kumweleza Waziri Mkuu wapi amezungumzia juu ya rushwa na ufisadi. Alizungumzia ripoti ya CAG na commitment ya Serikali, kwa maoni yangu mimi, Waziri Mkuu hajatoa uzito unaostahili kwenye hotuba yake kwa ajenda ya rushwa na ufisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uniruhusu nitoe mfano tu nimepigwa breki sana hapa.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ado kuna taarifa. Kanuni zetu zinaruhusu. Kuna taarifa ninaomba uipokee.
TAARIFA
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpe taarifa mzungumzaji rafiki yangu Mheshimiwa Ado, ninadhani atakuwa hajaisoma vizuri hotuba ya Waziri Mkuu. Ukisoma hotuba ya Waziri Mkuu kwenye eneo lote alilozungumzia utekelezaji wa shughuli za Serikali ameeleza kuhusu vita dhidi ya rushwa na ufisadi kwa ujumla, lakini ameeleza kwenye maeneo mahsusi.
Mheshimiwa Mwenyekiyi, Waziri Mkuu alipozungumza kuhusu ripoti ya CAG amesema, alipozungumza kuhusu kasi ya kuongeza ukusanyaji wa mapato amesema, kuhusu kuzuia kuvuja kwa mapato, hiyo ndiyo lugha ambayo Waziri Mkuu amesema (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri Mkuu ya masaa mawili lisaa limoja asingeweza kusema kila kitu, huwezi kumpangia aiseme kwa namna gani, lakini Waziri Mkuu ameisema na ujumbe umeenda nasi kama Wabunge tunatakiwa tuifanyie kazi hotuba ya Waziri Mkuu. Ninakushukuru. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ado ninakupa nafasi upokee taarifa hiyo na muda wako pia umekwisha.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawaacha kwa tafakuri ndogo tu na ninaomba unitendee haki kwa dakika moja tu halafu mtaona kama mimi nilikuwa naelekea wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira ya sasa ambayo tunapokea taarifa kwamba Serikali imeingia katika mtindo wa kuwa na makubaliano ya pembeni nje ya Mahakama za Kimataifa kuwalipa wanaotudai mabilioni ya fedha, mazingira ambayo yana harufu ya ufisadi, kwa mfano malipo ya bilioni zinazofikia 268 kwa Benki ya Standard Charter ambayo hiyo...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ado muda wako ulishaisha.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuhusu taarifa na muda, mimi ninavyoyaona mazingira ya ufisadi nchini sijaridhika na uzito ambao Waziri Mkuu ameuweka kwenye hotuba yake kwa ajenda ya ufisadi, mengine tutachangia kwa maandishi. (Makofi)