Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Chacha Mwita Wambura (4 total)

MHE. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii kwa ajili ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Nianze kwa kuipongeza Wizara ya Madini, ndugu yangu Mavunde kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, lakini pamoja na hayo ninaomba kuuliza swali moja.

Mheshimiwa Spika, tunajua kabisa kwamba suala zima la double taxation limekuwa halikubaliki lakini kwenye Wizara hii ya Madini suala zima la mrabaha tumeona double taxation mara kadhaa ikifanyika. Kuna baadhi ya mikoa ambapo tuna-charge mara mbili. Mara moja tuna-charge wakati mchimbaji anavyokuwa anagawa mawe pia wakati mwingine mchimbaji huyu aki-process akipata dhahabu akifika kule sokoni tena anatozwa mrabaha. Je, Wizara imejipanga vipi au ina mpango gani kuhakikisha kwamba suala zima hili la double taxation tunaliondoa na huyu mchimbaji aende kulipa kodi moja kwa mara moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ninapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba kodi zilizoidhinishwa rasmi na Wizara ni kodi ya mrabaha, kodi ya ukaguzi wa leseni na ile ya service levy inayokwenda kwenye halmashauri. Hizi tozo anazoongelea Mheshimiwa ni tozo ambazo watu wanapotoa madini mgodini na wakati huo ni mawe tu, anayetoa mawe mgodini, anapoyapandisha pale siyo yeye anayepeleka sehemu ya kuchakata yale madini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hakuna namna sisi tunaweza tukasubiri yaende mpaka kule mwisho wa eneo itakapotumika kuweza kuchaji. Kwa hiyo, anatozwa kwa asilimia ya mawe aliyogawa pale baada ya kutoa na yule anayekwenda kuchakata anawekewa kiwango ambacho kinalingana na zile tozo za Serikali.

Mheshimiwa Spika, tuko katika mpango wa kuhakikisha kwamba katika migodi yote uchenjuaji ufanyike palepale ili mawe yotozwe kodi ya Serikali baada ya kuwa yameshachakatwa.
MHE. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini kwa majibu yake mazuri, lakini niseme tu kwamba wote humu ndani tunajua kwamba tunazalisha dhahabu nyingi Tanzania na hususani katika Mkoa wetu wa Geita, lakini dhahabu yote hii tunai-export, tunaisafirisha kwenda nje bila kuitengenezea vifaa vinavyotokana na dhahabu. Tukiweza kutengeneza vifaa hivi kama pete, mikufu na vinginevyo ambavyo vinatokana na dhahabu tutaenda kuongeza ajira, mapato, lakini pia tutakuwa sasa tunatengeneza Tanzania tuna-export, tutategemea tutopata wageni, lakini tutapata watalii.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuhakikisha kwamba tunaanzisha kituo maalum cha utengenezaji hivi vitu ambavyo vinatokana na dhahabu ili basi tuweze kuhakikisha kwamba vijana na wajasiriamali wa Geita wanaweza kuhusika moja kwa moja kwenye mnyororo huo wa utengenezaji wa vitu hivi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; endapo itatokea Serikali haina mpango wa moja kwa moja wa kuanzisha kituo hiki, je Serikali iko tayari kushirikiana na sekta binafsi au Halmashauri ya Manispaa ya Geita kuwawezesha kuanzisha vituo hivi, maana ninaamini kabisa kwamba kwenye Geita na Taifa hili litaenda kuwa na faida kubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Chacha kwa maswali yake mazuri na pia nimkaribishe katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa sababu nina taarifa kwamba hivi karibuni amepata kuelekezwa awe Mjumbe wa Kamati hiyo. Ninajua kwamba ni Engineer mwenye uzoefu na tunahitaji kuvuna hazina ya elimu aliyonayo katika Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nijibu sasa maswali yake kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, viwanda vya kuchakata madini na kutengeneza bidhaa za mlaji wa mwisho (end user products). Tayari zipo katika sehemu mbalimbali nchini kama nilivyoelezea kwenye majibu ya swali la msingi, lakini kwa upande wa huko Geita sasa na kwa sababu Mheshimiwa Mbunge anataka kujua hasa bidhaa zinazotokana na dhahabu ni kweli kwamba sasa hivi dhahabu nyingi inachakatwa, wanachoma, wanatengeneza zile ground bars na zinauzwa hivyo hivyo ila ni kwa Geita tu na baadhi ya maeneo mengine nchini, lakini tayari tuna viwanda vinavyochakata dhahabu na kutengeneza bidhaa za dhahabu.

Mheshimiwa Spika, moja ya mfano hai ambao upo na hata Wanageita wanaweza kwenda kujifunza ni Kiwanda cha Banjul Limited kilichoko Dar es Salaam ambacho kinafanya biashara ya kuchakata madini ya dhahabu na kuuza dhahabu nje kama wanavyouza wengine, lakini pia wanatengeneza vidani, mikufu, pete, bangili, lakini siyo ya dhahabu tu na madini mengine mbalimbali ikiweko madini ya metali pamoja na madini ya vito.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia katika kujibu swali lake la pili kumwelekeza Mheshimiwa Mbunge, ashauriane na Halmashauri yake maana na yeye ni Mjumbe Halmashauri ya Geita siyo maskini, wakitaka kuanzisha kiwanda cha kuongeza thamani ya madini ya dhahabu na kutengeneza bidhaa za mlaji wa mwisho, sisi kama Wizara tuko tayari kutoa ujuzi na elimu kwa kuwaletea wataalam waweze kuanzisha kiwanda ambacho kitahakikisha kwamba dhahabu ile inatengenezewa bidhaa mbalimbali zinazoweza kutumika nchini na Watanzania wote, siyo lazima kuuza bidhaa ambazo zimechakatwa tu kwa asilimia Fulani.

Mheshimiwa Spika, tunaweza kutengeneza bidhaa za mlaji wa mwisho na wako wengi ambao ninapenda kuwapongeza wanaotengeneza bidhaa za madini ya vito hasa kule Arusha ambako kuna kile chuo chetu cha TGC, lakini pia kuna wadau mbalimbali katika mikoa mbalimbali nchini, Mererani pia wanafanya hivyo katika madini ya Tanzanite na Dar es Salaam kuna watu binafsi ambao wanajishughulisha na biashara hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi tuko tayari kama Wizara kuiwezesha Halmashauri ya Geita kwa kuwapa utaalam ili waweze kuanzisha kiwanda cha kuchakata madini au kituo kikubwa kama kile cha Tanzanite City Center.
MHE. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ninamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali ambayo ameyatoa, lakini pamoja na hayo ninaomba niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya ya Mbugani na Kivukoni ni maeneo ambayo kwa kweli yamekaliwa na wakazi wa Geita, lakini ni maeneo ambayo ni ya kibiashara, na kwa sababu hiyo, sasa ningependa kufahamu, je, Serikali haioni haja ya kuja na mpango wa dharura ili kuhakikisha kwamba tunakabiliana na changamoto hii ikizingatiwa kwamba imeshadumu kwa muda mrefu, wananchi wa maeneo haya wamekuwa wakipata hii changamoto kila mvua za masika zinapokuwa zinanyesha?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuuliza swali dogo la pili la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Ninawashukuru kwamba tulipata Mradi wa TACTIC wa barabara wenye urefu wa kilometa 17 pale Mjini Geita na barabara za nguzo mbili Mwatulole, nguzo mbili Mkolani na Nyankumbu mpaka Uwanja.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kupata mradi huu, umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu. Mwanzoni ulikuwa uishe mwaka 2025 mwezi wa Pili, lakini mkandarasi hakuutimiza, akaongezewa muda amalize mwezi wa Kumi, lakini bado mwezi wa Kumi mkandarasi hakumaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningetamani kufahamu sasa, Serikali ina mpango gani na inatoa kauli gani ili kuhakikisha kwamba inamsimamia yule mkandarasi ili mwisho wa siku hii kazi iweze kwisha na wananchi wa Geita Mjini waweze kufaidika na mradi huu ambao umeletwa na umechukua muda mrefu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mpango wa dharura wa ujenzi wa mitaro eneo la Mbugani na Kivukoni, eneo hili tayari upo mtaro ambao ndiyo tumebainisha kwenye tathmini kwamba unahitaji kupanuliwa, lakini maeneo ambako mtaro huu unapita wapo wananchi ambao wamejenga karibia na mtaro huu. Upanuzi wa mtaro huu utatutaka na unatulazimu kwa kweli kuwahamisha baadhi ya wananchi ambao wapo karibu na mtaro huu ili tupate nafasi ya kuupanua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia halmashauri yetu pale Geita Mjini, mwaka wa fedha huu ambao tunapitisha bajeti yake, tumetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuhamisha wananchi hawa ambao ni kama nyumba mbili, tatu au nne hivi ili waweze kupisha na tuweze kufanya upanuzi wa mtaro huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tunao Mradi wa TACTIC ambao ulikuwa awamu ya kwanza miongoni mwa ile miji 12 ambayo tulisaini mikataba 24 ilikuwa ni Geita Mjini. Ni kweli mkandarasi amekuwa akisuasua na Serikali iliamua kuchukua hatua kali za kuvunja mkataba ule baadaye tulipofanya mazungumzo naye ya kina, tulikubaliana mambo yafuatayo na mkandarasi huyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, tulikubaliana aongeze vifaa eneo la kazi, aongeze wataalamu eneo la kazi lakini na ahakikishe kuna flow ya fedha kwenye eneo la kazi. Siyo hivyo tu, tumekubaliana kwamba ili aendelee kukamilisha kazi hiyo, tutamkata fedha (liquidation damage) shilingi bilioni 2.2.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa amekubali masharti yetu, mkandarasi huyo hivi sasa ameshaanza kazi kwa kasi na anaendelea, na hata mpaka jana, alikuwa na material ya lami yanayotosha kuweka kilometa 11 zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Geita Mjini kwamba mradi huu sasa utakwenda kukamilika, na lengo la Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuweka shilingi bilioni 22 kwenye mradi huu, litakwenda kutimia.
MHE. ENG. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri amesema kwamba mapitio yanaendelea. Ninaomba kufahamu kwamba je, Serikali haioni haja ya kufanya mapitio haya kwa haraka ili basi uwanja ule uweze kukamilika na ikiwezekana ukamilike kabla ya mwakani ambapo tunaenda kuwa na mashindano ya AFCON ambayo yataenda kufanyika katika nchi zetu tatu za Afrika Mashariki na ambapo tunaamini Geita ni centre ya Kenya, Tanzania na Uganda?
Mheshimiwa Spika, kama tutaweza kukamilisha uwanja huu kwa wakati basi zile timu zinaweza zikafanya mazoezi au kutumia vile viwanja wakati wa mashindano.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali katika sehemu nyingine tumekuwa tukishirikiana na tukifanya vizuri sana, na tunavyoshirikiana na private sector, je, katika suala hili la viwanja hapa Tanzania, Serikali haioni sasa ni wakati sahihi ya ku-engage private sector ili kushirikiana nao na kuwa-support ili tuweze kupata viwanja vingi zaidi ili tuendeleze michezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Chacha Mwita Wambura kwa kufuatilia ujenzi wa uwanja huu. Pia ninaupongeza uongozi wa Mkoa wa Geita kwa kuwa karibu na wawekezaji hawa hadi kufikia kuweka fedha hizi kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kumpata mkandarasi mshauri, tayari kiasi cha fedha cha shilingi bilioni 3.4 zimetengwa kwa ajili ya ukamilishaji wa jukwaa juu, majukwaa ya watazamaji na sehemu ya kuchezea mpira (pitch) ambapo inakadiriwa kuwa ujenzi utakamilika ifikapo Oktoba, 2026.

Mheshimiwa Spika, kulingana na idadi ya wakazi wa Mkoa wa Geita inayokadiriwa kufikia milioni tatu kutokana na sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2022, uwanja huu Serikali inauona kama ni sehemu ya kuleta tabasamu kwa Watanzania walioko katika Mkoa wetu wa Geita.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kumwahisha mkandarasi kuweza kukamilisha ujenzi wa uwanja huu, tunao uhakika kabisa kwamba uwanja huu wenzetu wa Wizara ya Michezo wanaweza wakauona kama ni sehemu ya AFCON ya mwaka huu kama utakamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, Serikali inamhakikishia Mheshimiwa Mwita kuendelea kufuatilia kwa ukaribu ili kuhakikisha uwanja huu unaweza kutoa huduma hii ya michezo.