Primary Questions from Hon. Chacha Mwita Wambura (3 total)
MHE. CHACHA M. WAMBURA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Kituo cha Kuongeza Thamani na Soko la Bidhaa za Dhahabu katika Mji wa Geita?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuimarisha uongezaji thamani wa madini katika Mkoa wa Geita ili kuhakikisha manufaa ya rasilimali madini yanabaki nchini. Kutokana na uzalishaji mkubwa wa dhahabu, mkoa huu umewekewa miundombinu muhimu ikiwemo kiwanda kikubwa cha Kusafisha Dhahabu vya Geita Gold Refinery (GGR) na African Eyes Refinery na pia kuna viwanda vidogo vya teknolojia ya kisasa ya uchakataji wa madini ikiwemo mifumo inayojulikana kama (CIP (Carbon in Pulp)/CIL (Carbon in Leach)) pamoja na Vituo vya Umahiri vya Lwangasa na Katente vinavyosimamiwa na STAMICO. Hatua hizi, kwa kuzingatia sheria na sera zilizopo, zimefungua fursa kwa wadau mbalimbali kushiriki katika soko la bidhaa za madini Mjini Geita ikiwepo masuala ya usonara.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kiujuzi, kiuwekezaji na kisheria ili kuimarisha uongezaji thamani madini nchini. Aidha, Wizara kupitia Kituo chetu cha Jimolojia Tanzania (Tanzania Gemological Center) ambacho kiko Arusha) inaendelea kutoa mafunzo ya vitendo ya uongezaji thamani wa madini na kuandaa wataalam wa utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na dhahabu, fedha na vito. Hivyo, nitoe wito kwa Mheshimiwa Mbunge kuwahamasisha vijana wa Mkoa wa Geita hususani Jimbo lake la Geita Mjini kuchangamkia fursa hizi ili kujiajiri, kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya Taifa. Ahsante sana.
MHE. CHACHA M. WAMBURA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga na kukarabati mitaro katika Mitaa ya Mbugani na Kivukoni Geita ili kupunguza athari za mafuriko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Chacha Mwita Wambura, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya maeneo ya Mbugani na Kivukoni yana uelekeo wa maji mengi, hivyo hutokea mafuriko hasa nyakati za mvua nyingi. Ili kukabiliana na hali hiyo, tarehe 12 Disemba, 2025 ilifanyika tathmini ya awali kubaini chanzo cha mafuriko yanayotokea hasa nyakati za mvua za masika pamoja na kujiridhisha na hali ya miundombinu iliyopo hususan uwezo wa mitaro inayotiririsha maji katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini hiyo ilibaini uhitaji wa upanuzi wa baadhi mitaro ili kuruhusu maji mengi yaweze kupita kwa urahisi kuanzia eneo la stendi kuu ya mabasi kuelekea katika maeneo ya Mbugani hadi Kivukoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, TANROADS kupitia kwa Mkandarasi Ms. Yamma Contractors Co. Ltd anaendelea na upanuzi wa mitaro hasa katika maingilio ya maji maeneo ya Shilabela pembezoni mwa barabara kuu ya Mwanza – Geita kwa gharama ya shilingi milioni 460.
Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli hiyo kwa mujibu wa mkataba inatarajiwa kukamilika tarehe 15 Mei, 2026. Aidha, Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inaendelea kufanya tathmini ya kina kubainisha gharama za upanuzi wa mitaro katika maeneo ya Mbugani na Kivukoni. Baada ya tathmini hiyo ambayo itakamilika mwezi Mei, 2026 Serikali itaanza upanuzi wa mitaro hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ENG. CHACHA M. WAMBURA aliuliza:-
Je, hatua gani zimefikiwa katika kuandaa mpango wa kuendeleza na kukamilisha ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu - Manispaa ya Geita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): alijibu:-
Mheshimiwa Spika, uwanja wa mpira wa miguu - Geita ulianza kujengwa mwaka 2021 kwa kutumia fedha za uwajibikaji wa kijamii wa mashirika (CSR) kwa gharama ya shilingi bilioni 5.46 kupitia mgodi wa Geita Gold Mine. Hata hivyo, ujenzi ulisimama mwaka 2023 ukiwa 71%, baada ya Mkandarasi EFQ Co. Ltd kusitishiwa mkataba kutokana na mabadiliko ya kanuni ya miradi ya CSR.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na mgodi wa Geita Mine Ltd imepata mkandarasi mshauri NORPLAN ambaye amefanya mapitio ya gharama halisi za kukamilisha ujenzi wa uwanja huo na kiasi cha shilingi bilioni tano zinahitajika. Aidha, Serikali inaendelea na mapitio ya gharama zilizowasilishwa na mkandarasi mshauri ili kuweza kuendelea na ujenzi kupitia fedha za CSR zitakazotengwa katika mwaka 2026/2027.