MHE. KASSIM A. MBARAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani sana. Nina maswali mawili ya nyongeza: -
(a) Je, ni lini sasa Serikali itaamua kuingia ubia na wadau mbalimbali wa michezo wenye viwanja mbalimbali ndani ya Taifa hili ili kuweza kuviendeleza, kuviimarisha na kuviboresha viwanja hivyo ili kuondoa kero na adha ya viwanja mbalimbali nchini kufungiwa mara kwa mara?
(b) Je, ni lini sasa Serikali itakuja na mpango mkakati wa kutosha ndani ya Mkoa wa Tanga tuwe na uwanja mkubwa wa kisasa wa mpira, kwa sababu mpaka sasa hivi Serikali haina uwanja wowote wa mpira mkubwa wa kisasa wenye kukidhi viwango na haja ndani ya Mkoa wa Tanga, ukiacha kituo kilichokuwepo cha TFF katika Kata ya Mnyanjani? Ni lini? Tuweze kupata majibu hayo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Kwanza ninampongeza Mheshimiwa Amari Mbunge wa Tanga Mjini kwa maswali mazuri yenye kujenga, lakini halikadhalika kwa kuendelea kuwasemea kwa sauti kubwa wananchi wa Jiji la Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilishaanzisha mazungumzo na Chama cha Mapinduzi ambacho chenyewe ndicho kimekuwa na viwanja vingi katika Mikoa mbalimbali nchini, ili kuona namna ambavyo tunaweza kuingia ubia kwa utaratibu unaokubalika kwa mujibu wa sheria ili Serikali iweze kuvikarabati na kuviendesha viwanja hivi na wananchi wapenda michezo nchini wapate maeneo kwa ajili ya kufanya shughuli za michezo; iwe ni aidha kwa burudani, kwa kuweka afya zao sawa, ama kama ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mazungumzo haya hayajafa, yanaendelea na tutakapokuwa na taarifa ya nini kimefikiwa, na utaratibu gani utatumika, tutakuja kwenye Bunge lako Tukufu kuwafahamisha wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili kuhusu uwanja wa kisasa mkoani Tanga, ni kweli Serikali Awamu ya Sita chini ya mwanamichezo namba moja Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafahamu haja na hamu ya wananchi wapenda michezo kote nchini kuona kunakuwa na ongezeko pamoja na uboreshaji wa maeneo mbalimbali ya michezo nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili jambo siyo kwamba tumelifumbia macho. Kwa sasa Serikali imejielekeza kwenye ujenzi wa miundombinu itakayotumika kwa ajili ya mashindano ya AFCON, ambapo tunajenga uwanja mpya wa kisasa Jijini Arusha, tunafanya ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini tunajenga Uwanja wa Dodoma, halikadhalika na viwanja 15 vya mazoezi, pamoja na Uwanja wa Fumba kule Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakapomaliza azimio hili la kuhakikisha tuna miundombinu sawasawa kwa ajili ya ku-host AFCON, tutajielekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya michezo katika mikoa mbalimbali. Serikali hivi tunavyoongea imeshaanzisha mchakato wa uanzishaji wa taasisi mahususi kwa ajili ya ujenzi na usimamizi wa miundombinu ya michezo ambayo itaitwa SIMA, na ambayo hivi karibuni pengine itakuwa tayari kuanza kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo lake ni kuhakikisha kila mkoa na kila halmashauri nchini inakuwa na miundombinu sahihi ya michezo kwa ajili ya wananchi wapenda michezo.