Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JOHN J. NCHIMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu mpendwa aliyoitoa jana ambayo kimsingi iliakisi na kuonesha wazi nia na dhamira ya wazi kabisa ya Serikali yetu ya kutatua matatizo yanayoikabili nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninapenda kuchangia katika suala zima la ukombozi wa kiuchumi na maendeleo ya nchi yetu. Binafsi pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa, lakini bado ninaendelea kuamini kwamba ukombozi wa kiuchumi wa nchi hii na kuwafanya wananchi wetu kuacha kuendelea kumiminika kutoka vijijini kuhamia mijini; ni kuendeleza kwa juhudi kubwa mambo ya msingi ya kimaendeleo katika maeneo ya vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna yoyote ile, ni lazima tuje na jibu la kimsingi sana la kuwakomboa wakulima wetu, wanapolima kuhakikisha wanapata masoko, tunawasaidia wanalipwa kwa wakati, lakini pia tuwe na majibu ya zile taasisi mbalimbali zilizoundwa na Serikali kwa ajili ya kuwasaidia wao kimaisha kama tunavyoongelea vitu kama COPRA, Bodi za Kahawa, Bodi za Mbolea na kadhalika. Serikali lazima ihakikishe kwamba hizi zinafanya kazi vizuri na kwa uadilifu mkubwa ili kuwafanya wakulima wetu waweze kuwa na uhakika wa kwamba wanachokilima kinarudi kwao na kuwapatia faida ili waweze kuendesha maisha yao na familia zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunakabiliwa na matatizo makubwa katika maeneo ya vijijini. Mambo mengi yamjadiliwa, lakini kwa kuwa hii ni hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na huenda nisipate nafasi nyingine ya kuchangia kwa kina kama leo. Hivyo ninaomba sana, pamoja na yote yaliyosemwa, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu yupo hapa, bado tunalo tatizo kubwa sana hasa maeneo ya vijijini, miradi ya maji kule imekwama kwelikweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo sehemu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini yeye kama msimamizi mkuu wa Serikali, kwa kweli ninaomba aliangalie kwa jicho la pekee sana eneo hili. Mathalani katika wilaya yangu, Vijiji vya Mbanga, Lituhi, Puru, Nangombo, Ngendere, Ngumbo, Malungu, Lihuli, kote kuna miradi ya maji iliyowekwa, lakini miradi hii yote hakuna hata mradi mmoja unaoendelea mpaka sasa imesimama na hivyo kuwapatia maisha magumu sana wananchi wa vijijini ambao wengi wao wanatamani waje mijini kupata huduma bora wakati wangebaki kule na kulisaidia Taifa letu katika ukuzaji wa uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuzunguka na kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya Chama katika mikoa mbalimbali na wilaya mbalimbali. Mheshimiwa Waziri Mkuu anafanya kazi kubwa sana kwa niaba ya Serikali. Hata hivyo, ninaendelea kutoa rai kwamba kazi hii anayoifanya ni lazima iendane na kuunda controls, kuunda miundombinu ya Serikali itakayoweza kusimamia huko chini wanapoondoka na miradi inapokwenda iweze kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, controls hizi zitafanya kwamba si lazima kiongozi apite mwenyewe physically ili kupata taarifa ya maovu yaliyokuwa huko chini, ubovu na utekelezaji wa kazi huko chini uwe na muundo rasmi unaoweza kufanya Serikali Kuu kufahamu kila mahali nini kinafanyika, nini kinaendelea na matokeo yake yakaja huku kwa ajili ya utekelezaji. Sasa hivi hapa tukiongea karibu kila Mheshimiwa Mbunge atakwambia kuna miradi iliyokwama kwake na Serikali Kuu kwa muda mrefu haina taarifa na haijachukuliwa hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukiendelea kujenga Serikali ambayo itasubiri mpaka Viongozi Wakuu wafike kule ndiyo waweze kutatua yale matatizo na kuyaona, itatuchelewesha kama nchi. Tujenge controls, Wizara ya TAMISEMI ihakikishe inakuwa decentralized, inashuka chini kwenye halmashauri huko chini kuzisimamia. Ikiendelea kusimamia kutoka pale juu ni ngumu sana kufika na kuelewa nini kinafanyika huko chini na kurekebisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Serikali inabana matumizi kwa sababu tuliambiwa na Mheshimiwa Rais hapa kwamba masuala yanayoendelea kiuchumi duniani siyo rahisi kupata miradi na fedha nyingi tulikuwa tunapata kwa wafadhili. Sasa katika hili, ninaomba pia kuchangia na kutoa mawazo kwamba moja ya sehemu kubwa sana ambayo Serikali inatumia matumizi makubwa sana ukiangalia kwenye bajeti, ni matumizi ya magari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutoa rai kwamba, sasa hivi imefika wakati maalum ambapo Serikali ianze kuangalia aina ya magari yanayotumika na kazi anazofanya mtumishi. Unakuta mtumishi yeye ni Mkurugenzi, lakini anafanya kazi Dodoma tu hapa, hatoki nje ya Dodoma, kazi yake iko hapahapa Dodoma na njia zote ni za lami, lakini anatumia V8 ya shilingi 480,000,000/=. Kwa nini asingetumia gari ya kawaida kwa sababu yuko eneo la mjini hapahapa na haendi mbali. Serikali inatumia V8, Land cruiser zaidi ya mia nne na kitu ambacho wengine hata hawakupaswa kuyatumia hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho sasa hivi ninawakumbusha hata hawa ambao wanayatumia hayo magari kwamba sasa hivi tuna tatizo la mafuta. Utakuta sasa hivi bado madereva wetu wanakaa na haya magari asubuhi mpaka jioni wanatusubiri huku yanaunguruma tu, yanakula mafuta tu pale. Sasa unajiuliza haya mafuta wanajua yananunuliwa kwa dola? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni gharama ya Serikali, mtu anamsubiri bosi wake, anaungurumisha gari ya Land Cruiser asubuhi kuanzia saa mbili mpaka saa saba mchana linaunguruma eti lisipate joto, sasa lisipate joto namna gani na mafuta haya ni ya Serikali. Tunapotaka kudhibiti matumizi ya Serikali, tuanze na sisi wenyewe viongozi, tudhibiti matumizi ya aina ya magari tunayotumia lakini pia na matumizi ya mafuta yanayotumika na magari yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukifika kwenye gari lako muulize dereva wako kwa nini unaungurumisha gari toka asubuhi mpaka saa saba, haya mafuta ni kodi ya wananchi. Kwa hiyo, Serikali ina kila sababu sasa hivi ya kuhakikisha inatengeneza controls kuanzia za mtu mmoja mmoja mpaka za Serikali ili tuweze kubana matumizi na kuhakikisha fedha zinazobanwa zinarudi kwa wananchi kwa ajili ya kuleta maendeleo kwao.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuchangia haya, ninaomba kutoa shukrani tena kwa wananchi wangu ambao ninachangia kwa niaba yao na kwamba nitaendelea kuwahudumia na kuwaletea michango yao kadri wanavyonituma na ninashukuru sana kwa nafasi hii.