Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Moses Ludovico Kaegele (5 total)

MHE. MOSES L. KAEGELE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Kijiji cha Tundu ni kijiji chenye wakazi zaidi ya 3000 na kijiji hicho kipo pembezoni mwa Ziwa Tanganyika, namna pekee ya kufikia pale kijijini ni njia ya maji. Tokea ziwa limechafuka wakazi wa pale hawafikiki. Je, ni lini serikali itatenga fedha kwa ajili ya kufungua Barabara kutoka Kala kwenda Tundu na kujenga madaraja mawili ili wananchi hawa waweze kupata huduma za msingi kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, ninaomba nikiri kuwa Mheshimiwa Mbunge alikwishakuja ofisini kwenye ofisi zetu za TAMISEMI. Tumekwishakaa na watalam, tumeangalia umuhimu wa barabara hii ambayo ipo pembezoni kabisa, lakini inaenda kwenye kata yenye wakazi zaidi ya 3000. Kupitia mradi wetu wa Mheshimiwa RISE tunaangalia uwezekano wa kuweka madaraja; ambapo yanahitajika madaraja takribani matatu; ili tuweze kufungua uchumi kwa eneo lile na kusaidia wananchi wetu wa eneo lile.
MHE. MOSES L. KAEGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaipongeza Serikali kwa majibu ambayo yana matumaini, lakini nina swali moja la nyongeza. Katika vijiji hivyo yapo maeneo ambayo yapo nje ya Hifadhi ya Loasi ya mipaka ya Hifadhi ya Loasi halali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado maeneo hayo yanaendelea kulindwa na watu wa hifadhi; na kwa kuwa wananchi wanaongezeka, lakini ardhi haiongezeki, je, Serikali haioni ni muda mwafaka basi wa kwenda kuangalia hiyo mipaka ili yale maeneo ambayo yapo nje ya hifadhi yaweze kurejeshwa kwa wananchi waweze kujiandaa na msimu wa kilimo ujao kwa ajili ya kuwaepusha na migogoro mingine ambayo inaweza kutokea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali la Ndugu yangu Mheshimiwa Kaegele, kwanza ninampongeza sana kwa namna anavyowapambania wananchi wake hasa katika suala hili. Ni mara kadhaa anakuja ofisini, tunakaa kuzungumzia jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Serikali imepokea ushauri wake na ipo tayari kupeleka wataalamu wake kushirikiana na Halmashauri pamoja na Ofisi ya Mbunge ili kwenda kuhakiki mipaka hii na kutoa ufafanuzi unaofaa kwa maendeleo na maslahi ya wananchi.
MHE. MOSES L. KAEGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Wazir, Kata ya Myula yenye vijiji vitano, ndani ya vijiji vinne vyote hamna maji safi na salama lakini Shule ya Sekondari ya Myula nayo haina maji safi na salama. Ni upi mpango wa Serikali wa dharura wa kupeleka maji safi na salama katika Shule ya Sekondari ya Myula?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niwahakikishie Wabunge na nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ajenda yake hii ya maji. Ninataka nimhakikishie tumejipanga vizuri kwenye bajeti yetu maeneo ambayo nchi nzima ambapo hatujafikisha maji ni vijiji 1,575. Kwa hiyo, mkakati wetu wa Wizara ya Maji ni kuhakikisha bajeti hii katika kipindi cha miaka mitano vijiji vyote ambavyo vimebaki vinakwenda kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. MOSES L. KAEGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti,
ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Nkasi Kusini na hususan Kata ya Kizumbi na Kata ya Ninde, Kijiji cha Lupata, Lyapinda na Msamba havijaunganishwa na aina yoyote ile ya barabara na ni kweli hadi sasa mkandarasi ameshapatikana, lakini hajasaini mkataba.

Je, ni lini Serikali itatoa fedha ili huyu mkandarasi asaini
mkataba na kisha kufungua barabara ya kutoka Lupata – Msamba – Lyapinda ili wananchi waweze kupata usafiri na usafirishaji wa shughuli mbalimbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia mara kadhaa kuhusiana na ujenzi na ukarabati wa barabara hizo. Mimi nimhakikishie tu Mheshimiwa mbunge
kwamba, Serikali tunafahamu kwamba tunahitaji kupeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo na tunaendelea na hatua za kibajeti, tuko kwenye hatua ya kutangaza zabuni, lakini tuko kweye hatua pia za kupata fedha kwa ajili ya matengenezo ya dharura.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutahakikisha tunazipa kipaumbele barabara hizo ili ziweze kutengenezwa na ziweze kupitika vizuri zaidi. (Makofi)
MHE. MOSES L. KAEGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri, maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni kweli kwamba Serikali ilipeleka shilingi 200,000,000 na ikajenga kweli OPD ikakamilika, lakini sasa kituo hiki cha afya kinalisha wakazi zaidi ya 20,000. Ninataka kupata commitment ya Serikali, ni lini sasa jengo la maabara, theatre pamoja na jengo la kujifungua akina mama litaanza kujengwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kituo cha Afya cha Ninde kinapatikana umbali wa kilometa 100 kutoka Makao Makuu ya Halmashauri kwa maana ya wilaya, na changamoto imekuwa kubwa sana na kuongeza gharama kutokana na gharama za usafirishaji. Je, ni lini Serikali itapeleka wataalamu kwenda kufanya tathmini ya kujua gharama na hali ya ujenzi wa majengo haya mengine ambayo yamesalia ili sasa kuwezesha Serikali kutenga fedha inayotosha inapokwenda kule, basi ikakamilishe majengo yote haya kwa wakati? (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kaegele, Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwa kuuliza maswali madogo ya nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nkasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kujibu swali la pili, kwamba tayari timu ya wataalamu wa Halmashauri wakishirikiana na wataalam wa Mkoa, wameshafanya tathmini kuangalia ukubwa wa eneo la kujenga miundombinu hii, majengo matatu muhimu; Jengo la maternity complex, maabara na theatre. Kwa hiyo, tathmini imeshafanyika na wameshawasilisha andiko Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI. Nimhakikishie Mheshimiwa Kaegele, tumepokea andiko hilo na ndiyo sasa tunakwenda kutekeleza mpango wa pili wa bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mwaka 2027/2028 tunakwenda kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki cha afya. Mbali na hilo, tayari tumeshapeleka shilingi 250,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kate. Kwa hiyo, Mheshimiwa Kaegele, ndani ya eneo hilo tayari wananchi wetu wataendelea kupata huduma katika Kituo chetu cha Afya Kate. Ninaomba kuwasilisha.