Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Moses Ludovico Kaegele (2 total)

MHE. MOSES L. KAEGELE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaongeza ardhi kwa wananchi wa Vijiji vya Kasapa, King’ombe, Mlambo, Kala na Ng’undwe kutoka Hifadhi ya Lwafi kwa ajili ya kilimo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hifadhi ya Msitu Loasi ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 346 la 25/10/ 1957 ikiwa na ukubwa wa hekta 33,468. Msitu huu unazungukwa na vijiji vinne ambavyo ni King’ombe, Mlambo, Kilambo Mkorochi na Mpasa. Vijiji hivyo vilibainika kuvamia sehemu ya hifadhi kwa matumizi mbalimbali ya kijamii ambapo Baraza la Mawaziri kupitia Kamati ya Mawaziri nane wa kisekta lilielelekeza Serikali kumega hifadhi ili kupata suluhu ya migogoro hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, mwaka 2023 Serikali ilitekeleza Maelekezo hayo kwa kumega eneo lenye ukubwa wa hekta 10,834 (sawa na ekari 27,050) kutoka kwenye hifadhi na kugawiwa kwenye vijiji kulingana na mahitaji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali haioni haja ya kuendelea kumega eneo la hifadhi kutokana na umuhimu wake wa kiikolojia na kijamii. Hii inatokana na ukweli kwamba hifadhi hii ni chanzo kikuu cha maji ya Mto Loasi na Msalamba. Hali kadhalika, inahifadhi mimea na Wanyama, inasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuepusha migogoro ya wanyama wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine maji yanayotiririka kutoka hifadhi hii huchangia katika maporomoko maarufu ya Kalambo (Kalambo Water Falls) ambayo huchochea utalii na uchumi wa nchi katika ukanda huo. Aidha, Serikali inaendelea kuhimiza wananchi kushiriki katika shughuli za uhifadhi na kutumia hifadhi kwa shughuli rafiki za kimazingira kama ufugaji nyuki ili kujipatia kipato endelevu.
MHE. MOSES L. KAEGELE aliuliza:-

Je, lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Ninde kilichoanza kujengwa tangu mwaka 2013?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Moses Ludovico Kaegele, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi imepokea jumla ya shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya, shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya saba na shilingi milioni 840 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Ninde kilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi mwaka 2013. Aidha, katika mwaka 2018/2019 Serikali ilitoa jumla ya shilingi 200,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na vyoo vya nje. Jengo limekamilika na huduma za wagonjwa wa nje zimeanza kutolewa mwaka 2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu iliyosalia katika kituo cha afya Ninde ikiwemo jengo la wodi ya wazazi (maternity), jengo la upasuaji (operating theatre), jengo la maabara, jengo la wagonjwa wa kulazwa (IPD), jengo la mionzi, na jengo la kuhifadhia maiti (mortuary).

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.