Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Jafar Rajab Seif (83 total)

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niishukuru na kuipongeza sana Serikali kwa majibu haya mazuri. Uhalisia wa site ni tofauti na fedha ambazo zimeelezwa kwenye jibu la msingi kwamba, zinatengwa. Nini Kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba, mafuta haya yanapatikana kwenye halmashauri na Manispaa zetu, sambamba/sawasawa na fedha zinazotengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya shilingi milioni 182 zimetengwa kwa wanufaika 14,695 waliopatiwa mafuta ya lotion na pia, utambuzi unaendelea kufanyika katika maeneo yote. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Stella, kwenye maeneo ambayo bado utambuzi haujafanyika, tuendelee kuwatambua. Ni maelekezo ya Serikali kwa Wakurugenzi wetu kuendelea kuwatambua wahitaji wa mafuta haya.
MHE. NYAMIZI S. MHOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa kwa kuwa, ni mara yangu ya kwanza kuongea katika Bunge hili, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kuwepo mahali hapa, Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, namshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuniteua kuwa Mbunge, Viti Maalum, kundi la Wenye Ulemavu. Bila kuwasahau wapigakura wangu wote nchi nzima, ninawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la nyongeza ni kwamba, Wizara ina mpango gani wa kuajiri Madaktari wa Afya ya Ngozi, maalum kwa ajili ya watu wenye ualbino kwenye hospitali zote za halmashauri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa hawa watu kwenye halmashauri utasaidia kupanga bajeti ambayo wao watakuwa na idadi kamili ya mafuta na hata kufanyiwa check-up, siyo tu lotion; check-up kwa ajili ya watu wenye ualbino kwenye halmashauri zote, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita, kipindi cha kwanza na kipindi cha pili, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kundi hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli tayari tumewaelekeza madaktari wote wa halmashauri ambako kuna uhitaji mkubwa wa wenye changamoto ya ngozi. Hivyo, pamoja na wataalamu wale 5,000 ambao tumewaajiri mwezi Januari, wamo ambao wanahusika na kufanya utambuzi wa changamoto hizi za ngozi, pamoja na kutoa ushauri katika matibabu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nderiananga.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, ninaomba niongeze jambo kwenye eneo la mafuta kwa watu wenye ualbino.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua uhitaji wa mafuta ya ualbino kwa watu wenye ualbino nchi nzima, lakini ninamhakikishia dada yangu, Mheshimiwa Stella kwamba, Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Waziri wetu, Mheshimiwa Wiliam Lukuvi, tunao Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu Tanzania ambao kwa sasa tayari tumetenga fedha. Kupitia kwenye mfuko, tuta-push fedha hiyo ndani ya wiki mbili, tangu sasa, ili iende KCMC ika-produce mafuta mengi zaidi yaweze kusambazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa pili kupitia wenzetu Wizara ya Elimu, tunasambaza mafuta haya kwa wanafunzi. Tunanunua, kama eneo la vifaasaidizi, moja kwa moja yanawafikia shuleni. Kwa hiyo, nawatoa wasiwasi wenzangu wenye ualbino.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema na hili la pili kidogo. Tuna hospitali ambazo ni teule, kama hospitali za kanda. Kwa mfano, kule Mwanza Bugando yanafanyika matibabu hayo ya kufanya screening tangu mwanzo, watoto wanapokuwa wadogo, kwa ajili ya kutambua level yao ya aina ya ngozi, mafuta na kila kitu ambacho wanatakiwa wapate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna KCMC, tuna Ocean Road na tunaendelea kuhakikisha huduma hizi zinaendelea kusambaa hadi chini. Kwa hiyo, nawahakikishia watu wenye ualbino wasiwe na mashaka, tuko vizuri. Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia ya Kazi na Utu Tunasonga Mbele, tutaendelea kupeleka huduma kwao, ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Buchambi, Wilaya ya Maswa ina wakazi wengi, lakini haina kituo cha afya. Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha afya kwa Kata ya Buchambi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa katika Bunge lako Tukufu tayari tulishapeleka fedha za kujenga vituo vya kimkakati katika Majimbo 120. Majimbo mengine 94 tumeshayaombea fedha Hazina, nayo yatapata kwa awamu ili kuweza kukamilisha ujenzi wa vituo hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge Esther kwamba Wilaya ya Maswa ni wanufaika katika ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati. (Makofi)
MHE. NURU I. KASHAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaomba kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Je, ni lini Serikali itakamilisha Kituo cha Afya cha Kazulamimba, Kituo cha Afya cha Kata ya Mwakinzega na ni lini pia Serikali…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge swali la nyongeza ni moja tu.

MHE. NURU I. KASHAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge akiulizia kuhusu Kituo cha Afya cha Kazulamimba. Kituo cha Afya cha Kazulamimba ni pamoja na vituo vya afya 341 ambavyo tumeviainisha. Tutaendelea kutenga fedha za ndani za halmashauri na zile za Serikali Kuu ili kuhakikisha kituo hiki cha afya kinaanza kutoa huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Afya inataka kila Kata kuwa na kituo cha afya, lakini katika Jimbo la Kigoma Kaskazini mpaka sasa Kata za Mkongoro, Mkigo, Nyarubanda, Nkungwe, Mungonya, Kidahwe na Matendo hawana vituo vya afya na wakinamama wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya. Ni lini Serikali itakamilisha sera hii kwa kuleta vituo vya afya katika Kata hizi? Ahsante. (Makofi)


NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Kiza Mayeye, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, kwa kazi kubwa anayoifanya hapa Bungeni ya kufuatilia maendeleo ya Jimbo la Kigoma Kaskazini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kujenga vituo vya afya katika Kata zote. Awali tulianza na zile Kata za kimkakati kulingana na mahitaji na vipaumbele. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Kiza Mayeye, ndani ya awamu hii tunakwenda kujenga vituo vya afya kulingana na vipaumbele katika Jimbo la Kigoma Kaskazini. (Makofi)
MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize swali la nyongeza. Katika Zahanati ya Imalakaseko iliyopo Kata ya Goweko, Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora, Serikali ilitoa shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto lakini wodi hiyo bado haijakamilika. Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi wa wodi hiyo ya mama na mtoto katika zahanati ya Imalakaseko, Kata ya Goweko, Halmashauri ya Wilaya ya Uyui? Ahsante. (Makofi)



NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amegusia hasa katika zahanati ya Imalakaseko, Halmashauri ya Uyui. Kwanza Serikali imeshatenga shilingi milioni 80 kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema. Pia, ninamwelekeza Mkurugenzi kuendelea kutenga fedha za ndani Halmashauri ya Uyui ili kuweza kukamilisha ujenzi wa zahanati hii. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Lukozi ni kati ya vituo vya kimkakati ambavyo vimetengewa fedha na Serikali. Ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunaipongeza Serikali kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kilipelekewa fedha shilingi milioni 250 za awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaombea wale Waheshimiwa Wabunge ambao hawajapata, yale Majimbo 94, lakini tumeshawaelekeza Wakurugenzi wote katika Halmashauri kuendelea kutenga fedha za ndani ili kuhakikisha huduma zinatoka katika vituo vyetu vya afya, na maeneo yote yenye upungufu tutayaombea fedha Hazina. (Makofi)
MHE. HIJA HASSAN HIJA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninaomba nimuulize swali moja la nyongeza. Mwezi Novemba, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara kwenye hospitali moja hapa Mjini Dodoma na wananchi, hususan wazazi, waliipongeza Serikali kwa huduma nzuri za matibabu na dawa, lakini walilalamikia ukosefu wa mabeseni na ndoo, kwa ajili ya wajawazito; Mheshimiwa Waziri Mkuu akaagiza jambo hili litatuliwe. Ninaomba kujua limefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hija Hassan Hija. Tunakumbuka ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye kituo chetu, kile cha afya na akatoa maelekezo yale.

Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiyo maelekezo ya Serikali. Nami kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninawaelekeza Waganga Wakuu wote wa Mikoa, Waganga wote, ma-DMO wa Halmashauri na ma-MOI wetu waendelee kutekeleza majukumu hayo, waendelee kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maana kwamba, sasa mambo ya kuwatoza hivyo vifaa kama mabeseni na ndoo visiwe vikwazo kwa mama zetu wanapokwenda kujifungua katika hospitali zetu
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri na amesema, Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo, lakini maelekezo haya mpaka tunavyozungumza huko kwenye vijiji wajawazito bado wanapeleka mabeseni wembe na mipira. Ninataka majibu ya Mheshimiwa Waziri kuanzia sasa, ni lini hii hali itakoma kwa wajawazito kwa sababu, Kigoma Kaskazini na maeneo mengine bado akinamama wanapeleka mabeseni na vifaa vingine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni maelekezo ya Serikali. Ninarudia kwa kwamba, halmashauri zote nchini tunatoa wito kwa Wakurugenzi, Waganga Wakuu na ma-DMO watekeleze maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa maana maagizo hayo ndiyo maagizo ya Serikali.
MHE. JUMA R. MUSTAFA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Wizara. Kwanza kabisa ninapenda kuwapongeza kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kuzifanya, lakini ninampongeza Mheshimiwa Rais, wananchi wa Jimbo la Igalula wanamshukuru kwenye chanjo ya ruzuku, kuondoa na utambuzi wa mifugo.
Mheshimiwa Spika, nina swali moja la nyongeza; je, Serikali ina utaratibu gani wa kisheria na kiutendaji, ili kuhakikisha sasa maeneo haya yaliyotengwa hayavamiwi na hayabadilishiwi matumizi ili kuweza kuepuka migogoro kati ya wakulima na wafugaji ndani ya Jimbo la Igalula?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Mustafa Kawamba, Mbunge wa Igalula, Halmashauri ya Uyui, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na Sheria mbalimbali ambazo zimekuwa zikitu-guide na zimepitishwa na Bunge lako Tukufu. Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, hii ilikuwa inatoa hati ya Hatimiliki ya Kimila, lakini kuna Sheria ya Ardhi Namba Sita ya Mwaka 2007, ambayo imeainisha mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji, lakini kuna maeneo ya kilimo na malisho ya mifugo, yote yameainishwa katika Sheria hii. Sambamba na sheria hizi pia, kuna Sheria Namba 287, ambayo imewezesha halmashauri kutunga Sheria Ndogo. Kwa hiyo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaziagiza Halmashauri zote nchini zifuatishe Sheria hizi na kuona zinatatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, kwanza ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuweza kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Wilaya ya Sikonge kwa hivi sasa wanakabiliwa sana na ufinyu wa maeneo, kwa ajili ya shughuli za kiuchumi. Wilaya ya Sikonge ina jumla ya mapori tisa na kati ya haya, yaliyo mengi ni mapori ya akiba. Je, Serikali, ni wakati gani sasa haya mapori ya akiba yataanza kutumika, kwa ajili ya hao wananchi, ukizingatia kwamba, kwa kweli wananchi wanahitaji kuendesha shughuli zao za kiuchumi na hasa kilimo, ufugaji, pamoja na urinaji wa asali na kwa hivi sasa, hata viashiria vya uvunjifu wa amani vinaanza kuonekana?
SPIKA: Mheshimiwa swali lako limeshaeleweka. Ahsante.

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Sikonge, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI. Utakumbuka Bunge lako hili kipindi cha Mwaka 2021 mpaka 2025 iliundwa Kamati ya Mawaziri Nane, ambayo ilizunguka nchini kote kuainisha maeneo haya na kufanya tathmini. Hivyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge tathmini ikikamilika kwa wakati watatengewa maeneo ili wapate kufanya shughuli za uzalishaji mali, kilimo na ufugaji.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kuwatengea maeneo wananchi wa Wilaya ya Bunda, Nyatwali, kwa ajili ya ufugaji ambapo maeneo hayo yalitwaliwa na Serikali kurudishwa hifadhini. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kuwatengea wananchi, hasa wananchi wa Mkoa wa Mara kwa ujumla, maeneo ya kulishia wanyama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu hapo awali, swali hilo linaenda sambamba na swali la Mbunge kutoka Sikonge kwa maana ya kwamba ile Kamati ya Mawaziri Nane bado wanafanya kazi na tathmini ili tuweze kuwatengea maeneo wananchi wetu waweze kuendelea na shughuli za uzalishaji.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nini maswali mawili ya nyongeza: swali la kwanza; wakati tukisubiri Serikali ilete fedha, kwa ajili ya ukarabati, je, Serikali haioni ipo haja sasa ya kuanzisha huduma ya upasuaji kwenye kituo hiki, ambayo ni huduma muhimu sana kwa watu wa Masama?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Hospitali ya Wilaya ya Hai iko katikati na inapokea wagonjwa wengi sana wanaotokana na ajali kwenye maeneo mbalimbali kwenye Barabara yetu ya Arusha kwenda Moshi, lakini mpaka sasa hivi hatuna theatre, kwa ajili upasuaji. Je, Serikali ni lini italeta fedha ya kujenga theatre, kwa ajili ya upasuaji katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Hai? [MANENO HAYA SIYO SEHEMU YA TAARIFA RASMI ZA BUNGE]
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saashisha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kituo chetu cha Afya cha Masama, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza maswali ya msingi. Pili, ninamwelekeza Mkurugenzi kuendelea kutenga fedha za ndani na kuanza ujenzi wa jengo la upasuaji katika Kituo chetu cha Afya cha Masama.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tayari halmashauri ilijenga jengo la upasuaji katika Hospitali ya Hai na tayari kazi za upasuaji zinafanyika pale, wataalam wangu wameni-brief. Ninamhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge, kama taarifa hazijafika kwa wakati, ninamwomba DMO aweze kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge, lakini pia, Mkurugenzi anifikishie taarifa sahihi kwa Mheshimiwa Mbunge kwa maana ya kwamba, Hospitali ya Hai imeshaanza matibabu hayo ya upasuaji hadi upasuaji wa mifupa. (Makofi) [MANENO HAYA SIYO SEHEMU YA TAARIFA RASMI ZA BUNGE]
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Serikali iliahidi kujenga vituo vya afya vya kimkakati, ili wananchi wasiendelee kufuata huduma katika umbali mrefu sana. Katika Wilaya yetu ya Kilolo kuna Kata za Kimara, Idete, Ukwega, Kwiugumu na Image, wananchi wanapata mateso sana kufuata huduma za afya na barabara hazipitiki. Mpaka sasa hivi madaraja hayapo…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa uliza swali.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, je ni lini sasa hivi vituo vya kimkakati vitajengwa, ili wananchi wasiendelee kupata mateso makubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilimetenga bajeti ya zaidi ya vituo 120 katika majimbo 120 vya kimkakati, zaidi ya shilingi bilioni 30. Tayari tumeomba fedha zingine, kwa ajili ya majimbo 94 pamoja na yale majimbo ambayo ni mapya, yote yataingia katika mpango huo na tutakwenda kujenga hivi vituo vya afya vya kimkakati. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Hunyari kimejengwa ni miaka mitatu sasa hakina jengo la upasuaji. Wananchi wenyewe wakaamua kujenga jengo na Serikali ikasema itakwenda kuwasaidia kulimalizia. Sasa ni lini jengo hili litakwenda kumaliziwa kwenye Kituo cha Afya cha Hunyari? Ninakushukuru
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Getere. Kwanza tunawapongeza wananchi kwa hatua waliyochukua na kuanza kujenga majengo hayo katika hospitali aliyoiainisha. Ninamwelekeza Mkurugenzi aweze kutenga fedha na kuanza ujenzi wa majengo yanayopelea katika hospitali hiyo.
MHE. CHARLES M. NJAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Kwanza naanza kwa kumshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuletea pesa wiki iliyopita shilingi bilioni 1.4, kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali yetu ya Magunga. Hospitali ya Magunga imezeeka sana, imechakaa na ina umri karibu miaka 73 sasa. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari twende pamoja katika hospitali ile, kwa ajili ya kufanya tathmini, ili ikiwezekana tufikirie kujenga majengo mapya badala ya kuendelea kuweka viraka katika hospitali ile, ambayo inakuwa ni gharama kubwa zaidi kwa Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Charles, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi pamoja na timu ya wataalam tutaongozana pamoja na Mheshimiwa Mbunge kwenda kwenye hospitali hiyo kufanya tathmini na kuendelea kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Karema, Kituo cha Afya cha Kasekese na Kituo cha Afya cha Mwese kuna tatizo kubwa la ukosefu wa Jengo la Mama na Mtoto, Maabara na nyumba za watumishi. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha,ili iweze kukamilisha hivyo vituo vya afya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali kwamba, zaidi ya vituo 532 vimeishatengewa bajeti ya shilingi bilioni 102.08. Kwa hiyo, pamoja na vituo ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameviainisha vimo katika ukarabati huu mkubwa na kuweza kujenga majengo mengine ambayo yanahitaji, kama maabara, ili kuendelea kupata huduma kwa wananchi wetu.
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kuhusu kuboresha huduma katika hospitali yetu ya Manispaa ya Kahama, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Mheshimiwa Naibu Waziri amesema Serikali inatenga bajeti kwa ajiili ya kuboresha huduma kwa kujenga jengo la dharura na kuweka vifaa vya uchunguzi kwa maana ya CT- Scan. Sasa ni lini Serikali ina mpango wa kupeleka CT- Scan kwenye hospitali hii ambayo inapokea wagonjwa wengi sana kutoka hospitali zingine?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni lini sasa Serikali ina mpango wa kuboresha na kukamilisha majengo ya zahanati ambayo yamefikia hatua za lenta kama vile Chalya, Nyandekwa na sehemu zingine za Wilaya yetu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ngayiwa. Kwanza, ninampongeza Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI anatoa michango mizuri kwa ajili ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli kwa idadi kubwa ya wagonjwa ambao tunawapokea katika hospitali hii ya Halmashauri ya Manispaa ya Kahama na uhitaji wa CT- Scan kwa ajili ya upimaji, uchunguzi wa mifupa kwa wagonjwa wetu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa maana ya kwamba ndani ya muda mfupi Serikali imekwishafanya tathmini na uhitaji huo tumeshauona, tunaipeleka CT-Scan pale ili iende kutoa matibabu kuwahudumia wahitaji wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu zahanati nilikwishaeleza hapa kwamba zaidi ya zahanati 1,841 zinakwenda kufanyiwa ukarabati na kumaliziwa maboma, Serikali inajielekeza zaidi katika miradi hii ambayo tayari imekwishaanzishwa ili tuweze kuikamilisha kabla ya kuanza miradi mingine ya zahati na vituo vya afya. (Makofi)
MHE. JOHN J. NCHIMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, Kata yangu ya Mpepo katika Wilaya ya Nyasa ndiyo kata ya pili kwa ukubwa katika Wilaya yangu. Kwa bahati nzuri inapakana na nchi ya jirani ambapo mwaka jana ilisababisha maambukizi ya ugonjwa wa M-Pox kutoka katika nchi ya jirani, lakini kata hiyo mpaka sasa pamoja na unyeti wake haina kituo cha afya. Nini kauli ya Serikali ili kulinda maisha ya wananchi wa Nyasa kutokana na njia hiyo ambayo imeonekana inapitisha magonjwa mengi na bado hakuna sehemu ya afya ya kuwalinda wananchi wangu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa John John Nchimbi, Mbunge wa Nyasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali inaendelea kupambana na haya magonjwa ya mlipuko, kupitia vile vituo vya kimkakati Mheshimiwa Mbunge ataweza kutuambia kama kituo hicho kiende kikajengwe katika kata hii, yeye mwenyewe atatupa uelekeo huo na tutaona namna gani ya kwenda kuboresha katika kituo chetu cha afya hicho na tunaweza tukajenga kituo cha kimkakati katika Jimbo hilo.
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Mitaa hii mitano na siyo Kata, Mitaa hii mitano ilipimwa kama vijiji mwaka 1973. Je, ni hatua gani Serikali inachukua kuwanusuru wakazi wa Kata hii ya Mbalawala wapatao takriban 12,000 ambao wanategemea ardhi hii kwa maisha yao ya kila siku? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wakati Serikali inajiandaa kutwaa Bonde la Mzakwe iliwafidia wakazi wa vilivyokuwa vijiji vya Mzakwe na Mchemwa, baadhi kuwahamishia katika Kata ya Chahwa ambayo sasa hivi iko kwenye Jimbo la Mtumba. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwafidia wakazi wa mitaa hii ya Kata ya Mbalawala ili wapishe Bonde la Mto Ruvu kama ilivyowafidia waliokuwa wakazi wa Vijiji vya Mzakwe na Chahwa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Inyasi, Mbunge wa Dodoma Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na swali la pili, kwa maana kwamba sisi TAMISEMI ndiyo wamiliki wa ardhi, nitakaa na Mheshimiwa Mbunge kuona namna gani ya kuendelea kuwafidia wale ambao hawajapata kwa sababu Serikali imeendelea kutoa fidia katika maeneo mengi sana nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, mimi na Mheshimiwa Mbunge tutakaa pamoja na Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Ardhi kuona namna gani tunaweza tukafikisha maendeleo haya kwa wananchi wetu kwa maana ya kwamba vijiji vimeshapimwa toka mwaka 1973, tuone namna gani sahihi ya kuendeleza eneo hili. (Makofi)
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Spika, ninaomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza kutokea katika swali langu la msingi.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; mpaka hivi sasa ninavyozungumza hapa bado kuna mifugo katika mashamba ya wakulima huko katika Jimbo la Morogoro Kusini. Nini kauli ya Mheshimiwa Naibu Waziri sasa hivi ili iweze kutekelezwa na mifugo hiyo iondolewe katika mashamba ya wakulima?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wizara ina mpango gani sasa katika Jimbo la Morogoro Kusini kuongeza ujenzi wa majosho, malambo pamoja na kasi ya kuelimisha wafugaji juu ya ufugaji bora wa kisasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Mfaume, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa maswali yanayogusa changamoto hizi za wakulima na wafugaji. Sisi Ofisi ya TAMISEMI tunashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Uvuvi na Mifugo na wameendelea kutoa elimu wenzetu Wizara ya Mifugo na pia wanatoa mbegu za ruzuku kwa ajili ya malisho ili kuondoa migogoro hii kabisa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tunaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha mifugo inaondolewa katika maeneo ya wakulima wetu na baadae nitakaa na Mheshimiwa Mbunge pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo ili tuweze kuyaangazia maeneo haya na kupata ufumbuzi wa kudumu.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeendelea kujenga majosho mengi nchini. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge tuweze kuainisha eneo ambalo hasa amelizungumzia ambalo halijapata majosho mpaka sasa ili tuweze kujenga majosho hayo.
MHE. LUCY D. S. KOMBANI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa hii migogoro imekuwa ya muda mrefu sana na inaleta madhara makubwa sana kwenye hizi jamii zetu na kwa upande mwingine tukiangalia tuna wataalam ambao wamesomea utatuzi wa migogoro; je, Serikali haioni haja sasa ya kuwatumia wataalam hawa katika kumaliza haya matatizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2025 hakujaripotiwa migogoro yenye kuleta mapigano katika maeneo mengi nchini. Serikali inamuahidi Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kuwatumia wataalam hawa ili kuweka hali hii ya usalama wa wakulima na wafugaji. Tunaendelea kuhamasisha zile kampeni (kwa mfano, Kampeni ya Tutunzane) ili kuona kabisa wakulima na wafugaji wanavyohitajiana na waweze kuishi katika maeneo kwa usalama na uzalishaji mali uendelee.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, ndani ya Jimbo langu la Nanyumbu hivi ninavyozungumza kuna mgogoro mkubwa wa wafugaji na wakulima na kusababisha mashamba ya wakulima kuliwa na mifugo ya wafugaji. Je, Serikali ina kauli gani kuwalazimisha hao wafugaji ambao wamesababisha hasara kubwa kwa wakulima waweze kulipa gharama zote za uzalishaji na badala yake kuwaachia Polisi kushughulikia suala hilo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mhata, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia migogoro ya wakulima na wafugaji ni eneo sensitive sana na Serikali huwa haijiweki katika eneo la kupendelea, hivyo niwaelekeze wahusika wote wa halmashauri za vijiji na halmashauri zetu waweze kufuatilia mgogoro huo na waripoti kwa wakati ili tuweze kwenda kutatua tatizo hilo. Hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunaweza kuonana baadaye ili tuweze kuona namna gani ya kuli-handle hili bila kuleta pressure katika pande zote. (Makofi)
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa majibu niliyojibiwa ni tofauti na swali nililouliza, ninauliza swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuja Mwibara ili aone nilichouliza cha maboma ya zahanati ya Kigaga, Nambugi na Sikiro, na maboma niliyouliza ya shule ya msingi Mwibara, Sunsi, Gwanza, Busambu, Mwiruruma, Mgara ‘A’ na ‘B’, Sikiro, Majoro, Igundu, Buramba, Berendabufwe na Marama, Kasaunga, Masaunga na Magunga, Kenkombe pamoja na Nampangala ili baadaye afanyie kazi aone utofauti wa alichonijibu na kile nilichouliza? Je, yuko tayari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Kangi Lugola kwa kazi kubwa anayoifanya kuwasemea Wananchi wa Jimbo la Mwibara.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, tumekuwa tukifanya ziara tukiongozwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mimi na Mheshimiwa Mbunge tutafika Jimboni Mwibara na kujionea maboma hayo. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Mwibara kwamba Serikali imejielekeza kukamilisha maboma haya na tutaendelea kutenga fedha.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, tatizo hili la maboma hata katika Jimbo la Itwangi na Solwa ni changamoto kubwa sana. Ni upi mpango mkakati endelevu wa kuhakikisha kwamba yale maboma yaliyoanza kujengwa na wananchi yanakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali inatambua nguvu za wananchi na tunaendelea na utekelezaji wa kuhakikisha maboma haya yote yanakamilika. Mkakati endelevu na wa kudumu, kwanza tumesitisha uanzishwaji wa maboma mengine mapya na tunahakikisha tunakamilisha maboma yote ambayo tumeanzisha katika Majimbo yetu.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza. Maeneo ambayo pia yana changamoto ya kuwa na maboma kwenye sekta ya elimu pamoja na afya ni pamoja na Jimbo la Bunda Mjini. Ni lini sasa watamalizia ili wananchi wapate huduma ya afya na elimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, hata kupitia katika randama zetu za mikoa, tumekuwa tukielekeza kwamba tutenge bajeti hasa katika Halmashauri zetu ili kukamilisha maboma haya. Pia, upo mpango mkakati wa Serikali kupitia fedha za ruzuku ili kuhakikisha tunakamilisha maboma haya nchi nzima.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, ujenzi wa uzio katika vituo vya afya na hospitali zetu huko Halmashauri haujawa kipaumbele, ni ipi kauli ya Serikali kuzielekeza Halmashauri zijenge uzio kwenye vituo vya afya, zahanati pamoja na hizo hospitali za Wilaya?

Mheshimiwa Spika, pia, ninatamani kufahamu, ni upi mpango wa Serikali kupeleka zile fedha ambazo ilikuwa imeahidi kumalizia katika Kituo cha Kamsamba Jimbo la Momba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya msingi, kipaumbele cha Serikali hasa katika hivi vituo vyetu vya afya na zahanati zetu ni kuhakikisha angalau zile huduma za maternity complex, kuokoa maisha ya mama na mtoto. Pia, hatujaacha nyuma kujenga uzio katika maeneo yote ya hospitali.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Neema kwa kuendelea kuwasemea wananchi hawa, nasi tutaendelea kupeleka bajeti kwa ajili ya kujenga uzio.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili aliloelezea kuhusu hiki kituo cha afya, tayari tumeshazungumza kwenye vikao vyetu vya halmashauri, na tulikutana na Wakurugenzi ili kuhakikisha zile fedha ambazo Serikali imezielekeza, ni kweli ziende zikafanye kazi ya kumalizia ujenzi wa kituo cha afya.

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuuliza swali la nyongeza. Kituo cha Afya cha Tinde kimezungukwa na barabara kuu tatu; barabara iendayo Dar es Salaam, Kahama na Mwanza. Kituo hiki hakina uzio. Je, ni nini mpango mkakati wa Serikali kuhakikisha Kituo cha Afya cha Tinde kinajengewa uzio?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Azza kwa kuwapambania wananchi wa Jimbo la Itwangi. Kituo cha Afya cha Tinde ni njia yangu ya kuelekea Jimboni Busanda. Huwa mara zote ninapita pale na tunajionea sote kwa sababu kile kituo kiko njiani.

Mheshimiwa Spika, nilifanya ziara katika kituo hiki cha afya, hakika kinahitaji uzio kwa maana ya kwamba kipo karibu sana na barabara. Pia tunawaomba wenzetu wa TANROADS waweze kuzungumza na wale wafanyabiashara waliopo katika kingo ile ya barabara ili kukipa nafasi kituo na kuendelea kutenga bajeti.

Mheshimiwa Spika, nimeshafanya mawasiliano na Mkurugenzi ili kuweza kutenga bajeti na kufanya tathmini ya uzio huu na hitaji la kibajeti ili tuone namna gani ya kuweza kuanza kujenga uzio.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini kituo chetu cha afya kilichopo Kata ya Kipili, Jimbo la Sikonge, kitajengewa jengo la wagonjwa wa nje (OPD)?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, Serikali tumejielekeza katika mwaka huu wa fedha angalau kukamilisha majengo ya OPD katika vituo hivi vya afya na yaanze kutoa huduma. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, katika mwaka huu wa fedha tutakamilisha jengo hilo la OPD na lianze kutoa huduma.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ninapenda kujua Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini atapanga safari ya kwenda na mimi jimboni ili akajionee hali halisi ya Kata ya Nyamirembe ambayo ni makao makuu ya tarafa ambayo ina wakazi zaidi ya 23,000 na vijiji vinne ambao wanahitaji kwa haraka utekelezaji wa ujenzi wa kituo hiki cha afya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa vile tayari Serikali imeshapeleka fedha za kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kasenga, lakini Kasenga ni moja ya kata zilizoko kwenye Tarafa ya Kachwamba, ambapo kuna kata nne ambazo mpaka sasa hawana gari la wagonjwa (ambulance). Je, Serikali ina mpango gani katika kuhakikisha kwamba wananchi hao wanapata ambulance ambayo itawasaidia katika kuwaharakisha kuwapeleka katika hospitali nyingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya kaka yangu Mheshimiwa Cornel Lucas Magembe, kule tumezoea kumwita mwalimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Magembe kwa kuendelea kuwapambania Wananchi wa Jimbo la Chato Kaskazini. Nianze kwa kujibu swali la kwanza kwamba lini tutafanya ziara katika kata hii yenye wakazi zaidi ya 23,000 ili kujionea hali halisi na kuboresha miundombinu? Nimwambie tu kaka yangu, kwamba Jimbo la Chato Kaskazini liko katika Mkoa wa Geita, na mimi ninatokea Mkoa wa Geita, Jimbo la Busanda. Kwa hiyo, huyu ni jirani yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutatenga muda mimi na yeye tuweze kwenda kuwaona wananchi hao na kuwaambia nini Serikali inaendelea kufanya kwa ajili ya maendeleo yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeshawasiliana na wenzetu Wizara ya Afya, zile ambulance ambazo zimeshafika tuweze kuzitoa na tumalizie taratibu za Kiserikali ili tuweze kuwapatia hasa wahitaji, na hasa zile kata ambazo hazikupata na zile halmashauri ambazo hazikupata waweze kupata ambulance hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimekuwa nikisimama mara kadhaa hapa kuomba ujenzi wa Kituo cha Afya Matamba, kituo ambacho kinahudumia takribani kata tano. Kituo hiki kina hali mbaya sana, hakipo kabisa kwa maana ni cha mwaka 1970. Je, ni lini watajenga kituo kipya cha afya kama ambavyo wameahidi kwenye hotuba zao mara kadhaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sanga. Kwanza, tulifanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete. Ninampongeza tu kwamba, wananchi wa kule ni waungwana sana, walitupokea walitupa na wawadi. Japokuwa kuna miinuko na milima ya hatari, lakini tuliweza kufika tukafanya ziara nzuri tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Sanga, kituo hiki cha afya cha kimkakati tayari pamoja na yale majimbo mengine ambayo bado hayajapata, tumeshapeleka andiko Hazina, na tayari Hazina wameshapitisha andiko letu. Kwa hiyo, fedha zikiingia tutakwenda kukamilisha ujenzi wa kituo hiki cha kimkakati.
MHE. JOSEPH E. TAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya cha Igwisi katika Jimbo la Kaliua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kaliua kwamba pamoja na yeye tayari tumeshawasilisha andiko kuhusu hili ombi la fedha kutoka Hazina. Kwa hiyo, kituo cha afya cha kimkakati katika Jimbo la Kaliua, kwa confidence kabisa nimwambie Mheshimiwa Mbunge awaambie wananchi kwamba tunakwenda kukijenga na kianze kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali ilitoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya kilichopo Kata ya Myangayanga katika Jimbo la Mbinga Mjini, lakini yalijengwa majengo mawili: jengo la OPD pamoja na jengo la maabara. Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Myangayanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa Serikali ilitoa fedha za kujenga vituo vya afya hivi, kwa kuanzia na shilingi milioni 250 katika maeneo yote nchini. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, na nimwelekeze Mkurugenzi kwa niaba ya Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kuendelea kutenga fedha ili kukamilisha miundombinu katika hospitali zetu hizi hizi ili kuendelea kutoa huduma katika vituo vyote vya afya.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Tunduru Kaskazini ni moja kati ya majimbo ambayo hayana kituo cha afya kwa kila tarafa, na kwa kuwa Tarafa ya Nampungu ni tarafa pekee ambayo haina kituo cha afya na haijapata bajeti ya kutosha katika ukamilishaji wa ujenzi wa kituo hicho cha afya, je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Mpungu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pia Jimbo la Tunduru Kaskazini lipo katika mpango wa kupata kituo cha afya cha kimkakati; na kwenye yale maombi tuliyowasilisha Hazina kimo kituo hiki cha afya cha Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kukamilisha baadhi ya majengo katika vituo vya afya ambavyo bado havijakamilika ili kuendelea kutoa huduma kwa watu wetu wa Jimbo la Tunduru kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, Waziri na Naibu Waziri katika Wizara hii wote ni wageni natamani sana wapate fursa ya kufika kuona ujenzi unavyoendelea. Je, ni lini Waziri ataandamana nami kufika katika Kituo cha Iwondo cha Afya, ili aweze kuona ujenzi unavyoondelea pale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Natany Malima. Sisi Wizara tunafanyakazi ya kuzitembelea halmashauri zote nchini na tumekwishaanza zoezi hilo. Namhakikishia tu Mheshimiwa Natany Malima, baada ya Bunge hili tunaweza kuongozana kwenda Jimbo la Mpwapwa katika halmashauri hii na kukitembelea kituo hiki. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Halmashauri ya Mji wa Bunda tunajenga hospitali yetu ambayo iko Kata ya Bunda Stoo. Serikali imetupatia fedha, lakini tangu mwaka juzi, 2024, kuna shilingi milioni 800 zilirudi na hazijarudishwa bado, huo mradi umesimama. Ni lini mtaturudishia fedha zetu shilingi milioni 800 tuweze kukamilisha hospitali ya Wilaya ambayo ina mchango mkubwa kwenye Jimbo la Bunda Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, Serikali imejipambanua katika kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wote. Nawahakikishia wananchi wa Jimbo la Bunda, fedha zao zipo na tutazielekeza kuendelea na shughuli ambazo Serikali ilikuwa imezielekeza. (Makofi)
MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali hili la nyongeza. Kwanza naishukuru Serikali sikivu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia wahudumu 58 katika dirisha hili la ajira za afya kwa Wilaya ya Kyerwa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Kituo cha Afya cha Nkwenda ni kikubwa na kinatoa huduma zaidi ya Kata 19 na sometime kinatoa huduma nje ya Wilaya ya Kyerwa, lakini kituo hiki hakina gari ya uhakika ya wagonjwa (ambulance), je, ni lini Serikali itatupatia gari la uhakika kwa ajili ya kutoa huduma safi kwa kituo hicho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT.JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, tunakumbuka sote humu ndani katika kipindi cha miaka mitano Serikali imenunua jumla ya magari ya kubebea wagonjwa 316, pamoja na magari ya wakaguzi 212 na ambulance za awamu ya kwanza tumeshazigawa katika Halmashauri ambazo ziliainishwa. Nimhakikishie kuwa, awamu ya pili kituo hiki kitakuwa wanufaika wa gari la ambulance.
MHE. ENG. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri amesema kwamba mapitio yanaendelea. Ninaomba kufahamu kwamba je, Serikali haioni haja ya kufanya mapitio haya kwa haraka ili basi uwanja ule uweze kukamilika na ikiwezekana ukamilike kabla ya mwakani ambapo tunaenda kuwa na mashindano ya AFCON ambayo yataenda kufanyika katika nchi zetu tatu za Afrika Mashariki na ambapo tunaamini Geita ni centre ya Kenya, Tanzania na Uganda?
Mheshimiwa Spika, kama tutaweza kukamilisha uwanja huu kwa wakati basi zile timu zinaweza zikafanya mazoezi au kutumia vile viwanja wakati wa mashindano.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali katika sehemu nyingine tumekuwa tukishirikiana na tukifanya vizuri sana, na tunavyoshirikiana na private sector, je, katika suala hili la viwanja hapa Tanzania, Serikali haioni sasa ni wakati sahihi ya ku-engage private sector ili kushirikiana nao na kuwa-support ili tuweze kupata viwanja vingi zaidi ili tuendeleze michezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Chacha Mwita Wambura kwa kufuatilia ujenzi wa uwanja huu. Pia ninaupongeza uongozi wa Mkoa wa Geita kwa kuwa karibu na wawekezaji hawa hadi kufikia kuweka fedha hizi kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kumpata mkandarasi mshauri, tayari kiasi cha fedha cha shilingi bilioni 3.4 zimetengwa kwa ajili ya ukamilishaji wa jukwaa juu, majukwaa ya watazamaji na sehemu ya kuchezea mpira (pitch) ambapo inakadiriwa kuwa ujenzi utakamilika ifikapo Oktoba, 2026.

Mheshimiwa Spika, kulingana na idadi ya wakazi wa Mkoa wa Geita inayokadiriwa kufikia milioni tatu kutokana na sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2022, uwanja huu Serikali inauona kama ni sehemu ya kuleta tabasamu kwa Watanzania walioko katika Mkoa wetu wa Geita.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kumwahisha mkandarasi kuweza kukamilisha ujenzi wa uwanja huu, tunao uhakika kabisa kwamba uwanja huu wenzetu wa Wizara ya Michezo wanaweza wakauona kama ni sehemu ya AFCON ya mwaka huu kama utakamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, Serikali inamhakikishia Mheshimiwa Mwita kuendelea kufuatilia kwa ukaribu ili kuhakikisha uwanja huu unaweza kutoa huduma hii ya michezo.
MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, je, ni mpango upi wa Serikali wa kujenga kiwanja kikubwa cha kisasa katika Mji wa Kahama ambao unakua kwa kasi sana sasa hivi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mipango hii ya kuhakikisha vile viwanja ambavyo vipo chini ya Halmashauri vinajengwa kulingana na vipaumbele vya Halmashauri na jinsi wataalam wetu wanavyoweza kuibua miradi katika maeneo yao. Kama kitakuwa kipo ndani ya Halmashauri kiwanja hicho, tutaweza kuhakikisha kinajengwa kwa wakati, na kama kipo kwa wenzetu Wizara ya Michezo wataweza kutolea majibu katika swali hilo.
MHE. MOSES C. BUJAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, ningependa kuongeza maswali madogo mawili. Kituo cha Afya Budushi kina daktari mmoja, Kituo cha Afya Kadashi kina daktari mmoja, na Kituo cha Afya Isunga hakuna daktari. Ningependa kujua Serikali ina mpango gani wa dharura kuhakikisha kwamba tunapata watalamu katika vituo hivi vitatu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kituo cha Afya Budushi hakina gari la kubeba wagonjwa inapotokea dharura ya kupeleka wagonjwa hao kwenye Hospitali ya Wilaya iliyoko kilometa 33. Je, Serikali itatupatia lini gari la kubeba wagonjwa Kituo cha Afya Budushi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza maswali mawili ya nyongeza na ninaomba niyajibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu upungufu wa madaktari na ndiyo maana tulipata vibali vya kuajiri madaktari 5,000 nchi nzima na baadhi ya madaktari wameshafika maeneo yao ya kazi. Ninawaomba madaktari waliopangiwa kwenda kwenye vituo vyetu vya afya ili wafike kwa wakati, lakini kama haitoshi nimwelekeze Mkurugenzi kuendelea kutoa ajira zile za lazima hasa kwenye maeneo ambayo tuna upungufu kama alivyoainisha Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu magari ya kubebea wagonjwa, tayari tulishapeleka magari zaidi ya 594 katika maeneo yetu kwa Halmashauri zote nchini, lakini pia tunaendelea kuomba magari. Kadiri tunavyoyapokea kutoka Wizara ya Afya, tutaendelea kuyaelekeza katika vituo vyetu vya afya. (Makofi)
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kata ya Ilemba iliyoko Wilaya ya Sumbawanga DC yenye wakazi zaidi ya 27,000 haina Kituo cha Afya, na nimekuwa nikiuliza swali hili, na majibu ya Serikali yamekuwa ni yale yale. On a serious note, ni lini hasa ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Ilemba utaanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Sylvia kwa kuuliza swali hili la nyongeza. Nimhakikishie ya kwamba Wilaya ya Sumbawanga DC kwa kata aliyoiainisha Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie tunakwenda kujenga Kituo cha Afya na kitaanza kutoa huduma kwa watu wetu. Serikali ya awamu hii siyo ya busness as usual, tunakwenda kufanya hakika. Niwahakikishie wananchi wa Kata hii watapata huduma ya afya. (Makofi)
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kuniona. Kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Simiyu, ninaomba kuulizwa swali la nyongeza. Ni lini Serikali ina mpango wa kujenga Kituo cha Afya cha Bunamhala Wilaya ya Bariadi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza kuhusu Kituo cha Afya Simiyu, Bariadi. Katika vile vituo vyetu vya kimkakati Majimbo 94 na yale Majimbo mapya pamoja na Halmashauri ya Wilaya Simiyu na wao ni wanufaika, watakwenda kupata kituo cha afya. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaishukuru sana Serikali kwa kutujengea Vituo vya Afya viwili; Kituo cha Afya cha Miamba na Kituo cha Afya cha Mtii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vituo hivyo vyote viwili hakuna hata kimoja chenye wodi za kulaza wagonjwa. Je, Serikali itaanza lini kutujengea wodi hizi kwa sababu vituo vya afya ni vikubwa, vina kila kitu lakini wagonjwa hawana mahali pa kulala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vyote vya kimkakati vilipoanza kujengwa tulielekeza shilingi milioni 250 ambazo bado hazitoshi, na tayari tumeshawaelekeza Wakurugenzi kuanza kutenga fedha, mapato ya ndani kujenga wodi ambazo zinatakiwa kutoa huduma katika vituo vyetu vya afya. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninakiri kwamba tulipokea gari moja la wagonjwa, na gari moja la usimamizi, kama alivyosema kwenye jibu la msingi Tunaishukuru sana Serikali. Hata hivyo kwa jiografia ya Biharamulo, Wilaya ile ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoongelea Kituo cha Afya cha Nyakahura ni kilometa 82 kutoka Biharamulo Mjini, lakini Waziri Mkuu akiwa katika ziara Mkoa wa Kagera tarehe 21/09/2021 specifically alitoa ahadi ya ambulance kwa Kata ya Nyakahura kwa ajili ya hicho kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa kujua ahadi hiyo ya Waziri Mkuu ninayoiongelea ndiyo inayoelekea Nyakahura pale? Kwa hiyo, swali la kwanza, kwa sababu ni ahadi ya Waziri Mkuu, ni lini tutapa ile ambulance sawa na Waziri Mkuu alivyokuwa ameahidi kwa ajili ya wananchi wa Nyakahura? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kata ya Kabindi ni center kubwa sana ambayo inahudumia Kata karibu tano ukielekea njia ya Mwanza ambazo nyingine zinapatikana zaidi ya kilometa 70 mpaka 80 kutoka Biharamulo Mjini na center ile ni kubwa, lakini upande ule hatuna kabisa ambulance ambayo inaweza ikakaa pale kwa ajili ya kuhudumia hizo Kata tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na hii ya Nyakahura, ni lini sasa tutapata ambulance nyingine itakayokuwa inakaa Kabindi kwa ajili ya kuhudumia kata tano inapotokea dharura aidha waletwe Biharamulo Mjini au wapelekwe Mwanza kwa ajili ya kwenda kupata matibabu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kupata pia majibu ya Serikali kuhusu issue hiyo ya ambulance nyingine ya pili. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ninakiri na kwenye kampeni nilifika katika Jimbo la Biharamulo Magharibi na anayoyazungumza Mheshimiwa Chiwelesa yako sahihi. Nimhakikishie ahadi za viongozi wetu wakuu wote nchini zinakwenda kutekelezwa kwa wakati, na tumeshaomba ambulance nyingine, zinakuja kutoka Wizara ya Afya. Zikifika tunakwenda kutekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la pili, tunalichukua kama Serikali ili kuangalia kulingana na idadi za ambulance tutakazokuwa tunazipata ili kuweza kuwaongezea. Ni kweli Jimbo hili kijiografia ni pana na lina idadi kubwa ya watu. (Makofi)
MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itapeleka gari la kubebea wagonjwa Kituo cha Afya Kilambo, Mtwara DC ukizingatia kituo hicho kipo mpakani mwa Msumbiji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu magari ya kubebea wagonjwa, tuna maeneo yenye upungufu kweli, tunakiri, na tumeendelea kuyaomba magari haya pamoja na yale mengine ambayo tayari Serikali imeshayatoa katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ombi lake tunalichukua kwa maana ya kwamba tunapoenda kuomba magari mengine na yeye awe mnufaika katika gari hili la ambulance. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumwuliza Mheshimiwa Waziri, Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina Majimbo matatu na ina hospitali mbili zenye hadhi ya Wilaya kikiwemo na kituo kikubwa cha afya kilichopo Nyarugusu kwenye Jimbo lake Mheshimiwa Waziri na magari tunayo mawili tu. Anapopatikana mgonjwa kutoka Nyarugusu inalazimika kutoa gari kilometa 100 kwenye Hospitali ya Wilaya Nzera au kilometa 80 kule Katoro. Je, ni lini Serikali itapeleka ambulance kwenye kituo kikubwa cha Nyarugusu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwape pole na kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Busanda, Majimbo yote matatu yaliyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita DC kwanza kwa uvumilivu mkubwa na usikivu mkubwa na wanatuunga mkono viongozi wao. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Kasheku Musukuma, tutafanya namna ya kupeleka gari la ambulance ili kuokoa maisha ya wagonjwa wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuendelee kusubiri, Serikali tumeshaomba magari haya kutoka Wizara ya Afya. Hivyo, Jimbo la Busanda na lenyewe ni wanufaika katika kupata ambulance mpya. (Makofi)
MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninapenda kuuliza swali. Ni lini Kituo cha Afya cha Kata ya Rwamgasa kitakamilishwa na kuanza kutoa huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifika katika Kituo cha Afya cha Rwamgasa na kiukweli kimeanza kutoa huduma za OPD na kuna majengo yanazidi kuongezwa pale kupitia mbia wetu wa Buckreef, na majengo haya yanakwenda kukamilika ndani ya mwezi wa tatu na kuanza kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshatoa maelekezo mahususi kwa Mkurugenzi kufuatilia kwa ukaribu katika ujenzi wa majengo haya ili akina mama wetu wanaojifungua zaidi ya 200 mpaka 250 kwa mwezi waweze kupata huduma hii ya afya ya msingi. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika swali langu la msingi, niliuliza suala zima la ujenzi wa kituo ndani ya Kata ya Buguruni, lakini kwa masikitiko makubwa naona Serikali imejikita kunijibu kuhusiana na ujenzi wa Kituo cha Afya ndani ya Kata ya Kisukuru. Pamoja na yote, ninalo swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Kata ya Buguruni ni kitovu cha uchumi ndani ya Jimbo la Segerea, na kwa sababu hiyo kuna mwingiliano wa watu wengi ukiachilia mbali na hao wakazi 47 plus, jambo linaloonyesha wingi wa wananchi au wanaodumu ndani ya ile kata kwamba ni wengi zaidi ya 47,000 ambayo Serikali imetaja, sasa kwa umuhimu, ningependa kufahamu kwa uhakika kabisa, Serikali imetenga kiasi cha shilingi ngapi kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya ndani ya Kata Buguruni, na ni lini hasa ujenzi huo utaanza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali nyongeza la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Segerea, kama ifuatavyo: Tayari Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetenga jumla ya shilingi bilioni nne, kwa maana ya; kwanza, kulipa fidia na kuongeza eneo; pia kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kisukuru kilichoko ndani ya Kata ya Buguruni.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua hatima yake, hapa sasa itafika wakati wananchi watawaogopa kwenye mambo haya. Vituo vya mkakati vya afya vinavyojengwa na Serikali, maana yake mlisema mtapeleka shilingi milioni 250 na baadaye shilingi milioni 250 nyingine zitafuata. Sasa kama Kituo cha Mkakati cha Mihingo kinajengwa kwa shilingi milioni 250 na Serikali, halafu tukapata majibu kwamba sasa halmashauri itenge fedha ya kujenga hayo majengo. Sasa hapa kuna mchanganyiko, tunataka tuelewe lipi? Serikali Kuu ndiyo itajenga hivyo vituo kwa maana iliahidi kutoa hiyo shilingi milioni 250 kwa milioni 250; au imeahirisha tena, Mkurugenzi ndio atoe fedha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Bunge lako Tukufu lilipitisha kujenga vituo vya kimkakati katika majimbo yote nchini. Tayari tumeshapeleka shilingi bilioni 30 kujenga vituo vya afya vya kimkakati katika majimbo 120 na tayari tumeshaomba fedha nyingine kwa ajili ya kujenga vituo vya afya hivi katika majimbo mengine 94 na yale mengine mapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tayari tumezielekeza halmashauri kuendelea kujenga majengo ya kutoa huduma katika hospitali hizi zote, lakini kama haitoshi, tutaendelea kuainisha halmashauri zile zenye uwezo na zile ambazo hazina uwezo ili tuweze kutoa fedha Serikali Kuu.
MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Butiama ina kata 18, lakini kati ya hizo, kata tisa tu ndiyo zenye vituo vya afya. Pia kuna kata kubwa kama vile Buruma, Buiregi, Bumangi, hazina vituo vya afya. Je, Serikali ina mpango gani kujenga kituo cha afya angalau kwenye kata ya Buruma yenye vijiji sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, Serikali inapongeza kwa maana ya kwamba tayari ana vituo tisa ndani ya kata 18, wakati huo kuna baadhi ya kata 14 ina vituo viwili. Kwa hiyo, ni juhudi kubwa ambayo imefanyika na tunaendelea kushirikia na Mheshimiwa Mbunge kuona ya kwamba tunazidi kuongeza vituo vya afya katika jimbo hilo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Mbali na mpango wa Serikali wa kujenga vituo vya afya na hospitali, mmekuwa na mpango wa ukarabati wa hospitali ambazo zimechakaa. Hospitali ya Manyamanyama iliyopo kwenye Jimbo la Bunda Mjini ni hospitali ambayo majengo yake ni chakavu sana na inatoa huduma katika wilaya za jirani. Ni lini sasa mtatukarabatia Hospitali ya Manyamanyama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika zile fedha ambazo Serikali ilitenga shilingi bilioni 102.08 za ukarabati wa hospitali hizi na hospitali hii aliyoiainisha Mheshimiwa Mbunge imo katika ukarabati huo. (Makofi)
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kituo cha Afya cha Nangara kimejengwa na nguvu za wananchi na ni jengo moja tu la OPD. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha nyingine ili kuweza kumalizia majengo mengine ili wananchi hao ambao wanafuata huduma umbali mrefu waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki cha afya, kwanza tunawashukuru sana wananchi kwa kutoa nguvu zao na kuweza kuunga mkono juhudi za Serikali, lakini pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nimeshaongea na Mkurugenzi, na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI niendelee kumwelekeza Mkurugenzi kutenga fedha za ndani ili kukamilisha baadhi ya majengo katika kituo hiki baada ya kutoa OPD waendelee kutoa na huduma nyingine ambazo zinatakiwa kwenye kituo cha afya. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mchinga halina hospitali hata moja, na lina vituo vya afya viwili. Kwa kuwa jimbo hili halina hospitali, je, ni lini Kituo cha Afya cha Kitomanga kitapandishwa hadhi ya kuwa hospitali, na kwa sababu mchakato wake wa kupandishwa hadhi ni wa muda mrefu, nilikuwa ninaomba majibu ya Serikal, lini kituo hiki kitapandishwa hadhi na kuwa hospitali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mama Salma kwa kufuatilia afya za wananchi wake katika Jimbo la Mchinga. Pili, tayari tumeshachukua maombi ya kupandisha Kituo cha Afya Kitomanga kuwa hospitali ili kiweze kutoa huduma katika eneo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshakaa na wataalamu, na nimhakikishie Mheshimiwa Mama Salma Kikwete kwamba ndani ya muda mfupi tathmini itatoka na kuanza ujenzi na kukipandisha kituo hiki kuwa hospitali. (Makofi)
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tunduru, hususan Jimbo la Tunduru Kusini ina vijiji vingi ambavyo bado pamoja na jitihada za Serikali za kufungua, lakini hivyo vijiji havijawahi kupata hizo barabara. Mimi nafananisha barabara kama uwepo wa mishipa ya damu kwenye mwili wa binadamu kwamba ili tu-speed up maendeleo tunatakiwa pale sehemu ambapo tunaweza tukatengeneza ukaribu wa vijiji kuwasiliana ikafanywa hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa mfano, kipo Kijiji cha Semen na Kijiji cha Chiwana au kuna Kijiji kinaitwa Nalasi na Kijiji cha Mnemasi. Ukitoka Semen kwenda Chiwana ipo shortcut ya kilometa tano tu, lakini hivi tunavyoongea leo, ili kukifikia kijiji hicho unahitaji kutembea kilometa 17. Sasa swali je, Serikali haioni umuhimu wa kuhakikisha kwamba vile vijiji ambavyo vinakaribiana kwa mtindo huo vinafanyiwa sasa? Hilo swali langu la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ipo barabara inatokea Chiungo inapita Mkambara inaenda mpaka Mkasale. Barabara hii ilifunguliwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, kinachoombwa sasa ni ile barabara kusajiliwa ili iweze kupata huduma ya TARURA na ukitoka hapa Mkambara kwenda Mkasale ni kilometa zisizozidi nne katikati pale pana mto ambao huwa unajaa, sasa wananchi wa Mkambara wanategemea Hospitali ya Mkasale.

Je, Serikali itakamilisha lini jambo la kuisajili ile barabara kwa sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Fadhili, engineer huyu. Kwa bahati nzuri nilifika katika Jimbo lake na tulifanya mkutano mkubwa sana pale jimboni na wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini pamoja na Tunduru Kaskazini ni waungwana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, maswali yake mawili ya nyongeza. Hili la kilometa tano nawaelekeza TARURA kuanzia sasa wafike eneo hili kufanya tathmini katika shortcut hii na kuweza kuitengea bajeti ya kuanza utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kusajiliwa; tuna utaratibu wa kusajili barabara hizi katika Wakala wetu wa TARURA na pia nawaelekeza Meneja wa TARURA wa Mkoa pamoja na yule wa Wilaya waweze kuisajili barabara hii iweze kutoa huduma kwa watu katika Jimbo la Tunduru Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Baracuda kupitia Chang’ombe kupitia Majichumvi kwenda kule Majumba Sita ni zaidi ya mwaka sasa imepata mkandarasi. Huyo mkandarasi alichofanya ni kwenda kuweka bango lake la ukandarasi pale, mpaka hivi sasa ninavyoongea hakuna chochote kinachoendelea kwenye hiyo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kufahamu siku ya leo, ni lini ujenzi wa hiyo barabara utaanza? Zingatia ni lini ujenzi huo utaanza? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnesta Kaiza, kama alivyoliuliza.

Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Agnesta Kaiza kwa kuwapambania wanajimbo la Segerea na amezitaja barabara kama alivyoziainisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii tayari inaye mkandarasi, anachosubiri ni advance payment ili aweze kuanza kufanyakazi. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, barabara hii itaweza kuanza kujengwa katika bajeti hii kadri tunavyoendelea kupata fedha na kumlipa mkandarasi aweze kuanza kufanya utekelezaji huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. HARAN N. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza napenda kuipongeza Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa mtandao wa barabara kilometa kama 45, lakini naomba niulize swali tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata wakandarasi sita ambao wanatekeleza utengenezaji wa zile barabara za DMDP, lakini toka nimefanya ziara ni miezi minne sasa hivi wameingia site, wengine wameweka vifaa, lakini hawapo site hadi sasa hivi tunavyoongea hapa na kila ukiwauliza wanazungumza wanasema labda fedha hazijatoka.

Sasa tunaomba kauli ya Serikali, ili wananchi wale waweze kupunguziwa adha ya zile barabara walizokuwa wamezitindua maana zinakwamisha upitaji. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Sanga, Mbunge wa Kigamboni na bahati nzuri alipata ziara ya Waziri wetu, alifika kule na akajionea barabara hizi. Pia namhakikishia Mheshimiwa Sanga, mimi na yeye baada ya hapa tuwasiliane ili tuone fedha hizi ambazo Serikali imeshazielekeza kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizi kilometa 45. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa mvua inayoendelea ina mchango mkubwa katika uharibifu wa miundombinu ya barabara Kata ya Mapinga, Nianjema na Kisutu, Jimbo la Bagamoyo. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri upo tayari ukipata fursa ya kutembelea maeneo hayo ili kuona zile fedha za TARURA na kuelekeza maeneo korofi ikiwemo mifereji ili maji yaweze kwenda baharini na kuwaacha wananchi katika maeneo ya nchi kavu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza kwa ujumla, ni kwamba tumepata changamoto ya mvua hizi katika maeneo mengi nchini likiwemo Jimbo langu mwenyewe la Busanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata changamoto ya mvua katika maeneo yote na yale ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha. Mimi niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge katika maeneo haya kwenda kufanya tathmini, lakini pia kuwaelekeza TARURA kujenga miundombinu ambayo itakua ni himilivu katika kipindi hiki kwa kadri tunavyopata vipindi vya mvua ili miundombinu iweze kuwa himilivu.
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa kwamba kumekuwa na changamoto kubwa katika urejeshaji wa mikopo na tunafahamu Serikali yetu imekuwa ikitenga fedha kwa kila halmashauri kila mwaka, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri, changamoto za urejeshaji zimekua ni kubwa sana.

Je, ni lini Serikali itaamua kuweka elimu ya fedha kwa wanufaika hawa ili waweze kuelewa biashara wanazoenda kuzifanya, ili tuweze kukusanya mapato yetu kwa ukamilifu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Devotha Daniel kwa kuuliza swali la nyongeza ambalo anawapambania wananchi, hasa wa Mkoa wa Kagera, lakini ni kwa nchi nzima ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, tumekwishaelekeza watalamu wetu, Maafisa Maendeleo waweze kutoa elimu ya mikopo. Sambamba na hilo Kamati ya TAMISEMI ilitoa maelekezo mahsusi na sisi kama Wizara tumeyachukua na tumewaelekeza wataalam wetu kule halmashauri waweze kutoa elimu ya mikopo hii na pia waweze kutoa elimu ya namna ya kusaidia vikundi hivi kuweza kufanya marejesho, lakini pia waweze kupata zile kazi za 30% za PPRA ili kuweza kusaidia vikundi hivi katika mikopo viweze ku-qualify na vile vingine ambavyo ni vipya vianze kukopeshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la mikopo hii liko wazi katika miongozo kwa maana ya kwamba ni kuwasaidia mitaji. Kwa hiyo, tunawaomba sana Watanzania wanaopata mikopo hii ya vikundi waweze kufanya marejesho kwa wakati ili tuweze kuwakopesha na wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. FARAJI B. NANDALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri.

Swali langu, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ndanda, nataka kufahamu ni lini Serikali itaona ipo haja ya kupunguza siku za maombi ya mikopo hii kutoka siku 90 zilizopo sasa hivi mpaka siku saba au 14, ili tuweze kuwafikia Watanzania wengi kwa muda mfupi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama alivyoliuliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi siku 90 zipo kwa utaratibu, kwa maana ya kwamba wapewe elimu ambayo Mheshimiwa Mbunge ametoka kuuliza ni kipindi cha kupewa elimu, lakini kufanya ufuatiliaji wa kuona kwamba vikundi ambavyo vimeomba ni kweli vina haki ya kupewa mikopo ile na vina uwezo wa kurejesha. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tunauchukua ushauri wake na tutaufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naanza kwa kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayoifanya na hususan kuhakikisha kwamba suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi linatekelezwa ipasavyo. Naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa malengo haya ambayo yanakwenda kumuongezea kipato mwananchi kuanzia ngazi ya kaya mpaka Taifa na hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuiuliza Serikali swali hili, katika malengo haya mazuri ya Serikali ya kuwakopesha wajasiriamali hususan wanawake na hasa wanawake wa Mkoa wa Tabora.

Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba mikopo hii wanayopewa wanawake wajasiriamali, wanazalisha bidhaa zenye kukidhi haja na soko lililopo sasa hivi nchini na nje ya nchi ili sasa bidhaa zao zile wanazozalisha ziweze kuwa na tija na kukidhi soko la ndani na soko la nje ili waweze kuinua kipato chao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, ufuatiliaji wa mikopo hii, je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba mikopo inayotolewa inafuatiliwa na kweli inakwenda kuzalisha kwa tija?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji majibu ili sasa wanawake hawa waweze kuzalisha kwa tija na hususan wanawake wa Mkoa wa Tabora ili kipato chao kiweze kukua kuanzia ngazi ya familia na Taifa. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwapigania wananchi hasa akinamama wa Mkoa wa Tabora, anataka tuhakikishe tunapeleka tabasamu. Ninapokea pongezi ambazo amezitoa na hiyo ndiyo nia ya dhati ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha anatukomboa kiuchumi wapambanaji wetu akinamama wa Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwishatoa maelekezo kwamba maafisa maendeleo wetu hawana kazi tu ya kukusanya fedha na kuzipeleka kwenda kwenye mikopo, wanayo kazi ya kutoa elimu ya tija ya kutosha na kufuatilia marejesho ili tuweze kuwakopesha na wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Kwa kuwa Serikali imeshatoa kanuni, imetoa maelekezo, lakini bado kuna wananchi ambao wako vijijini hawajapata elimu ya mikopo, nini mkakati wa Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Mnzava kama ambavyo ameliuliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali ni kuendelea kutoa elimu na kufanyia marekebisho mapungufu ambayo yanaendelea kujitokeza. Nimesema awali ya kwamba, Kamati ilitoa ushauri wa kutosha kabisa, Kamati ya TAMISEMI nasi kama Wizara tunakwenda kufanyia kazi ili kuendelea kurekebisha yale maeneo yenye upungufu ili elimu iwafikie wakopaji na waweze kukopesheka, waweze kujiinua kiuchumi na waweze kufanya marejesho kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekti, ahsante, kwanza ninaishukuru sana Serikali kwa majibu yake mazuri na ninapongeza watoa huduma kwa maana ya watumishi wa afya Wilaya ya Hai kwa kazi nzuri wanayoifanya wakiongozwa na Mkurugenzi wetu na DMO.
Swali la kwanza; Serikali ilituahidi kujenga Chuo cha Afya Narumu pamoja na kituo cha afya, tukahamasisha wananchi wakaanza ujenzi wa msingi na mimi kama Mbunge nikashiriki, je, ni lini sasa Serikali itatimiza ahadi yake hii?

Swali la pili, Wilaya ya Hai inavyo vituo, zahanati chakavu nne, zahanati chakavu kwa maana ya Uswaa, Mtakuja, Weruweru na Uroki. Serikali ina mpango gani mahsusi wa kukarabati zahanati hizi chakavu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Jimbo la Hai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwapambania wananchi wa Jimbo la Hai na hakika ziara ya Waziri Mkuu tuliifuatilia wote na Waziri Mkuu alisema kweli Hai imepata Mbunge wa uhakika, smart boy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kwanza tunawashukuru wananchi wa Jimbo la Hai kwa nguvu zao ambazo walitumia kupata eneo hilo na kuanza ujenzi, pia ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kutenga Mfuko wa Jimbo kuona tunasukuma mbele gurudumu la maendeleo ya afya katika Jimbo la Hai. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu zahanati, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tumekwishatenga bajeti ya kuanza kuboresha zahanati zile chakavu hasa zile za zamani. Kwa hiyo, katika Jimbo la Hai na lenyewe tutalipa kipaumbele kutenga bajeti hizi za kuboresha miundombinu ya zahanati zile za zamani. Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Jimbo la Hai, tunawahakikishia kwamba Serikali itaendelea kupeleka fedha kadri tunavyozipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, awali ya yote kwanza ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia afya njema na kuwa sehemu ya Wabunge katika Bunge lako hili, haikuwa rahisi lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu hakuna kinachoshindikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa kata zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ni pamoja na Kata ya Kidodoma. Kata ile ina vijiji vitano lakini mpaka hivi tunavyozungumza ile kata haina kituo cha afya na mpango wa Serikali ni kuhakikisha tunakuwa na vituo vya afya katika kila kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatamani kujua, ni nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha tunapata kituo cha afya katika Kata ile ya Kidodoma? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sikudhani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kuhakikisha tunajenga vituo vya afya kila kata. Bunge lako Tukufu liliridhia kuanza na vituo vya afya vya kimkakati, ambapo tayari tumekwishajenga vituo vya afya 120 na tayari tumekwishaomba fedha kwa ajili ya kujenga vituo vingine vya afya vya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mbunge kwamba katika eneo hili la kituo cha afya, kwanza wanazo zahanati ambazo zinaendelea kutoa huduma, lakini na wenyewe tutaweka katika kipaumbele ili tuweze kuwajengea kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, Kituo cha Afya Kwekanga ni kituo cha kimkakati lakini ujenzi wake umechukua muda mrefu sana. Tunaomba majibu ya Serikali, ni lini Serikali itapeleka fedha kwenye Kituo cha Afya Kwekanga katika Wilaya ya Lushoto kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo katika kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sekiboko, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vituo vya afya ambavyo tayari vilishatengewa fedha na vikapelekewa zile shilingi milioni 250, Serikali inatambua siyo kwamba zile shilingi milioni 250 tayari zinatosheleza, tumekwishawaelekeza Wakurugenzi, hasa kwenye zile halmashauri zenye mapato makubwa ili waweze kuendelea kuboresha miundombinu ambayo itaendelea kutoa huduma kwa watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tunaendelea kulichukua jukumu hili ili kuona vituo vyote ambavyo tumevianzisha vinakamilika na vinatoa huduma kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kuniona na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Mpendo, Jimbo la Chemba ni kata iliyoko pembezoni lakini kata hii ina zahanati moja tu ambayo inatoa huduma kwa vijiji vinne. Nini mkakati wa Serikali wa kuwajengea kituo cha afya wananchi wa Kata ya Mpendo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mheshimiwa Kunti kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mkakati wa Serikali ni kuhakikisha tunajenga vituo hivi vya afya na katika jimbo hili tutawapa kipaumbele ili kuona namna gani tunaanza ujenzi wa kituo hiki katika kipindi hiki cha fedha. Katika miaka hii kuanzia Bunge hili la mwaka 2026 mpaka mwaka 2027 tutaona namna ya kuboresha na kujenga kituo hicho cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. JUMA R. MUSTAFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza kwenye Wizara ya TAMISEMI. Kwanza kabisa ninapenda kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ambazo inaendelea kufanya.

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya umaliziaji wa maboma ya vituo vya afya vilivyomo ndani ya Jimbo la Igalula? Vituo hivyo vilivyopo ndani ya Jimbo la Igalula ni Kata ya Tura, Goweko, Kizengi, Lutende na Loya, kwani ndani ya Jimbo la Igalula hatuna hata kituo kimoja cha afya kilichokamilika majengo. Tunaiomba Serikali itusaidie kutupelekea fedha.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kawamba, Mheshimiwa Mbunge wa Igalula na ninampongeza sana ndugu yangu kwa kufuatilia hali na mahitaji ya wananchi wa Jimbo la Igalula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie na hata Bunge lililopita nilimhakikishia kwamba tutakwenda kuhakikisha tunaboresha maeneo haya ya vituo vya afya, tunamalizia maboma ambayo bado yameonekana ni changamoto ili kuweza kutoa huduma katika Jimbo la Igalula na Wana-Igalula waweze kupata tabasamu la Mheshimiwa Dkt. Samia Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. YOHANA S. MSITA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nami kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Itigi ninapenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri.

Kwa kuwa Jimbo la Itigi lina kata 13 na tunavyo vituo vinne tu vya afya na hili jimbo lipo scattered sana. Je, nini mpango wa Serikali kujenga vituo vya afya angalau kwenye kata tatu za Ipande, Mgandu pamoja na Mwamagembe ili kupunguza adha ya wananchi wangu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yohana, Mbunge wa Jimbo la Itigi kama ambavyo ameliuliza. Jimbo la Itigi ni miongoni mwa majimbo ambayo tumekwishayaombea fedha Hazina ili tuweze kujenga vile vituo vya afya vya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge nitampa ushirikiano wa dhati ili kuweza kuhakikisha angalu kwenye kata hizi tatu alizoziainisha ziweze kupata kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninapenda kumshukuru Naibu Waziri TAMISEMI kwa majibu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali hii ya Halmashauri ya Shinyanga imeanza kujengwa mwaka 2008 mimi nikiwa mtumishi wa Halmashauri kama Medical Officer in Charge na msimamizi wa ujenzi ule. Awamu ya mwaka 2018/2019 imekuta ile hospitali tayari imeshaanza kujengwa, lakini haijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni upi mpango mkakati wa Serikali kutoa kipaumbele kwa Halmashauri ya Shinyanga, hizi shilingi milioni 200 zilizotengwa? Tunahitaji shilingi milioni 500 tu kukamilisha ujenzi ule. Je, ni nini mpango mkakati wa Serikali kuipa kipaumbele Halmashauri ya Shinyanga? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Ujenzi wa majengo ya kutolea huduma umekwenda sambamba na ujenzi wa nyumba za watumishi. Pale kuna nyumba tatu tu, kuna madaktari 17 ambao tunahitaji wakae eneo la hospitali. Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi, shilingi milioni 200 hizi zinaelekezwa kwenda kukamilisha yale majengo saba yaliyosalia, lakini tutafanya tathmini kuona uhitaji na kuweza kuwaongezea bajeti kadiri tunavyopokea fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu nyumba za watumishi, nilishajibu katika Bunge lako Tukufu. Tayari tumefanya tathmini na uhitaji zaidi ya nyumba 2,000 na tunahitaji zaidi shilingi bilioni 241 ambazo tayari TAMISEMI imeshaanza kushirikiana kuzitafuta fedha hizi ili kuona namna tunavyoweza kukamilisha nyumba hizi ambazo tutazielekeza pia katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi kubwa iliyofanyika ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Karatu na huduma zinazoendelea kutolewa, bado kuna upungufu wa ukosefu wa jiko kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa. Wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Wilayani Karatu, tuliahidiwa kwamba fedha zitaletwa. Je, ni lini fedha hizo zitaletwa ili utekelezaji na ujenzi wa jiko uweze kufanyika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Karatu ni miongoni mwa hospitali ambazo zimo katika bajeti ya mwaka 2026/2027 ambapo tumetenga jumla ya shilingi bilioni 56.25 kwa ajili ya ukamilishaji wa hospitali 105.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Paresso, tutapanga bajeti kulingana na ukamilishaji wa miundombinu ambayo inapelea katika Hospitali yetu ya Karatu.
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kituo cha Afya Mtina kinachohudumia kata mbili, hakina jengo la mama na mtoto, hali inayosababisha staha ya wakina mama kuondoka hasa wakati wanapojifungua. Tulishaanzisha ujenzi pale na jengo halijakamilika, nini mpango wa Serikali kukamilisha jengo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Eng. Fadhili, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini kwa kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa vituo hivi vya afya ambavyo tayari tulishaanza kujenga na tunatoa huduma zile za OPD, lakini tunajua miundombinu ambayo bado inatakiwa kukamilishwa, tunaendelea kutenga bajeti kukamilisha miundombinu hiyo.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa hospitali ya Wilaya ya Halmashauri ya Shinyanga inahudumia majimbo mawili yenye kata 26 na hivyo kuwafanya wananchi wa Jimbo la Itwangi kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kupata huduma ya Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kukipandisha hadhi Kituo cha Afya cha Tinde ili kiwe na hadhi ya kiwilaya kutokana na mazingira yaliyopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI, MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Azza, Mbunge wa Jimbo la Itwangi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza kwa kuendelea kufuatilia hali ya Kituo cha Afya cha Tinde. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ina mpango wa kuendelea kujenga yale majengo ambayo yanatakiwa pale kwa awamu ili kukamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilisha majengo yale katika kituo cha afya cha Tinde, tutawa-consult wenzetu wa Wizara ya Afya ili waweze kukipandisha kwenda Hospitali hadhi ya Wilaya kulingana na uhitaji na vigezo ambavyo vitatimizwa katika kupewa kibali cha kupandisha kuwa Hospital ya Wilaya. (Makofi)
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Wilaya ya Muleba ni kati ya Wilaya kongwe, na zenye watu wengi. Ninaishukuru Serikali kwa kutupatia ujenzi wa hospitali ya wilaya, lakini umekuwa ukidorora. Je, ni lini Serikali itamalizia na kutupatia pesa ya kutosha ili tukamilishe Hospitali ya Wilaya ya Muleba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu awali kwenye maswali madogo ya nyongeza, Serikali imefanya tathmini na tayari tumeshatenga bajeti kwa mwaka huu wa fedha 2026/2027 zaidi ya shilingi bilioni 56.25.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetenga bilioni hizi ili kukamilisha ujenzi wa hospitali za wilaya 105. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hiyo hospitali itakuwemo kwenye mpango huu na tutaweza kuikamilisha.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Nami niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaishukuru TAMISEMI. Nilizungumza hapa kuwa kuna fedha zilirudi shilingi milioni 800, sasa mmezirudisha katika ujenzi wa hospitali yetu ya Halmashauri ya Mji wa Bunda, tunashukuru. Hata hivyo, hospitali bado haijakamilika, kuna majengo yanahitajika; kichomea taka, wodi ya watoto, bohari ya dawa na jengo la utawala. Vyote hivi vinagharimu takribani shilingi milioni 700.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itatuletea fedha hiyo ili tukamilishe hospitali hiyo ya Halmashauri ya Mji, na wananchi waweze kupata huduma ya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge anakiri kwamba Serikali ilipeleka fedha zile ambazo zilikuwa zimerudishwa ili kwenda kukamilisha baadhi ya miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutaendelea kushirikiana kuhakikisha tunakamilisha na tunatenga bajeti kwa awamu kuendelea kukamilisha vichomea taka na yale majengo aliyoyataja ili kuweza kutoa huduma zinazotakiwa katika hospitali yetu hii.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tunaishukuru Serikali kwamba tunayo Hospitali ya Wilaya ya Sikonge, lakini haina uzio na kumekuwa na changamoto nyingi sana zinazosababishwa na kukosekana kwa uzio. Je, ni lini Serikali itatujengea uzio katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Sikonge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kusisitiza halmashauri, kwanza kufanya tathmini na kutenga fedha za kujenga uzio. Pia tutawasilisha maombi haya TAMISEMI, na kujiridhisha, kisha kuanza ujenzi wa uzio katika hospitali zote za halmashauri.
MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Katika Hospitali ya Wilaya ya Katoro, tuna changamoto ya jenereta, limeharibika kwa muda mrefu, na huduma zimesimama. Lini sasa Serikali itapata jenereta ili kutimiza mahitaji ya wananchi katika Hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali hii ya wilaya inaendelea kutoa huduma kwa kutumia umeme wetu, lakini sasa huwa tuna yale majereta ya dharura ambapo sasa nimwelekeze Mkurugenzi afike eneo la tukio na aone kwanza namna gani ya kuweza kulirudisha jenereta lililokuwa linafanya kazi pale ili liendelee kuwa la dharura na kutoa huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)
MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kuchukua nafasi hii kwanza kuishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo saba, ambayo yanaendelea kujengwa kwa sasa. Uhakika ni kwamba, majengo ambayo yamekamilika ni manne. Sasa majengo tisa ambayo bado yanahitajika, kwa mfano jengo la huduma ya macho, jengo la kuhifadhia maiti, majengo ya huduma ya kinywa na meno, pamoja na karakana ya hospitali na jiko, haya ni majengo muhimu sana ambayo yanahitajika.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mkakati gani kuongeza kasi kuhakikisha kwamba majengo haya yanakamilika ili wananchi wa Butiama waweze kupata huduma nzuri ya afya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri ikiwezekana mwezi wa Saba tuambatane naye aende kuangalia hali halisi ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Butiama, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, tunaendelea kusisitiza ukamilishaji wa majengo haya na tunawaelekeza wataalamu wetu kuwa waadilifu katika kazi hii. Tayari Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, imetuma baadhi ya timu yetu kwenda kuangalia ujenzi wa mejengo haya ili yakamilike kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, nikijibu swali lake la pili, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, tuko tayari muda wowote kufanya ziara. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge lako hili Tukufu la Bajeti tutaongozana naye kwenda Butiama kujionea miundombinu hii, ili iweze kutoa huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)
MHE. DOTTO J. BAHEMU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Sisi Hospitali yetu ya Wilaya ya Ngara, na ya Mbuba, pia kuna ujenzi ambao unaendelea, lakini jengo la mochwari, jengo la wodi za wagonjwa pamoja na theatre vilevile bado hayajakamilika. Je, ni mpango gani wa Serikali kuhakikisha kwamba haya majengo yanakamilika ili wananchi waendelee kupata huduma bora sana. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, sote tutakumbuka kwamba Serikali katika bajeti ya mwaka 2026/2027 tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 52.25 kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo, miundombinu katika hospitali zetu za Halmashauri 105. Nimhakikishie Mheshimiwa Bahemu, yupo ndani ya mpango, tutakwenda wote pamoja kuhakikisha kwamba hospitali hii tunakwenda kuikamilisha katika miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninaomba niishukuru Serikali kwa kupeleka fedha awamu ya kwanza kujenga Kituo cha Afya cha Tarafa ya Nyakakika. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha awamu ya pili ili kukamilisha kituo cha afya? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, tayari tulishapeleka fedha awamu ya kwanza, na tayari tumeshaomba fedha Hazina awamu ya pili ili kuhakikisha tunakamilisha kwa wakati vile vituo vyote ambavyo tulivianzisha ambavyo tulivitengea shilingi milioni 250. Nimhakikishie Mheshimiwa Bashungwa, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, tutaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha kituo hiki kinakamilika kwa wakati.
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Ninaomba kumwuliza Naibu Waziri atusaidie, Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kukarabati kituo kikongwe cha afya cha Umbwe ambacho kipo Kibosho Magharibi, kituo ambacho kinawanahudumia Tarafa yote ya Kibosho yenye Kata sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, tayari tuna mpango mkakati pale Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha vituo vya afya kongwe, na hospitali zile kongwe tumezitengea bajeti kwa ajili ya kwenda kuzikamilisha, ikiwa ni pamoja na kurekebisha miundombinu chakavu ili ziendelee kutoa huduma kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tutaendelea kutenga bajeti ili kukamilisha vituo kongwe kama ambacho amekiongelea.
MHE. CHARLES M. NJAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa namna ambavyo wameendelea kutoa jicho lao kwa ajili ya ukarabati wa majengo yale, lakini kwa kuwa hali ya majengo yale ni chakavu mno na hayaridhishi kabisa, tunaomba aweze kupanga safari yeye pamoja na wataalam wake ili twende tukaone hali halisi kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, ninaamini baada ya kuiona tunaweza tukawa na mpango wa pamoja ambao utatufanya tuharakishe zaidi kufanya matengenezo, kwa kuwa kiasi cha milioni 600,000,000 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bado ni kidogo mno ukilinganisha na hali ya uhitaji uliokuwepo katika majengo yale.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je ni lini ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Kwamndolwa utaanza, kwa kuwa imekuwa ahadi ya muda mrefu kwa wananchi wa Kwamndolwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, pongezi ambazo amezitoa Mheshimiwa Mbunge zinaelekea moja kwa moja kwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu yeye alifanya ziara na aliahidi fedha hizi ziende kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ambayo imetajwa.

Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge lako Tukufu, tutapanga ratiba ili twende ziara katika hospitali yetu hii kujionea uchakavu wa miundobinu na pia thamani ya fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya kukamilisha miundobinu hiyo.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba katika swali lake la pili la nyongeza kuhusu kituo cha afya, tukiwa katika ziara hii tutapita kwenye kituo cha afya alichokitaja ili tuone namna gani ya kuendelea kutenga fedha ili kukamilisha miundobinu ya ujenzi wa kituo hicho.
MHE. HAIDERALI H. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Ninataka kujua, ni lini Hospitali ya Manispaa ya Mpanda itapata jengo la emergency?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu kwenye majibu ya awali, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Hospitali ya Mpanda nayo imo katika mpango wa zile hospitali 105 ambazo tumeshatenga bajeti katika mwaka wa fedha 2026/2027, jumla ya shilingi bilioni 52.25, ambazo tutazielekeza katika kukamilisha baadhi ya miundombinu muhimu.

Mheshimiwa Spika, ni kweli jengo la emergency ni muhimu sana kwa sababu linatoa huduma kwa wakati na baadhi ya wagonjwa huishia tu kutibiwa emergency na kwenda nyumbani. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa jengo hili muhimu.
MHE. DKT. GEORGE V. LUGOMELA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa tuna Kata ya Ipililo, kimejengwa kituo cha afya katika Kata ile na Kata ya Ipililo ndiyo Kata yenye wakazi wengi katika Jimbo la Maswa Mashariki. Ninaomba kuuliza, je, kituo cha afya hiki kitaanza kufanya kazi lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge aliuliza swali la nyongeza kuhusu kituo cha afya Kata ya Maswa. Kwanza tumejielekeza kutoa katika vile vituo ambavyo havijakamilika kwanza viweze kutoa huduma zile za OPD. Kwa hiyo, mimi na Mheshimiwa Mbunge tutakaa chini baada ya Bunge hili leo, ili tuone namna gani katika kituo chetu hiki cha afya kitaanza kutoa huduma za msingi kwa ajili ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii ili na mimi niulize swali. Kituo cha Afya cha Katoro kinapokea wagonjwa wengi sana kuliko Hospitali ya Wilaya ya Katoro. Je, ni lini Kituo cha Afya cha Katoro kitapata jengo la emergence ili kuongeza ufanisi kuhudumia wananchi wa Katoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, ni kweli pale Katoro kuna ongezeko kubwa sana la watu ndiyo maana wananchi wetu wanaona bora waende kwanza wakapate huduma katika kituo cha afya, lakini tayari Katoro wanayo hospitali ya wilaya inayotoa huduma za msingi, na wana jengo bora kabisa la emergency.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunawaomba wananchi waendelee kwenda kupata huduma hizo katika jengo la dharura la hospitali yetu ya Wilaya huku tukiendelea kujielekeza kuboresha miundobinu rafiki na miundobinu ya dharura katika kituo chetu cha Afya cha Katoro.