Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Jafar Rajab Seif (22 total)
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: -
Je, Serikali inachukua hatua zipi kwa Halmashauri ambazo hazitengi fedha za kununua mafuta ya Watu Wenye Ualbino?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji wa mafuta kwa watu wenye ualbino kupitia halmashari zote nchini. Katika mwaka 2024/2025 Serikali ilitenga shilingi bilioni 8.74, kwa ajili ya huduma za ustawi wa jamii na shilingi bilioni 1.4 zilitengwa kwa ajili ya ununuzi wa mafuta maalum ya ngozi kwa watu wenye ualbino.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuzielekeza halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya watu wenye ualbino. Katika mwaka 2025/2026 jumla ya shilingi bilioni 1.9 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya watu wenye ualbino kwa kuzingatia sera, sheria na miongozo ya utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Zahanati Kata ya Nsalala Wilayani Shinyanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, TAMISEMI kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetoa shilingi milioni 44.45 kwa ajili ya ukamilishaji wa boma la zahanati katika Kata ya Nsalala. Aidha, Serikali katika mwaka wa fedha 2025/2026 imetenga shilingi milioni 22, kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kwa ajili ya ukamilishaji. Ujenzi wa zahanati ya Nsalala utakamilika na kuanza kutoa huduma kabla ya mwezi Juni, 2026.
MHE. HIJA HASSAN HIJA aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka vifaa tiba vya kutosha, hususan vifaa vya kujifungulia, katika hospitali zote nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri ninayeshughulikia masuala ya afya, TAMISEMI. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Hija Hassan Hija, Mbunge wa Kiwani.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitenga fedha, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ya msingi vinavyoendelea kujengwa kote nchini. Aidha, katika kipindi cha miaka mitano, 2021/2022 hadi 2024/2025, Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 285.6, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vikiwemo vifaa vya kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 shilingi bilioni 32 imetolewa, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, ngazi ya msingi. Shilingi bilioni 9.6 imetolewa, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali za halmashauri kote nchini.
MHE. JUMA R. MUSTAFA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga maeneo ya malisho katika Jimbo la Igalula ili kupunguza migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Mustafa Kawamba, Mbunge wa Jimbo la Igalula, Halmashauri ya Uyui, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI:-
Mheshimiwa Spika, eneo la Igalula limekuwa na migogoro midogo ya wakulima na wafugaji, hususan katika maeneo ya kulishia mifugo. Aidha, migogoro hii imekuwa ikitatuliwa kupitia maridhiano ya mtu na mtu na hata kuwahusisha viongozi wa Serikali, kwa ajili ya kusimamia taratibu za fidia kwa hasara inayojitokeza. Aidha, Serikali imetenga jumla ya hekta 6,226.92 katika vijiji 16 vilivyopo Igalula.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha, kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Matumizi Bora ya Ardhi, ikiwa ni pamoja na kuainisha na kutenga maeneo maalum ya wakulima na wafugaji, kwa ajili ya ustawi wa wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui. Pia, Serikali inatoa wito kwa viongozi ngazi ya mkoa na halmashauri kote nchini kuhakikisha wanatatua migogoro ya wakulima na wafugaji kwa wakati na kuweka utaratibu mzuri wa matumizi bora ya ardhi.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza:-
Je, lini Serikali itakarabati Kituo cha Afya Masama pamoja na nyumba za watumishi wa Kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Saashisha kutoka Jimbo la Hai.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Masama kilijengwa Mwaka 1979, hali inayosababisha kuwa na miundombinu michache na chakavu. Kituo hicho kinahitaji miundombinu muhimu, ikiwa ni pamoja na jengo la huduma za wagonjwa wa nje (OPD), maabara, jengo la huduma za uzazi, jengo la upasuaji, jengo la kufulia, kichomea taka, vyoo vya nje na nyumba za watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya tathmini na kuainisha vituo vya afya kongwe 532 kote nchini, ambavyo vinahitaji kuongezewa na kukarabatiwa miundombinu yake. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 102.08 zinahitajika, kwa ajili ya uboreshaji wa vituo hivyo. Serikali itaendelea kutenga fedha, kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya afya kongwe kote nchini, kikiwemo Kituo cha Afya Masama. (Makofi)
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuipandisha hadhi Hospitali ya Manispaa ya Kahama kuwa Hospitali ya Rufaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kufanya maboresho katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, ikiwa ni pamoja na kuwezesha utolewaji wa huduma za kibingwa. Huduma za kibingwa zinazotolewa ni pamoja na huduma za magonjwa ya ndani (internal medicine), matibabu ya mifupa, magonjwa ya uzazi, magonjwa ya macho, pamoja na huduma za uchunguzi wa mionzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Kahama Manispaa ina upungufu wa miundombinu muhimu ikiwemo jengo la huduma za dharura, jengo la huduma za wagonjwa mahututi na baadhi ya vifaa vya huduma za uchunguzi. Serikali itaendelea kutenga fedha, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu muhimu katika hospitali hiyo kisha kufuata Miongozo ya Wizara ya Afya kupandisha hadhi kuwa hospitali ya hadhi ya mkoa.
MHE. PASCHAL I. CHINYELE aliuliza:-
Je, kwa nini wananchi wa Kata ya Mbalawala wamezuiwa kuendeleza ardhi wanayomiliki kwa maelezo kuwa ni sehemu ya Bonde la Kati Singida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Paschal Inyasi Chinyele, Mbunge wa Dodoma Mjini. Bonde la Mzakwe linasimamiwa na Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu Water Basin na Mamlaka ya DUWASA na siyo Bonde la Kati la Singida kama swali lilivyoelekezwa. Bonde hili lilipimwa kisheria na kusajiliwa Aprili, 2000 kwa ramani yenye Namba 45977.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hilo lina ukubwa wa hekta zaidi ya 34,000 na lipo katika Kata za Chihikwi, Kawawa, Matangizi, Makulu na Mtaa wa Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu zilizopelekea kuzuiwa kufanya maendelezo katika bonde hilo ni kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kuwa kuna zaidi ya visima 20 vinavyotoa huduma ya maji yanayotumika na wananchi wa Dodoma Mjini na maeneo jirani, eneo ilo kitaalam lina kimo cha maji kilichopo juu. Serikali imechukua hatua za kusitisha upimaji na umilikishaji pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya athari ya kuendeleza eneo hilo.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME aliuliza:-
Je, lini Serikali itadhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo ya Mvuha, Selembala, Dutumi, Kisaki, Bwakila Juu, na Kolelo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Yahya Mfaume, Mbunge wa Morogoro Kusini:-
Mheshimiwa Spika, kipindi cha kiangazi hutokea adha ya upungufu wa malisho maeneo mengi, ambapo hupelekea wafugaji kuanza kuhama kwa ajili ya kutafuta maji na malisho. Hali hii inasababisha wimbi la wafugaji vamizi kutoka nje ya Wilaya ya Morogoro kuleta mifugo mingi ambayo husababisha mwingiliano na uharibifu wa mazao.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na migogoro, ikiwa ni pamoja na kutenga na kutambua maeneo ya malisho kwa wafugaji kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi, ambapo jumla ya vijiji 68 vimefanyiwa mpango wa matumizi ya ardhi kwa kutenga hekta 54,577. Watendaji wote wa vijiji na kata kutoruhusu wafugaji wageni kuingia kwenye maeneo yao bila kufuata taratibu, kuhamasisha uzalishaji wa malisho ili kuongeza upatikanaji wa malisho kwa wafugaji.
Mheshimiwa Spika, wizara za kisekta zimeendelea kuimarisha huduma za ugani kwa kutoa elimu ya ufugaji wenye tija wa kuwa na mifugo michache.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine ya ulinzi na usalama kufanya operesheni maalum ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya mashamba ya wakulima katika Wilaya ya Morogoro. Pia, Serikali inapopata tetesi ya mgogoro kwa wafugaji na wakulima, Viongozi ngazi ya Mkoa na Wilaya hufika kwa wakati na kuhakikisha migogoro inatatuliwa.
MHE. KANGI A. LUGOLA aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha maboma 49 ya madarasa ya shule za msingi na maboma matatu ya zahanati za vijiji vitatu vya Jimbo la Mwibara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Kangi Alphaxard Lugola, Mbunge wa Jimbo la Mwibara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 hadi kufikia 2025/2026, Serikali imetoa jumla ya shilingi milioni 379 kukamilisha maboma 33 ya madarasa na shilingi milioni 250 kukamilisha maboma matano ya zahanati za Nambaza, Muranda, Mwiseni, Neruma na Sozia katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imetoa jumla ya shilingi milioni 241 kwa ajili ya ukamilishaji na uimarishaji wa huduma za mama na mtoto katika Zahanati ya Kabainja na shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma manne ya madarasa. Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa awamu kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya madarasa na zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza: -
Je, upi mpango wa Serikali katika kuhakikisha hospitali zote za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati zinakuwa na uzio?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uzio ni hitaji muhimu kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya nchini kwa ajili ya usalama wa watoa huduma wetu, wagonjwa, jamii inayozunguka vituo vya kutolea huduma za afya, mali pamoja na kuzuia uvamizi wa ardhi ya kituo. Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tayari imetoa maelekezo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha maeneo yote ya taasisi za umma, hususan vituo vya huduma za afya na shule yanapimwa na kutengenezewa hatimiliki.
Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu wa uzio kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, kwa sasa Serikali imejielekeza katika kukamilisha miundombinu muhimu ya kutolea huduma za afya, ikiwemo jengo pacha la huduma za uzazi/upasuaji, jengo la kufulia, wodi na jengo la kuhifadhia maiti. Aidha, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri itaendelea kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya ujenzi wa uzio kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. CORNEL L. MAGEMBE aliuliza: -
Je, lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya Nyamirembe ambapo ni Makao Makuu ya Tarafa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Cornel Lucas Magembe, Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 hadi mwaka 2025/2026 Serikali imejenga na kuboresha jumla ya vituo vya afya vitano katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato kwa gharama ya jumla shilingi bilioni 2.64.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 na mwaka 2025/2026 Serikali imetoa jumla shilingi milioni 489 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu katika zahanati ya Kasenga na kuwa kituo cha afya chenye uwezo wa kutoa huduma za dharura na za upasuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imetenga jumla shilingi milioni 300 kwa ajili ya ukamilishaji wa vituo vya afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato kikiwemo Kituo cha Afya Iparamasa kilichotengewa jumla shilingi milioni 108.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye kata za kimkakati kikiwemo Kituo cha Afya Nyamirembe ili kusogeza huduma za dharura na upasuaji kwa mama wajawazito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. GEORGE N. MALIMA aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa kituo cha afya Kata ya Iwondo ili wananchi waanze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2021 mpaka 2022 Serikali ilitoa shilingi milioni 500, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Iwondo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa. Fedha hizo zilitumika kujenga Jengo la Huduma za Wagonjwa wa Ne (OPD), maabara na kichomea taka, ambayo yamekamilika na yanatumika. Jengo la huduma za uzazi na upasuaji, ujenzi upo hatua ya plasta na jengo la kufulia hatua ya kupaka rangi.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imetenga jumla ya shilingi milioni 50 katika mwaka wa fedha 2025/2026. Mwaka 2026/2027 itatenga jumla ya shilingi milioni 50, kwa ajili ya kukamilisha majengo yaliyosalia katika Kituo cha Afya Iwondo. (Makofi)
MHE. ENG. CHACHA M. WAMBURA aliuliza:-
Je, hatua gani zimefikiwa katika kuandaa mpango wa kuendeleza na kukamilisha ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu - Manispaa ya Geita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): alijibu:-
Mheshimiwa Spika, uwanja wa mpira wa miguu - Geita ulianza kujengwa mwaka 2021 kwa kutumia fedha za uwajibikaji wa kijamii wa mashirika (CSR) kwa gharama ya shilingi bilioni 5.46 kupitia mgodi wa Geita Gold Mine. Hata hivyo, ujenzi ulisimama mwaka 2023 ukiwa 71%, baada ya Mkandarasi EFQ Co. Ltd kusitishiwa mkataba kutokana na mabadiliko ya kanuni ya miradi ya CSR.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na mgodi wa Geita Mine Ltd imepata mkandarasi mshauri NORPLAN ambaye amefanya mapitio ya gharama halisi za kukamilisha ujenzi wa uwanja huo na kiasi cha shilingi bilioni tano zinahitajika. Aidha, Serikali inaendelea na mapitio ya gharama zilizowasilishwa na mkandarasi mshauri ili kuweza kuendelea na ujenzi kupitia fedha za CSR zitakazotengwa katika mwaka 2026/2027.
MHE. MOSES C. BUJAGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itatimiza ahadi ya ujenzi wa Vituo vya Afya Walla, Mwambomba, Mwagi, Mhandi na Mwamala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Moses Charles Bujaga, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi 2024/2025 Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya kwa ujenzi wa vituo vya afya katika kata za kimkakati kote nchini, zikiwemo Kata za Isunga, Kadashi, Kikubiji na Hungumalwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Disemba, 2025 Serikali ilikuwa imekamilisha ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya 898 ambavyo vinatoa huduma ngazi ya kituo cha afya ikiwa ni pamoja na huduma za upasuaji wa dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa kujenga vituo vya afya katika Kata za kimkakati ikiwemo Kata ya Walla ambayo imetengewa jumla ya shilingi milioni 250 katika mwaka wa fedha 2025/2026. Utekelezaji utaendelea kwenye Kata zitakazokidhi vigezo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kadiri fedha zitakavyopatikana. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -
Je, lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kupeleka gari la kubebea wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Nyakahura Wilayani Biharamulo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi 2024/2025 imenunua jumla ya magari 594 zikiwemo ambulance 382 na magari ya usimamizi ufuatiliaji 212 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo imepokea gari moja la kubebea wagonjwa mwezi Novemba, 2023 na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo. Aidha, idadi hii inafanya Halmashauri ya Biharamulo kuwa na jumla ya magari matatu ya kubebea wagonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa magari ya wagonjwa kwa awamu kwa ajili ya vituo vya afya vyenye uhitaji kote nchini kikiwemo Kituo cha Afya Nyakahura. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Afya katika Kata ya Buguruni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Segerea, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya ngazi ya msingi kwa kujenga vituo vya afya kwenye kata za kimkakati. Buguruni ni miongoni mwa kata zilizopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam yenye wakazi wapatao 47,278. Kwa sasa hii wanapata huduma za afya katika Kituo cha Afya cha Buguruni na Zahanati ya Bungoni umbali usiozidi kilometa mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2023/2024 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilifanya uthamini na kulipa fidia nyumba tatu kiasi cha shilingi milioni 245 kwenye eneo lenye ukubwa wa takribani mita za mraba 900 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, eneo hilo halitoshelezi ambapo mwaka 2026/2027 Serikali kupitia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imefanya tathmini na kulipa fidia takribani nyumba saba ili kuongeza ukubwa wa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Buguruni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2025/2026 Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetenga jumla ya shilingi bilioni nne kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Kisuru. Ujenzi huu ni wa ghorofa na Halmashauri ya Jiji ipo katika maandalizi na utaratibu wa manunuzi ya kumpata mzabuni. (Makofi)
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara za kuunganisha vijiji vilivyoanzishwa toka mwaka 1974 katika Jimbo la Tunduru Kusini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Fadhili Sandali Chilombe, Mbunge wa Tunduru Kusini, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuunganisha vijiji vyote 65 vilivyopo katika Wilaya ya Tunduru ili kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kufikisha huduma za kijamii. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imeendelea kuhudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 1,203.61 katika Wilaya ya Tunduru ambapo maeneo ya Jimbo la Tunduru Kusini pia yamepewa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuunganisha vijiji ambavyo havijafikiwa tangu mwaka 1974, Serikali kwa kutumia fedha za maendeleo ya jimbo na nyongeza ya tozo ya mafuta imeendelea kufungua barabara za kuunganisha vijiji. Mpaka sasa imeshafungua barabara mpya zenye urefu wa kilometa 117.7 ambapo shilingi bilioni 1.25 zimetumika kufungua Barabara za Semen – Tupendane – Mchesi, Nalasi – Nasomba – Lukala, pia Barabara ya Chikomo – Mkandu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtandao wa barabara wa TARURA ni kilometa 144,149.18 ambapo Serikali inaendelea kupanua mtandao huu, ili kuwezesha kufikia maeneo mbalimbali, ikiwemo ya vijijini. Kadri Serikali inavyojenga uwezo wa kibajeti wa wakala itawezesha maeneo mengi nchini kufikiwa, vikiwepo vijiji vilivyoanzishwa toka mwaka 1974 katika Jimbo la Tunduru Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA aliuliza:-
Je, hatua gani inachukuliwa kuhakikisha usimamizi, utoaji, urejeshaji wa mikopo 10% ya halmashauri unakuwa wazi na unawafikia walengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Daniel Mburarugaba, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Kagera kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kuhakikisha mchakato mzima wa usimamizi, utoaji na urejeshaji wa mikopo unakuwa wa uwazi na usawa. Utaraibu huo umeainishwa kwenye kanuni na katika mwongozo ambao halmashauri zote nchini zimepatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni, mwongozo pamoja na vitini vya mafunzo vinaelekeza halmashauri baada ya kukusanya fedha kwa ajili ya mikopo zinapaswa kutoa tangazo kwa njia mbalimbali ili kuufahamisha umma. Sambamba na hilo Serikali imeunda mfumo wa kielektroniki wa utoaji na usimamizi wa mikopo ambapo kila mwombaji anautumia kuomba mkopo. Mfumo huu unatumika pia katika usimamizi wa shughuli za vikundi pamoja na kufuatilia marejesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua hii imesaidia kuweka wazi uwajibikaji katika kila hatua ya utoaji wa mikopo, usimamizi na marejesho. Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa kunakuwa na uwazi katika uombaji na utoaji wa mikopo, kama kanuni na miongozo inavyoelekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Afya Mnadani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Jimbo la Hai, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2025/2026, Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 3.08 kwa ajili ya ujenzi wa ukarabati wa miundombinu katika Hospitali ya Wilaya ya Hai, ujenzi wa Vituo vya Afya Chekimaji, Masama na Nkwansira pamoja na ukamilishaji wa maboma nane ya zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kimkakati cha KIA. Ujenzi wa kituo hicho umekamilika na taratibu za usajili zinaendelea na kitaanza kutoa huduma za wagonjwa wa nje (OPD) mwezi Mei mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ujenzi wa vituo vya afya kote nchini kikiwemo Kituo cha Afya Mnadani katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Shinyanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Halmashauri ya Shinyanga ni miongoni mwa hospitali za awamu ya kwanza 68 zilizoanza kujengwa katika mwaka 2018/2019. Mpaka sasa jumla ya shilingi bilioni 3.49 zimeshatolewa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Shinyanga ambapo jumla ya majengo 17 yamejengwa. Majengo mengine 10 yamekamilika na majengo saba yapo katika hatua ya ukamilishaji. Hospitali ya Halmashauri ya Shinyanga ilianza kutoa huduma Julai, 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa miundombinu ya Hospitali umekuwa ukitekelezwa kwa awamu. Katika mwaka wa fedha 2026/2027 Hospitali ya Halmashauri ya Shinyanga imetengewa shilingi milioni 200 kwa ajili ya kukamilisha majengo saba yaliyosalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa awamu kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. DKT. WILSON C. MAHERA aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa majengo muhimu yanayohitajika katika Hospitali ya Wilaya Butiama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, naomba kumjibu Mheshimiwa Dkt. Wilson Mahera, Mbunge wa Jimbo la Butiama:-
Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Butiama ni moja kati ya hospitali 25 ambazo zimejengwa katika awamu ya tatu ya ujenzi wa hospitali za halmashauri ambao ujenzi ulianza mwaka 2021/2022. Jumla ya majengo tisa yamejengwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Butiama kwa gharama ya shilingi bilioni 3.02.
Mheshimiwa Spika, majengo yaliyokamilika ni pamoja na jengo la OPD, maabara, EMD, jengo jumuishi la uzazi, yaani martenity complex. Aidha, jengo la OPD limekamilika na huduma za wagonjwa wa nje zimeanza kutolewa mwezi Novemba, 2024.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2026/2027 hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama imetengewa shilingi milioni 500, kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo yaliyosalia. Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa awamu, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu muhimu katika hospitali za Halmashauri Wilaya ya Butiama.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. CHARLES M. NJAMA aliuliza:-
Je, Serikali haioni kuwa ipo haja ya kujenga majengo mapya katika Hospitali ya Magunga badala ya kuendelea kuweka viraka kila mwaka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles Mhando Njama, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hospitali ya Magunga ni moja ya hospitali kongwe nchini ambayo imejengwa mwaka 1952 na inahitaji ukarabati mkubwa. Katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 Serikali imetoa jumla shilingi bilioni 1.06 kwa ajili ya ujenzi wa jengo jumuishi la huduma za uzazi Maternity Complex kwa muundo wa ghorofa. Taratibu za kibali na michoro zinaendelea.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imetenga fedha shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa theatre pamoja na ukarabati wa jengo la kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Magunga. Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mipya inayohitajika katika Hospitali ya Magunga ili iweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.