Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Amosy William Maganga (4 total)

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, kwanza ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuweza kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Wilaya ya Sikonge kwa hivi sasa wanakabiliwa sana na ufinyu wa maeneo, kwa ajili ya shughuli za kiuchumi. Wilaya ya Sikonge ina jumla ya mapori tisa na kati ya haya, yaliyo mengi ni mapori ya akiba. Je, Serikali, ni wakati gani sasa haya mapori ya akiba yataanza kutumika, kwa ajili ya hao wananchi, ukizingatia kwamba, kwa kweli wananchi wanahitaji kuendesha shughuli zao za kiuchumi na hasa kilimo, ufugaji, pamoja na urinaji wa asali na kwa hivi sasa, hata viashiria vya uvunjifu wa amani vinaanza kuonekana?
SPIKA: Mheshimiwa swali lako limeshaeleweka. Ahsante.

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Sikonge, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI. Utakumbuka Bunge lako hili kipindi cha Mwaka 2021 mpaka 2025 iliundwa Kamati ya Mawaziri Nane, ambayo ilizunguka nchini kote kuainisha maeneo haya na kufanya tathmini. Hivyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge tathmini ikikamilika kwa wakati watatengewa maeneo ili wapate kufanya shughuli za uzalishaji mali, kilimo na ufugaji.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja tu la nyongeza. Kwa vile Barabara ya kutoka Ipole – Rungwa imekuwa kwenye ahadi ya Serikali kwa kipindi kirefu sasa na barabara hii imekuwa ni sehemu ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Je, Serikali haioni umuhimu kwamba sasa fedha zipatikane na barabara hiyo ianze kutengenezwa na impendeze Mwenyezi Mungu hii barabara ikamilike hata kabla ya mwaka 2030?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Mheshimiwa Mbunge kwamba hii barabara imeshafanyiwa usanifu na kwa sisi kama Serikali imekuwa ni moja ya barabara kubwa na Barabara Kuu (Trunk Road) ndefu ambayo haijajengwa kwa kiwango cha lami. Tunavyoongea sasa hivi, Serikali inatafuta chanzo sahihi kwa maana ya kuijenga hiyo barabara kuanzia Ipole – Rungwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, atakubaliana nami, lakini kutoka Rungwa – Singida ambako tumeshaanza na kutoka Rungwa – Makongorosi ili kuiunga Tabora, Singida na Mkoa wa Mbeya kwa kiwango cha lami. Mpango upo mkubwa wa kutafuta chanzo cha uhakika ili kuikamilisha barabara hiyo. Ahsante.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini kituo chetu cha afya kilichopo Kata ya Kipili, Jimbo la Sikonge, kitajengewa jengo la wagonjwa wa nje (OPD)?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, Serikali tumejielekeza katika mwaka huu wa fedha angalau kukamilisha majengo ya OPD katika vituo hivi vya afya na yaanze kutoa huduma. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, katika mwaka huu wa fedha tutakamilisha jengo hilo la OPD na lianze kutoa huduma.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tunaishukuru Serikali kwamba tunayo Hospitali ya Wilaya ya Sikonge, lakini haina uzio na kumekuwa na changamoto nyingi sana zinazosababishwa na kukosekana kwa uzio. Je, ni lini Serikali itatujengea uzio katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Sikonge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kusisitiza halmashauri, kwanza kufanya tathmini na kutenga fedha za kujenga uzio. Pia tutawasilisha maombi haya TAMISEMI, na kujiridhisha, kisha kuanza ujenzi wa uzio katika hospitali zote za halmashauri.