Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Shaffin Ahmedali Sumar (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. SHAFFIN A. SUMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote ninaanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya na uhai na hatimaye tumeweza kukutana leo hii. Ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kwa ajili ya Watanzania. Ninamshukuru sana pia kwa kuniteua kuwa miongoni mwa wagombea kupitia Chama Cha Mapinduzi na hatimaye leo hii nipo mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana wananchi wote wa Jimbo la Uyui kwa kuniamini na kwa kunichagua na hakika nitawatumikia. Bila kusahau, ninampongeza sana Jemedari wetu, Mwenyekiti wetu wa Mkoa wa Chama Cha Mapinduzi, ndugu Said Mkumba kwa namna anavyotushauri na kuendeleza masuala ya chama katika mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kusahau, ninampongeza sana Mkuu wetu wa Mkoa, ndugu Paul Matiko Chacha kwa namna ambavyo anaifanyia kazi Tabora yetu kwa kushirikiana na timu yake ya Ulinzi na Usalama. Hakika Tabora sasa hivi inapiga hatua za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme suala moja la huzuni ambalo limetokea sasa hivi kwa bahati mbaya katika Jimbo langu la Uyui Kata ya Ilolangulu, Shule ya Msingi ya MCBS Roma hivi sasa inaendelea kuteketea na moto. Ninaomba nitumie nafasi hii kuwapa pole wahanga wote, lakini jambo la kushukuru ni kwamba hakuna mtoto au mwanafunzi hata mmoja aliyepoteza maisha. Zimamoto wameshafika na wanaendelea kusaidiana na wananchi Mungu asimame nao katika kipindi hiki kigumu na mimi pia niko pamoja nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo chetu cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kilianzishwa mwaka 1963 ni dhahiri kwamba chuo hiki kimekuwa cha zamani, lakini ni miongoni mwa vyuo vichache ambavyo vilianzishwa hapa Tanzania baada ya uhuru. Pamoja na uchakavu wa chuo hiki bado kinafanya kazi nzuri sana. Nimpongeze sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa chuo hiki na cha kihistoria ameanza kupeleka fedha kwa ajili ya mabweni na jengo la utawala, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la utawala limeshakamilika kwa takribani 80% kilichobakia ni kipande kidogo wanahitaji kama bilioni 4.7 hivi ili jengo likamilike ikiwa ni pamoja samani zote zinazohitajika. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, namna ambavyo anafanya kazi nzuri, namna ambavyo anawatetea Watanzania, ninaomba na hii sehemu ya Tengeru atuone kwa jicho la huruma atusaidie hizo fedha tuweze kukamilisha huo mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo kama hivi vinatuzalishia vijana ambao wanaenda kufanya kazi za maendeleo ya jamii. Hawa ndiyo wanaenda katika kata mbalimbali wanashirikiana na jamii, kuisaidia jamii kupata maendeleo. Sasa vijana wanapokuwa wametoka chuoni na kwenda kwenye kata mbalimbali nafasi wanapata kazi za Maafisa Maendeleo ya Jamii, lakini wanakosa usafiri wa kwenda kuwazunguzukia jamii. Ninaiomba Serikali ione namna bora ya kuwasaidia hawa Maafisa wetu wasibaki kuwa ofisini tu, wasaidiwe usafiri waweze kuitembelea jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii sasa hivi inafanya vizuri sana. Hapa nimpongeze sana Waziri wa Kazi, Ajira, Mheshimiwa Deus Sangu anasimamia vizuri, anazifanyia kazi vizuri. NSSF imekuwa ikifanya vizuri mwaka hadi mwaka na uwekezaji wa NSSF sasa hivi kwa kweli ni mkubwa sana, unaridhisha. Tunaridhika kwa sababu fedha hizi ni fedha za Watanzania tunaona kabisa zinaenda kufanya kazi na faida inapatikana. NSSF wamewekeza kwenye kiwanda cha sukari, lakini pia NSSF wanaenda kumalizia jengo la Mzizima Towers ambayo inaenda kukamilika mwezi Desemba, 2026. Mwakani Insha Allah Dkt. Samia Suluhu Hassan ataenda kuzindua panapo uzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji kama huu ndiyo unahitajika katika nchi yetu. Leo ukitizama Mfuko wa PSSSF nao pia wamewekeza vizuri katika Kiwanda cha Ngozi kilichopo Kilimanjaro ni uwekezaji mzuri sana. Sisi Watanzania na Serikali yenyewe tunatakiwa tuunge mkono juhudi za Mifuko yetu ya NSSF. Nitaiomba sana Serikali yetu kwamba, kwa kuwa tuna Kiwanda cha Ngozi ambapo pia viatu vya aina mbalimbali vinatengenezwa vikiwemo vya kijeshi, basi Serikali yetu kupitia majeshi yetu wanunue viatu vyote kutoka kwenye kiwanda chetu cha ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA imezungumziwa sana hapa na wengi sana wanalalamika kuhusiana na suala zima la barabara. Nami pia katika jimbo langu ni muathirika wa barabara. Bajeti inayopangwa kwa TARURA kwa mwaka haiendani na uhalisia wa wingi na mtandao wa barabara. Kwangu bajeti iliyopo ni bilioni 1.5 kwa mwaka hivi tunavyoongea katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 fedha ambazo zimepelekwa TARURA hazizidi hata milioni 350. Kwa hali hii tunawasaidiaje Watanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali iangalie namna mbadala katika tozo ambazo zimewekwa kwa ajili ya barabara kupitia TARURA, basi hizo fedha ziweze kupatikana kwa wakati. Nitatoa mfano mdogo sana ambao unafanana na mifano mingi ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia hapa kabla yangu. Nina Barabara moja ambayo ni ya Ndono – Ufuluma – Makazi ina kilometa 43 tu, lakini leo tunavyoongea huu ni mwaka wa saba barabara hiyo haijafanyiwa marekebisho hata kidogo, hali ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi wanaoishi katika hizi kata tatu ni zaidi ya kata 52,000 kufuatana na Sensa ya 2022. Wakazi 52,000 wanakosa huduma ya barabara, lakini barabara hii katika msimu na msimu unaanza katikati ya mwezi Aprili na kuelekea mwishoni mwa mwezi Aprili. Kwenye msimu barabara hii inasafirisha tumbaku yenye thamani ya bilioni 22. Hakika hii inaonyesha kwamba TARURA haina uwezo wa kuhudumia hii barabara ambayo ina kilometa 47 tu. Ninaomba sana ama fedha ziongezwe kwa TARURA, ama hii barabara ipewe kipaumbele basi ipandishwe hadhi iwe chini ya TANROADS iweze kuhudumiwa ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa juhudi za Dkt. Samia Suluhu Hassan, sisi katika Mkoa wetu wa Tabora tunanufaika na Mradi mkubwa wa Maji kutoka Ziwa Victoria. Kwa kweli mradi ni mzuri na ifikapo mwaka 2028 nina uhakika kwamba wilaya zote za Mkoa wa Tabora zitakuwa zinatumia maji ya Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri, maji ya Ziwa Victoria kwa Manispaa ya Tabora Mjini yamefika sehemu inaitwa Bwawa la Igombe. Kutoka Bwawa la Igombe miundombinu iliyopo inasambaza maji haya, lakini pale pale pembezoni mwa Bwawa la Igombe kuna vijiji vingi ambavyo bado havijanufaika na maji ya Ziwa Victoria na havimo katika mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Waziri Mkuu kupitia Wizara husika ya Maji aangalie utaratibu wa kuwasaidia wananchi ambao wako pembezoni mwa Bwawa la Igombe kwa sababu tukisubiri mradi huu ukamilike na uwafikie ni muda mrefu. Tunaweza tukapata solution ya muda mfupi tukawasaidia hawa wananchi wakanufaika na maji ambayo Mama Samia ameyafanyia kazi kwa juhudi kubwa na anataka kuona kila kitongoji kinapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa kuja na programu nzuri ya uanagenzi. Hii programu ni nzuri na imetengewa fedha vizuri. Kuna theluthi moja ambayo inatokana na mapato ya SDL yanayokusanywa na TRA. Fedha hizi zinapokusanywa kila mwezi kabla ya tarehe saba (7) huwa zinaenda TRA na ni fedha za uhakika…

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umekwisha?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ndiyo, muda wako umekwisha Mheshimiwa.

MHE. SHAFFIN A. SUMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie. Ninaomba hizi fedha ambazo zinavyokusanywa na TRA, inafanya kazi nzuri ya kukusanya zaidi ya makadirio, basi fedha kwa ajili ya wanagenzi iweze kutolewa kwa usahihi na kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)