MHE. EDIFONSI J. KANONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pia ninashukuru kwa kupata mradi wa barabara kutoka Matai – Kashesha ambayo ni ya kilometa 50.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ikikamilika, itachochea uchumi sana katika Wilaya ya Kalambo, na Serikali itakusanya mapato katika Kituo cha Forodha Kashesha. Wananchi wa Kalambo wanataka kupata majibu ya Serikali, je, ni lini barabara hii ambayo inaendelea kusuasua, itakamilika ili waweze kufaidika? Watapata ajira, tutachochea Uchumi, na pia tutapata wawekezaji kwa sababu ipo mpakani mwa Zambia na Tanzania.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakiri kwamba hii barabara ni muhimu sana na hasa kwa kipindi hiki kwa sababu ni moja ya barabara kuu, na pia tuna kituo chetu cha forodha kule. Tunavyoongea barabara hiyo kutoka Matai – Kasese ina kilometa 50. Mheshimiwa Mbunge atakubalina, kwamba, ili kufanya haraka tumeigawa katika vipande viwili, kwa maana ya lots; Matai – Tatanda, Tatanda – Kasesya na tuna Wakandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tumechelewa kwa sababu mkandarasi alikuwa anadai. Tumeshamlipa na mkandarasi wa kipande cha pili tunafanya maandalizi ya kumlipa ili barabara hii iweze kukamilika, kwa sababu sasa magari mengi yanayotokea Zambia yanapita huko kwenda mikoa ya Kaskazini na hata kwenda nchi jirani. Kwa hiyo, tunalitambua hilo na tunalipa umuhimu mkubwa sana kuhakikisha kwamba hiyo barabara yote inajengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.