Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Edefonce Joackim Canoni (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. EDIFONSI J. KANONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Maendeleo ya Vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi siku ya leo. Pia ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Pia, ninakishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi Wilaya ya Kalambo na viongozi wote wa Chama cha CCM Mkoa, bila kuwasahau wananchi wangu wa Wilaya ya Kalambo ambao walinipa kura za kutosha ili niweze kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maono yake makubwa kwa kuunda Wizara ya Vijana kwa ajili ya kuwakilisha vijana, na hasa kwa kumpata Mheshimiwa Waziri kijana ambaye ana maono makubwa kwa ajili ya kuwakilisha vijana katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajielekeza kwenye mikopo. Mheshimiwa Rais amekuwa na maono makubwa kuhakikisha anawakwamua vijana kiuchumi, na hususan ukizingatia kuwa vijana ni wengi, ambao wako 76%, katika Taifa letu. Takwimu zinaonesha kuwa vijana wanaohitimu elimu ya vyuo vikuu ni kati ya vijana 500,000 mpaka 600,000 kwa mwaka. Tathmini katika miaka mitano mpaka miaka kumi tutakuwa na vijana karibu 7,000 mpaka 8,000 ambao watakuwa wamehitimu elimu mbalimbali katika vyuo vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa kulizingatia hilo, na kwa kuwa na maono makubwa, akaweka mpango wa kuunda Wizara ya vijana na kuweka fedha kwa ajili ya kuwasaidia vijana. Hili ni jambo kubwa sana ambalo linatakiwa kuungwa mkono kwa nguvu zote kwa maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha, shilingi bilioni 200 zimegawanyika katika Wizara za kisekta. Wazo langu, ninaishauri Serikali, fedha hizi zirudi katika sekta ya vijana ili vijana wawe wanajua kwamba fedha zetu ziko Ofisi ya Rais (Maendeleo ya Vijana). Zimeenda kilimo, zimeenda uvuvi, na zimeenda maendeleo ya jamii, zirudi kwa vijana ili Mheshimiwa Waziri awe anazisimamia mwenyewe. Sasa kama vijana wanaenda huku wanaambiwa rudi huku, hii haitaweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali, nina imani sana Mheshimiwa Nanauka. Hawa vijana wana shida ya kuwa matajiri na Mheshimiwa Rais ndoto yake ni kutengeneza vijana wengi kuwa matajiri...

MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kanon kuna taarifa.

TAARIFA

MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninaomba nimpe taarifa Mheshimiwa Kanoni, kwamba hata hizi Wizara mbili zilipotoa matangazo ya mikopo kwa vijana, Wizara ya vijana walisema kijana aje na andiko lisilozidi kurasa tano, halafu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikasema kijana aje na andiko lisilozidi kurasa mbili. Utaona hata Wizara hizi zinapokuwa nyingi zinawachanganya vijana. Kwa hiyo, anachosema ni sahihi. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kanoni, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. EDIFONSI J. KANONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa kwa mikono miwili. Ninasema hivyo kwa sababu gani? Mheshimiwa Rais ana malengo makubwa juu ya vijana wetu, na sisi kama Wabunge tunahitaji kuona vijana wanafanikiwa, na vijana wawe tayari kupokea mkopo kwa sababu hakuna mtu anayependa umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vijana wanamaliza vyuo vikuu halafu wanabaki, mimi mwenyewe ni mzazi ninaangalia, kama Mheshimiwa Rais anajitoa kutoa fedha kwa ajili ya kuwainua vijana kiuchumi, Serikali isisite kutoa fedha kwa ajili ya kwenda kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wanafuata hizi fedha kwenda kukopa, lakini masharti yanakuwa ni mengi. Tangazo la Serikali linasema Mheshimiwa Rais ametoa fedha kuwawezesha vijana kiuchumi. Wakienda benki wanakuta kuna masharti. Unamwambia kijana aliyetoka Chuo Kikuu aonyeshe biashara, ataonyesha biashara gani ambayo ameanzisha? Sasa hii inasababisha hizi fedha kukwama na hazitoki kama tunavyokusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama zinabaki benki, ni kwa manufaa ya nani? Sheria zibadilishwe, usimamizi ubadilishwe, na masharti yapungue. Kama ni dhamana, Wabunge tupo, Madiwani wapo, Wenyeviti wa Serikali wapo, na wa vitongoji wapo. Masharti yawe nafuu, wakopeshwe vijana ili waweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatokea Kalambo. Vijana zaidi ya 1,500 hawana kazi, lakini wana imani kubwa sana na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba hizi fedha zitawafikia na wao watanufaika kiuchumi. Hata hivyo, wanalalamika wakienda sekta ya benki wanakuta kuna masharti, wanaomba fedha mpaka miezi mitatu wanakata tamaa. Masharti yabadilishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kutengeneza vijana wa dira ya miaka 25. Tunawatengeneza vipi kama hatuwezi kuwapa fursa za fedha? Wape imani hawa vijana. Uwezo wa kufanya kazi wanao. Serikali iwape imani, kusiwe na mashaka, na kusiwe na kigugumizi katika kuwapa fedha, watafanya mageuzi makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tuna lengo la miaka mitano miaka 20, au 25, hatuwezi kwenda bila hawa vijana. Uchumi wa nchi na uchumi wa dunia unaendeshwa na sekta binafsi. Sasa kama ni sekta binafsi, halafu mikopo inatoka kwa kusuasua, unategemea kitu gani kitatokea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mashaka na Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Nanauka. Asimamie, na sisi kama Wabunge tupaze sauti hizi, fedha zirudi katika Wizara yenye dhamana na vijana ili waweze kuzisimamia wao wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoka ukanda wa kule Ziwa Tanganyika. Wale vijana wavuvi unamwambia aweke dhamana, anaweka dhamana gani? Wale vijana wengine ambao hawana shughuli, wako mtaani wataweka dhamana gani? Kwa hiyo, Serikali iamue namna ya kupunguza masharti ili vijana waweze kunufaika. Wako hapo wanasikiliza tunavyowasilisha hoja zao. Wananajaza fomu za maombi ya mikopo labda vijana 100 au 50, wanapata watu wachache kwa sababu ya masharti. Masharti yapungue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, vikundi ambavyo vinasemwa, masharti ya kuunda vikundi siyo lazima. Ikiwezekana, kama kuna utaratibu, sheria zibadilishwe ili aweze kukopa mtu mmoja mmoja, kwa sababu kuna watu wanaingia kwenye vikundi na hawataki, na hawana sifa. Sasa analazimika kuingia kwenye kikundi, anakopa fedha, na mwisho marejesho yanakuwa yanakuwa ni ya shida...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. EDIFONSI J. KANONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. EDIFONSI J. KANONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana. Kipekee kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi siku ya leo ili niweze kuchangia katika Hotuba ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Pia, nikishukuru chama changu kwa kusimama hapa kwa mara ya kwanza katika Bunge lako Tukufu. Pia nishukuru sana wananchi wa Kalambo walionichagua na kunipa dhamana ya kuja kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu. Pia nimshukuru Mheshimiwa Rais chini ya Kamati Kuu kwa kuniteua na hatimaye kushinda uchaguzi. ninasema sina cha kumlipa Mheshimiwa Rais, zaidi ninamwombea dua na afya njema na wasaidizi wake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajielekeza kwanza kwenye kilimo. Mimi ninatoka Jimbo la Kalambo na wananchi wa Kalambo ni wakulima. Nishukuru sana kipekee kwa huduma ambayo Mheshimiwa Rais anaendelea kutoa kwa kutoa ruzuku kwenye pembejeo. Sisi kama Kalambo na wananchi wa Kalambo wamenituma nilete salamu za shukurani kwa Mheshimiwa Rais na Serikali yake; kwamba tumeendelea kunufaika vizuri, tumeendelea kuvuna vizuri na wananchi wamehamasika sana, wamelima kwa juhudi na tumeendelea kuvuna zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika hilo wamenituma nije niseme kuomba kwa Serikali. Mwaka jana tulikuwa na mavuno ya tani 265,600, lakini Serikali ilinunua tani 3,500. Mwaka jana Serikali ilinunua tani 5,500, kati ya tani 265,000. Mwaka huu tunatarajia kuvuna tani 299,500. Niombe kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na chini ya Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Chongolo, bajeti iongezwe kwa ajili ya kuweza kununua mahindi ya kutosha ili hawa wananchi waweze kunufaika kwa sababu uzalishaji umeongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mahindi yanayonunuliwa ni kidogo, yanayobaki ni mengi. Serikali iangalie namna itakavyoweza kuongeza fedha na kupanua masoko ili kuboresha hao wakulima wetu, ambapo tegemeo la wananchi wa Kalambo 97% ni kilimo. Kwenye hayo mahindi au mazao ambayo inaendelea kununua Serikali imekuwa ikichukua mahindi hailipi fedha kwa wakati. Ijitahidi kuhakikisha inaboresha mifumo ili wananchi walipwe kwa wakati ili baadaye wajiandae katika na msimu ule unaokuja wa kilimo. Hizo ni salamu za wananchi wa Kalambo hususan hawa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninakwenda TAMISEMI; nimeendelea kumsumbua sana Profesa Shemdoe pale kutokana na changamoto ambazo ziko upande wa TAMISEMI. Ninaanza na miundombinu kwa sababu miundombinu ndiyo uchumi wenyewe. Jiografia ya Kalambo ina wakazi laki tatu hamsini na zaidi, lakini kuna changamoto ya miundombinu. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais ameendelea kuleta fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu hasa upande wa barabara za vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Pamoja na kuletwa kwa fedha hizo, kuna baadhi ya barabara ambazo zimekuwa hazipitiki kwa muda mrefu, hususan Barabara ya Samazi ambayo ina kilometa 22, haijakarabatiwa kwa zaidi ya miaka 12. Barabara hii ina urefu wa kilometa 22. Wananchi wanavyotoka kule chini ziwani kuja kufuata mahitaji yao wilayani na mkoani hiyo kilometa 22 wanatumia masaa mawili na nusu. Tunaomba kupitia Wizara ya TAMISEMI Mheshimiwa Waziri aweze kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mahitaji ya Daraja la Mto Saisi ambalo linaunganisha kata mbili, Kata ya Mambwekenya na Mambwe Nkoswe ambako kuna wakazi zaidi ya 60,000 hili daraja ni muhimu sana kwao kiuchumi. Pia limeendelea ajali kutokana na kujaa kwa maji katika msimu wa mvua. Hata wiki jana tumepoteza kijana mmoja wa Kizambia ambaye alikuwa anavuka kufuata mahitaji Tanzania, pamoja na mtoto mchanga wa miezi saba. Pia tuna mahitaji ya daraja la kuunganisha Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga DC na Wilaya ya Kalambo ya Kilometa 22.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Matai ni mji ambao unakua kwa kasi kutokana na shughuli za uchumi wa kilimo, lakini hatuna barabara za lami. Tunaomba ikimpendeza tupate barabara za lami ambazo nilimwomba Mheshimiwa Rais wakati anapita kwenye kuomba kura mwaka 2025. Ikimpendeza basi tuanzie na kilometa 10 ili kuboresha mazingira. Ule Mji uko pembezoni mwa Kongo na Zambia, kwa hiyo kiuchumi tukiboresha barabara zetu zitavutia zaidi na zitachochea uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katikati ya Mji wa Matai vilevile, tuna mahitaji ya daraja. Kuna daraja moja linalounganisha Makao Makuu ya Mji ambalo lipo katikati. Daraja lile ni la muda mrefu na limeendelea kuleta shida. Kwa hiyo limeendelea kuleta shida wakati wa msimu wa mvua. Tupate daraja la kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa afya, afya ni maisha. Jiografia ya Jimbo la Kalambo tuna kata 23. Katika kata 23 tuna vituo vya afya vitatu vinavyofanya kazi. Kimoja ni cha mwaka 1982, kipo katika Kata ya Mpombwe katika Kijiji cha Ngorotwa. Kimekuwa ni chakavu. Tangu mwaka 1982 hadi leo hakijakarabatiwa. Tunaomba kupata fedha kwa ajili ya kukiboresha kituo cha afya hicho kikongwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vituo vya afya vinne ambavyo vimeanza kujengwa zaidi ya miaka saba, lakini havijakamilika. Wananchi wanasubiri vikamilike ili viendelee kutoa huduma. Pia, hospitali yetu ya wilaya imeendelea kujengwa na kuboreshwa, lakini kuna upungufu wa watumishi. Mahitaji ni 201 tulionao ni 84. TAMISEMI waangalie namna ya kuweza kutuwezesha ili wananchi waendelee kunufaika na huduma ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya vituo vya afya vilivyobaki ni 15, ikiwa ni pamoja na Kasanga, ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka 2019, Waziri Mkuu Mstaafu. Vilevile kuna Kata za Mkowe, Kisumba, Mbuluma, Msanzi, Ulumi, Kanyezi, Katazi pamoja na Kata nyingine kama hizo; kuna mahitaji makubwa sana ya vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na shule chakavu nyingi, tuna magofu ambayo ni mapagale zaidi ya 143. Tunahitaji mchango wa Serikali ili tuweze kukamilisha katika shule hizi. Tuna mahitaji ya sekondari, sekondari ziko tatu tu, ambazo zipo katika Kata za Sundu, Kilesha na Katazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwa upande wa uvuvi, mimi ni mdau wa uvuvi. Kwa taarifa tulizonazo ni kwamba Serikali inategemea kufungua Ziwa Tanganyika. Hili Ziwa Tanganyika lina historia kubwa, lakini kutokana na uharibifu wa mazingira pamoja na uvuvi haramu, ambapo sheria zimeshindwa kusimamiwa, ndiyo maana unaona hii hali ya kuendelea kufunga ziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali, pamoja na kufunga Ziwa, kama hatutaweza kusimamia sheria haitatusaidia kitu chochote. Uvuvi haramu umeshamiri sana katika maeneo yetu. Maafisa Uvuvi wapo, sheria zipo, lakini inaonekana ni butu, hazifanyi kazi. Sasa hata kama watafunga ziwa leo na bado wakifungua uvuvi haramu utaendelea ina maana tunaua mazalia ya samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ziwa Tanganyika tuna aina ya samaki 220; na hakuna ziwa ambalo lina samaki wa mapambo Tanzania kama Ziwa Tanganyika, lakini kwa sababu ya uharibifu wa mazingira samaki wanaendelea kupungua. Pia kumetokea oparesheni ambazo zimekuwa zikiendelea katika kudhibiti uvuvi haramu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeishauri Serikali waanze kudhibiti kwanza wale ambao wanasambaza hivi vifaa vya uvuvi haramu halafu badaaye ndipo waende huko katika kusimamia hizo sheria. Kwa hiyo niombe sana, kwa sababu ya kutaka kufunga ziwa waangalie kwanza zile sheria wamezisimamia kwa kiasi gani. Pia watupe tathmini. Samaki walioko kule wanaovuliwa ni migebuka na dagaa, lakini kuna sangara pia. Sangara walioko mwanza walipandikizwa kutoka Ziwa Tanganyika, mwaka 1955; mbona hatujapewa rekodi ya samaki hao hadi sasa hivi? Maana kiasi cha samaki sangara wanaovuliwa katika Ziwa Tanganyika ni karibu chini ya asilimia tano. Sasa hao samaki sangara wako wapi? Kwa nini wanaongelewa migebuka tu? Sangara pia wapo. Kuna aina nyingi ambazo tunaweza kunufaika kwa ajili ya kuboresha maisha yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, uvuvi haramu umeendelea na kuharibu vyanzo na pia uharibifu wa mazingira. Hizi nyavu zinazotumika, nyavu ile ikikatika kwenye maji inaoza baada ya miaka 100. Sasa, itakua imeharibu kizazi kiasi gani cha samaki?

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali vilevile ije na mpango wa kuunda mitumbwi ili kunusuru maisha ya wavuvi. Wavuvi wanakufa sana kutokana na vifaa na miundombinu wanavyotumia ambavyo ni vya kizamani. Serikali ilete mpango wa kutengeneza vifaa vya kisasa kama vile fiber ili kunusuru maisha yao. Wanapoteza sana maisha; ukianzia mpakani Kagunga mpaka uje huku Kasanga wananchi na wavuvi wanapoteza sana maisha kwa sababu ya kukosa vifaa vya kisasa. Hata hivyo, kwa kuhifadhi mazingira vitapunguza; kwa sababu kuanzia Kigoma mpaka kufika huku Rukwa ni mitumbwi zaidi la laki tatu; ambayo yote inavuna miti kutoka kwenye maeneo yetu ya Serikali na kuhatarisha mazingira katika maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante muda wako umekwisha, malizia…

MHE. EDIFONSI J. KANONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamalizia kwa kuchangia upande wa suala la mafuta. Mafuta imekuwa ni changamoto ya dunia. Niombe kwa Serikali sikivu ya Mheshimiwa Rais iangalie namna ya kumsaidia mwananchi wetu huyu ambaye kipato chake ni cha chini. Katika lile ongezeko la shilingi elfu moja Serikali iangalie itachangia kwa kiasi gani ili kuweza kusaidia maisha ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)