Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Juma Ramadhani Mustafa (3 total)

MHE. JUMA R. MUSTAFA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Wizara. Kwanza kabisa ninapenda kuwapongeza kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kuzifanya, lakini ninampongeza Mheshimiwa Rais, wananchi wa Jimbo la Igalula wanamshukuru kwenye chanjo ya ruzuku, kuondoa na utambuzi wa mifugo.
Mheshimiwa Spika, nina swali moja la nyongeza; je, Serikali ina utaratibu gani wa kisheria na kiutendaji, ili kuhakikisha sasa maeneo haya yaliyotengwa hayavamiwi na hayabadilishiwi matumizi ili kuweza kuepuka migogoro kati ya wakulima na wafugaji ndani ya Jimbo la Igalula?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Mustafa Kawamba, Mbunge wa Igalula, Halmashauri ya Uyui, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na Sheria mbalimbali ambazo zimekuwa zikitu-guide na zimepitishwa na Bunge lako Tukufu. Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, hii ilikuwa inatoa hati ya Hatimiliki ya Kimila, lakini kuna Sheria ya Ardhi Namba Sita ya Mwaka 2007, ambayo imeainisha mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji, lakini kuna maeneo ya kilimo na malisho ya mifugo, yote yameainishwa katika Sheria hii. Sambamba na sheria hizi pia, kuna Sheria Namba 287, ambayo imewezesha halmashauri kutunga Sheria Ndogo. Kwa hiyo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaziagiza Halmashauri zote nchini zifuatishe Sheria hizi na kuona zinatatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao.
MHE. JUMA R. MUSTAFA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninapenda niipongeze Serikali kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kuzifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Kata ya Loya ni kata ya kimkakati kiuchumi katika Jimbo la Igalula imepakana na kata sita, lakini pia imepakana na Halmashauri ya Igunga na Halmashauri ya Ikungi Mkoa wa Singida.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni haja sasa ya kupitia hizi barabara zilizopo ndani ya Kata ya Loya na kuweza kubaini maeneo korofi na ili kuweza kuyaunganisha kwenye bajeti ya ujenzi wa daraja hili, kwani tukienda kuwekeza hizi shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili, kama kuna maeneo mengine yatakuwa hayapitiki kirahisi, hatutakuwa tumeweka tija zaidi katika uwekezaji huu ambao Serikali inakwenda kuwekeza shilingi bilioni 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ni lini mkandarasi msimamizi atapatikana? Ni lini ujenzi utakwenda kuanza kwa daraja hili la Loya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu kwenye swali langu la msingi, tayari Serikali imeshaanza kutenga fedha, na wote tunafahamu kwamba ujenzi unakua hatua kwa hatua. Kwa hiyo, tukitenga shilingi milioni 318 kwa ajili ya kufanya usanifu, ndiyo maana tumeweza kujua gharama halisi za madaraja yote Matano; kubwa moja na yale madogo manne kwa gharama ya shilingi bilioni 26.68.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mwaka wa fedha huu unaokuja tutakwenda kuzijenga Barabara ya Loya, lakini siyo tu barabara hiyo, kwenye jimbo la Mheshimiwa Mbunge tunakwenda kujenga Barabara ya Esuli Minyenze, vilevile Barabara ya Mwisole - Minyeze - Nyahua, Barabara ya Malongo – Mabeshi; na kwenye hilo daraja, linaunganishwa na Barabara ya kutoka Mabeshi pamoja na kutoka Miswaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imejipanga kikamilifu kujenga barabara hizo ili wananchi wa Igalula waweze kunufaika nazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili kama nilivyosema kwenye swali la msingi, tupo hatua za mwisho za manunuzi za kumpata Mhandisi Msimamizi. Muda wowote kuanzia mwezi Mei, kama nilivyosema, tutakuwa tumeshapata mkandarasi na ujenzi utakuwa unaanza.
MHE. JUMA R. MUSTAFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza kwenye Wizara ya TAMISEMI. Kwanza kabisa ninapenda kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ambazo inaendelea kufanya.

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya umaliziaji wa maboma ya vituo vya afya vilivyomo ndani ya Jimbo la Igalula? Vituo hivyo vilivyopo ndani ya Jimbo la Igalula ni Kata ya Tura, Goweko, Kizengi, Lutende na Loya, kwani ndani ya Jimbo la Igalula hatuna hata kituo kimoja cha afya kilichokamilika majengo. Tunaiomba Serikali itusaidie kutupelekea fedha.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kawamba, Mheshimiwa Mbunge wa Igalula na ninampongeza sana ndugu yangu kwa kufuatilia hali na mahitaji ya wananchi wa Jimbo la Igalula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie na hata Bunge lililopita nilimhakikishia kwamba tutakwenda kuhakikisha tunaboresha maeneo haya ya vituo vya afya, tunamalizia maboma ambayo bado yameonekana ni changamoto ili kuweza kutoa huduma katika Jimbo la Igalula na Wana-Igalula waweze kupata tabasamu la Mheshimiwa Dkt. Samia Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.