MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi nyingine ya maswali ya nyongeza. Swali langu la kwanza la nyongeza, ninataka kuuliza mradi wa umwagiliaji wa Kata ya Sigili, Vijiji vya Iyalemwalagwa na Bulambuka umefikia 39%; na mradi huu umeanza kujengwa tangu 2023, wastani sasa wa chini ya 10% kila mwaka.
(a) Je, ni lini wataweza kuukamilisha mradi huu ili uweze kuwasaidia wananchi katika shughuli za kilimo?
(b) Je, ni lini mtaanza ukarabati wa bwawa lililopo Kata ya Kahama ya Haranga, ili liendelee kusaidia wananchi walioko huko katika shughuli za kilimo, ufugaji pamoja na uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Luhende, Mbunge wa Jimbo la Bukene kwa maswali yake ya msingi. Nimthibitishie tu jambo moja, kwamba miradi yote ambayo inatekelezwa katika eneo la jimbo lake na maeneo mengine yote nchini, Serikali tulishaiweka katika mipango. Jukumu letu ni kuhakikisha kwamba inakamilika kwa wakati. Kwa hiyo, hata hili Bwawa la Bulambuka ambalo amesema ni lini litakamilika, niseme litakamilika kulingana na mkataba ambao tulikuwa tumeandikishana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba muda ulizidi kwa sababu kulikuwa na changamoto ya kifedha. Sasa hivi Wizara ya Fedha imeji-commit kutoa fedha kila mwezi ambazo zitasaidia sisi kuwalipa wale wakandarasi ili waweze kukamilisha ile miradi kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jibu hilo la kwanza ndilo linaloambatana na vilevile katika mradi wa Bwawa la Kahama Mlanga, kwamba kwa sababu sasa tuna uhakika kwamba tutakuwa na flow nzuri ya kupata fedha, maana yake miradi hii sasa tutakuwa tuna uwezo wa kuipelekea fedha na kukamilika kama vile ambavyo imepangwa.
MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi ya mara ya pili. Suala hili la usajili ya Bodi ya Wajiolojia limeanza kushughulikiwa na Wizara tangu mwaka 2017 na limekuwa ni tatizo sugu sana kwa muda mrefu na viongozi mbalimbali wa Serikali ikiwemo Waziri Mkuu, Mawaziri mbalimbali wameweza kuhudhuria makongamano ya taasisi hii tunayotarajia kuisajili ya hawa wataalamu wa kijiolojia.
Mheshimiwa Spika, swali langu la msingi, sasa hivi kama Serikali tunaelekea kufanya utafiti nchi nzima kwa kurusha drone mbalimbali pamoja na njia nyingine za utafiti. Sasa Serikali imejipangaje kuhakikisha katika utafiti huo hatupati data za uongo kwa kuwa tunaenda kwenye utafiti tukiwa hatuna Bodi wa Wajiolojia ya kusimamia ubora wa taarifa hizo za kijiolojia pamoja na policy...
SPIKA: Mheshimiwa, twende kwenye swali.
MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Spika, kumekuwa na vishoka wengi sana mtaani wanaendelea kutapeli wachimbaji wadogo wakijiita wao ni wataalamu wa kijiolojia. Serikali imejipangaje kuthibiti hili tatizo kwa sababu tunaendelea na shughuli za madini, lakini hatuna bodi ambayo inasaidia kuondoa hili tatizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Luhende, Mbunge wa Bukene kwa sababu ya maswali yake kuhusu hii bodi ambayo imesubiriwa kwa muda mrefu. Pili, nitambue kwamba Jimbo lake la Bukene ni moja ya maeneo yetu ya madini ya dhahabu, kwani yanapatikana pia huko kwa wingi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la ubora wa data inayotafutwa katika tafiti zinazoendeshwa na Taifa hili kwa maelekezo ya mama, Mheshimiwa Dkt. Samia zinasimamiwa kwa umakini mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwajulisha Wabunge na Bunge lako Tukufu kwamba kati ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini kongwe na yenye uzoefu wa hali ya juu na wataalamu wanaojitosheleza ni Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania ijulikanayo kama GST. GST imeanzisha mwaka 1925 ina miaka 101 sasa na ndiye msimamizi mkuu wa tafiti hizi zinazokwenda kufanyika.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika tafiti yoyote kubwa inayokwenda kufanyika na inayofanyika, kunakuweko na mshauri mwelekezi mtaalamu anayetoka katika kampuni ya Kimataifa yenye uzoefu ambaye ndiye anayefanya kazi mbili za muhimu sana.
Mheshimiwa Spika, kazi ya kwanza, anafanya kitu kinachoitwa quality assurance kuhakikisha kwamba data inayokusanywa ina vigezo vyote vya ubora wote unaotakiwa, lakini pia anafanya quality control kuhakikisha kwamba data inayokusanywa imesimamiwa itoe majibu yanayotarajiwa. Isitoshe katika kuhakiki hiyo data na kuikamilisha Taasisi ya GST ndiye custodian, ndiye anayetunza data zote kwa ajili ya walaji wawekezaji wakubwa, na wawekezaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili la vishoka, ninaomba tena niseme hapa kwamba GST pamoja na STAMICO ambaye ndiye mlezi mkuu wa wachimbaji wadogo ambao ndio wanaumizwa sana na hawa vishoka, wana mandate na jukumu la kuwasimamia wachimbaji wadogo. Nitoe wito kwamba wasiwatumie wanajiolojia ambao hawajahakikiwa na GST kwa sasa wakati ambapo hatuna bodi.
Mheshimiwa Spika, kazi ya GST ni kutoa ushauri, ni kusaidia kupima sampuli, na pia ina watalaamu wanaoweza kutumiwa. Kwa hiyo, unapomchukua ambaye sio wa Serikali, pitia GST uliza kama huyu mtu anafaa?
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, kwa sababu hili suala lake ni la muhimu sana, ninaomba tu nitoe wito kwamba kwa kuwa bado bodi hii haijasajiliwa, na sisi pia tuko nyuma yao kuwasukuma wasajiliwe. Bodi hii itakaposajiliwa, kazi yao siyo kuhakiki data, wala ubora wa data, kazi yao ni kuwadhibiti wa jiosayansi ambao wamesajiliwa.
Mheshimiwa Spika, hiyo bodi wanapokwenda kufanya kazi yao, wawe na sifa, na Watanzania watakwenda kuwatumia hao sasa katika tafiti zao. Wakishasajiliwa, usimchukue mtu ambaye hajasajiliwa na bodi hii ambayo inakwenda kuanzishwa siku za karibuni. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Ninapenda kuuliza swali kwa Serikali, ni lini sasa mtaanza ujenzi wa soko pamoja na stendi katika Jimbo letu la Bukene? Maana jimbo hilo halina stendi pamoja na soko. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Bukene ni moja ya maeneo ambayo yana uhitaji wa stendi na soko. Mheshimiwa Mbunge katika kipindi hiki kifupi amekuwa anafuatilia mara kwa mara Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Bukene kwamba, hiyo ni dhamira na mpango wa Serikali kwenda kujenga miundombinu ya masoko na stendi katika maeneo yote yenye sifa hizo kwa awamu. Tutaendelea kutoa kipaumbele katika eneo la Bukene kwa kadiri tunavyopata fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninatumia nafasi hii kusisitiza kwamba, Wakurugenzi wetu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni lazima wawe na vipaumbele ambavyo ni mahitaji ya wananchi. Katika kila mipango yao ya bajeti ya kila mwaka wahakikishe angalau wana-reflect kwa kuanza kutenga kiasi kidogo cha fedha, kwa ajili ya shughuli hizo wakati Serikali ikiwa inatafuta fedha kwa ajili ya kumalizia miradi hiyo.