MHE. JOHN S. LUHENDE aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga skimu za umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha kisasa katika eneo la Kisasiga Jimbo la Bukene?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Tabora ikiwemo Jimbo la Bukene. Kwa mwaka 2025/2026, jumla ya miradi nane ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika Jimbo la Bukene inaendelea, ambapo utekelezaji wa miradi hiyo umefikia wastani wa asilimia 39.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo ni Kahamanhalanga, Mambali, Ikindwa, Malolo, Igombe, Lakuyi, Nindo na Sigili. Kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu, kutaiwezesha Serikali kujua gharama halisi kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji pamoja na kuimarisha miundombinu ya mashambani ili kuwezesha kufanyika kwa kilimo chenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika mwaka 2026/2027 imepanga kufanya tathmini katika eneo la Kisasiga kwa lengo la kubaini mahitaji halisi ya miundombinu ya umwagiliaji. Baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo, mradi huu utaingizwa katika mipango ya Serikali kwa ajili ya utekelezaji.
MHE. JOHN S. LUHENDE aliuliza:-
Je, lini usajili wa Bodi ya Wanajiolojia nchini utakamilika ili kulinda na kuongeza ufanisi katika shughuli za utafiti na uchimbaji madini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa John Stephano Luhende, Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na hatua za uanzishwaji wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Jiosayansi Tanzania (Tanzania Geoscientists Registration Board), kwa kifupi itajulikana kama (TGRB). Taratibu ambazo zimeshatekelezwa ni pamoja na uandaaji wa rasimu ya Waraka wa Mapendekezo ya Baraza la Mawaziri, kuhusu kuanzishwa kwa bodi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa, Wizara ya Madini ipo katika hatua ya ukusanyaji wa maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau kuhusu masuala mbalimbali likiwemo suala la kuainishwa kwa vyanzo vya mapato vitakavyohakikisha bodi pendekezwa inaweza kujiendesha.
Mheshimiwa Spika, baada ya zoezi la ukusanyaji na uchambuzi wa maoni kutoka kwa wadau kukamilika, Wizara itawasilisha waraka huo kwenye ngazi za maamuzi za Serikali ikiwa ni pamoja na ngazi ya kikao cha kitaalamu cha Makatibu Wakuu (IMTC) na kikao cha Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kujadiliwa na kupata ridhaa ya kuanzishwa rasmi kwa bodi hiyo kwa mujibu wa sheria. Ahsante sana.