Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Abubakar Alli Omari (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ABUBAKAR A. OMARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninakushukuru sana kwa kunipa fursa hii na kwa kuwa leo ndiyo ninasimama mara kwanza mbele ya Bunge lako Tukufu, ninaomba kwa idhini yako nizungumze mambo mawili matatu yafuatayo kabla sijaingia kwenye uchangiaji wa hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia afya na uwezo nimesimama hapa mbele ya Wabunge na mbele yako Mwenyekiti. Pili ninapenda kukishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuniteua kuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi. Tatu ninapenda kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Manonga kwa ujumla wao, walitupa kura za kutosha kwa wagombea wote wa CCM kuanzia Mwenyekiti ambaye ni Rais wetu, Mbunge na Madiwani wote 19. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kutoa pole kwa familia ya Mheshimiwa Sawawa, Diwani wa Kata ya Ziba, ambaye alifariki 1/1/2026 Mungu ailaze roho ya ndugu yetu mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijikita kwenye hotuba ya Waziri Mkuu hii ni hotuba ambayo inaakisi ile hotuba ya Rais na hapa Rais kwenye hotuba yake aliweka road map ya uchumi wetu tunataka tutoke wapi tuende wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hotuba inatakiwa iangaliwe kwa makini kwa sababu haiwalengi Watanzania tu, hii hotuba inalenga hata wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza katika nchi yetu, kwa hiyo ni lazima tuiangalie kwa makini na tuitafakari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hayo yote, nchi yetu ni kubwa sana na maendeleo yamekuwa yapo tofauti tofauti katika kila sehemu. Ili sehemu zote ziwe kwenye safari ya kuelekea kwenye pato lile la Taifa la dola 7,000 kwa kila mtu. Kwa mfano, sasa hivi kwa ripoti ya mwaka jana tu 2025/2026 ambayo ilitolewa na Benki Kuu, pato la mtu mmoja kwa Mkoa wa Tabora ni shilingi 6,000. Statistics ambazo zimetolewa na Idara ya Takwimu (National Bureau of Standards) inaonesha kila mtanzania mmoja ana watu watano wanaomtegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia pale watu kipato cha mtu mmoja ni shilingi 6,000 ukigawanya kwa watu watano inakuja kwenye 1,000 na kitu. Sasa tuna safari ndefu sana kutoka hapo kwenye 1,000 mpaka Mtanzania apate dola 7,000 na leo tunavyozungumza ile dira yetu ya miaka 25 tayari mwaka mmoja umeshapita, tunatakiwa tufanye kazi kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Rais yeye ameshanyoosha njia, kaonyesha barabara tunatakiwa tupite hapa ni jukumu letu sasa tuliobakia hapa kila mtu kivyake. Waheshimiwa Wabunge na Mawaziri lets do our best, tuna kazi ndefu sana siyo masihara. Hapa tunasikia Wabunge wote wanalalamikia masuala ya pesa, sasa mimi kama mtu wa kodi, mwenye asili ya kodi na jambo ambalo kwa ajili ya muda nitakwenda nalo haraka tu tuweze kwenda pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maeneo ambayo yako nyuma kwa mfano Jimbo langu la Manonga, liko nyuma kweli na kwa sababu ya vichocheo vya uchumi havipo hasa barabara, tuna Barabara moja kuu inatoka Choma – Ziba – Nkinga mpaka Puge, Jimbo zima kwa ujumla halina lami hata moja hata kilometa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninashukuru kwamba Awamu ya Sita pesa zimeletwa kuanzia ile awamu ya kwanza, katika awamu ya sita na sasa hivi na tunakokwenda tunaenda kuona barabara ya lami inaenda kujengwa. Nimshukuru sana Waziri, Naibu Waziri wa Ujenzi tumesumbuana sana, nimemsumbua sana lakini hatimaye tumepata kilometa kadhaa kuanzia Ziba kwenda Nkinga na kuanzia Puge kwenda Ndala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe tu pale atuongezee angalau kwa awamu ya kwanza hizo kilometa zifike Nkinga na za huku zitoke mpaka Puge mpaka Ndala. Hiyo itakuwa imetusaidia kabisa, kwa sababu hizo Hospitali zote za Ndala na Nkinga ni hospitali kubwa, ile Nkinga ni Hospitali ya Rufaa ambayo ndiyo wananchi wote wa Mkoa wa Tabora na mikoa ya jirani wanaitegemea hiyo hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ninataka kulizungumzia ni masuala ya barabara hizi zingine za mtaa. Tunaomba hii Barabara ya kutokea Nsimbo – Igoweko mpaka Mabeshi ipandishwe daraja iwe barabara ya TANROADS na pale tuna madaraja mawili tu katika Mto Roya. Mbunge mwenzangu, jirani yangu kaelezea, hiyo ni barabara muhimu sana kwa Jimbo la Manonga ili tuweze kufungua uchumi wa wananchi wa Manonga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara zingine za huko na zenyewe pia zina umuhimu, hivi ninavyozungumza hakuna mawasiliano kati ya Mwisi na Mizanza na kuna Barabara nyingine ya kutoka Chibiso kwenda Choma, hizo barabara zipo katika hali mbaya na nyingine ni ya kutokea Nyandekwa kupitia Ntigu mpaka Ulaya, kwa hiyo tumeona kama mahitaji ni mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye suala la maji, hili suala la maji kwenye Jimbo langu la Manonga limekuwa kitendawili. Juzi niliomba kuonana na Waziri wa Maji akanipa appointment bahati mbaya nimeenda ofisini kwake sikumkuta. Tuna Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria. Maji ya Ziwa Victoria yamefika mpaka Jimboni kwetu, huo mradi umeenda mpaka Choma, Choma umetumia zaidi ya milioni 400, lakini mpaka sasa hivi ninavyokueleza shida ya maji kule bado iko vilevile, hivyo, tunahitaji maji. Pia huwa kuna Mradi huo wa Maji ya Ziwa Victoria yanatakiwa yatoke Nkinga Hospitali kupitia Mwisi – Chabutwa mpaka Nsimbo. Huo mradi ulikuwa ukamilike mwaka jana lakini mpaka leo huo mradi umesimama sijaelewa na sijui tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masuala ya kilimo tunaishukuru Serikali imeweka pesa za kujenga bwawa la umwagiliaji kule maeneo ya Choma. Masuala ya elimu pia tumepata vya kutosha, afya na michezo. Sisi tunayo shule moja ya Sekondari ya Ziba hiyo imeanzisha timu ya watoto wasichana na sasa hivi inaenda kucheza ligi daraja la kwanza. Ninamwomba Waziri Makonda aje naye atie nguvu yake kwenye suala hilo. Hii ni timu ya Kata pekee Tanzania hii ambayo inacheza ligi ya Taifa tena ya wasichana na hiyo timu ya wasichana imeshatoa wachezaji wanne kwenda timu ya Taifa. Kwa hiyo hilo jambo na lenyewe linatakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuje sasa kwenye suala zima la uchumi wa nchi hii. Ndugu zangu mimi kama nilivyosema ni mtoza kodi, uchumi wa nchi hii unahitaji kwa kweli kutizamwa kwa jicho la tatu, lazima mifumo yetu na sera zetu za kodi ziwe zinatabirika na zenye kukaa muda mrefu. Tumesema ili tufikie maendeleo ya 2050 tunahitaji wawekezaji ambao watakuja kusukuma hapa, bila kuwa na sheria za kodi ambazo zinatabirika itakuwa ni shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwa haraka haraka ni tunatakiwa ili tupate maendeleo ya kweli, lazima tukusanye kodi vizuri kila shilingi inayotakiwa ikusanywe ikusanywe na matumizi yawe mazuri, ndiyo tutapata maendeleo. Sasa kwenye suala la kodi Rais alizungumza kuhusu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Abubakar, muda wako umekwisha.

MHE. ABUBAKAR A. OMARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa ninamalizia dakika moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kodi inabidi tunapo-tax madini yetu sasa hivi hayatupi tija sana, kwa sababu ya muda, nilitaka nieleze hapa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa utakuwa na muda mwingi, tunayo bajeti ya Wizara ya Fedha, tuna Bajeti Kuu, zote ni kodi tupu kwa hiyo utapata muda mwingi tu.

MHE. ABUBAKAR A. OMARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache ninaomba, kwa niaba ya wananchi wa Manonga baada ya kutoa haya, nina imani kabisa Waziri Mkuu katika majumuisho yake ataangalia haya tuliyosema Wabunge kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja kwa niaba ya wananchi ya Manonga. Ahsante sana. (Makofi)