Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Musa Godfrey Mbuga (1 total)

MHE. MUSA G. MBUGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi hii. Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali imefanya kazi kubwa sana ya kuunganisha barabara zinazounganisha mikoa kwa kiwango cha lami. Sambamba na kazi kubwa hiyo iliyofanywa na Serikali, bado ipo mikoa michache ambayo haijaunganishwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, je, ni upi mpango wa Serikali kuhakikisha hizi barabara chache zinazounganisha mikoa zinatengenezwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa uchumi? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Musa Mbuga, Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mkoa wa Simiyu, kwa swali zuri na ambalo linagusa moja kwa moja masuala yanayochochea ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa awamu zote za Serikali ya Tanzania zimewekeza nguvu kubwa katika kutengeneza miundombinu ikiwemo barabara na madaraja ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa pamoja na watu kutoka eneo moja kwenda eneo lingine.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita imefanya jitihada kubwa za kuweza kuhakikisha kwamba mikoa ambayo haijaunganishwa kwa barabara za lami inaunganishwa ili kuhakikisha kwamba mawasiliano pamoja na biashara katika mikoa hiyo inafanyika. Hadi sasa tuna mikoa michache ambayo bado kazi hiyo haijakamilika.

Mheshimiwa Spika, ninatambua kutoka Katavi kwenda Rukwa kulikuwa bado na eneo ambalo halijaunganishwa kwa kiwango cha lami, lakini hadi tunavyoongea, mkandarasi yuko site kwa ajili ya kuunganisha Mkoa wa Rukwa na Katavi. Kadhalika kutoka Mkoa wa Katavi kwenda Kigoma kulikuwa na sehemu ambayo haijaunganishwa kwa kiwango cha lami fedha.

Mheshimiwa Spika, kazi ya kuunganisha Mkoa wa Katavi kwenda Kigoma kwa sehemu ambayo ilikuwa bado haijapata mkandarasi, zoezi hilo litakamilika. Sehemu ambazo ziko na wakandarasi, kazi inaendelea kuhakikisha kwamba huko na kwenyewe kunaunganishwa. Kutoka Katavi kwenda Tabora imebaki sehemu za umaliziaji, kwani kazi kubwa imeshakamilika. Ni umaliziaji tu, barabara yote hiyo inakuwa ya lami sasa.

Mheshimiwa Spika, muuliza swali ninajua kiu yake kubwa ni barabara ambayo inaunganisha sasa Mkoa wa Singida kupitia Mkalama, Daraja la Sibiti kwenda mpaka Meatu na baadaye kutawanyika kwenda Maswa na kwenda Bariadi na mpaka kuunganisha na Mkoa wa Mara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki kitakuwa ni moja ya kipaumbele kitakachofuata baada tu ya kuwa tumeshamaliza hili zoezi ambalo tulikubaliana Waheshimiwa Wabunge kwamba tumalizie barabara ambazo wakandarasi walikuwa wameshapunguza kasi ya utekelezaji, lakini pia tumalizie barabara ambazo zilishasainiwa mikataba ila walikuwa bado hawajapata malipo ya awali.

Mheshimiwa Spika, tutaenda kwenye barabara ambazo ni za kipaumbele katika maeneo yetu, na Waheshimiwa Wabunge wote mlishaainisha barabara pamoja na miradi ambayo ni ya kipaumbele katika maeneo yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, punde tutakapokuwa tumemaliza miradi ambayo ilikuwa inaendelea, ambayo kazi yake ilipungua kidogo na miradi ambayo mikataba ilishasainiwa ila wakandarasi walikuwa bado hawajapata malipo ya awali, tutakwenda kwenye barabara ambazo ni za kipaumbele ikiwemo hii ya kutokea Singida - Sibiti - Meatu kwenda mpaka Maswa na Bariadi hadi Mara; tuna barabara kama hii ya kutokea Mbeya kuja Chunya kwenda mpaka Itigi mpaka Mkiwa; tunayo barabara ya kutoka Handeni kwenda Kiteto - Kondoa - Kwamtoro mpaka Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna barabara ya kutoka Makete kwenda Mbeya na barabara nyingine nyingi ambazo Waheshimiwa Wabunge maeneo yote walishayaainisha zitakwenda kuwa kipaumbele kitakachofuata tu mara tutakapokuwa tumemaliza kufanya miradi ambayo ilikuwa imesimama simama iendelee na miradi ambayo ilishasainiwa mikataba ambayo ilikuwa bado haijaanza kufanya kazi malipo ya awali yatoke miradi yote ilendelee. Then, tutakwenda kwenye miradi hiyo iliyo ya kipaumbele ili kutekeleza sera hiyo ya kuunganisha mikoa na nchi jirani kwa kiwango cha lami. (Makofi)